Author: Honest Mwanitega

MASHUJAA YAANZA LIGI KUU KISHUJAA.

TIMU ya Mashujaa ya Kigoma iliyopanda Ligi Kuu ya NBC ikitokea Ligi ya championship imeanza kibabe baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Mashujaa ilipata mabao yake kupitia kwa Adam Adam dakika ya 15 na Othman Dunia dakika ya 73 kwa mashuti yaliyopigwa kwa mguu wa kushoto.

Timu ya Kagera imepoteza mchezo wa kwanza wa ligi kwa misimu miwili mfululizo baada ya kupoteza pia kwa Azam ya Dar msimu uliopita kwa mabao 2-1.

Mchezo wa pili siku ya leo haukuweza kuendelea na kumalizwa dakika ya 18 baada ya wachezaji wawili wa Kitayosce kuumia na kusalia sita pekee ambao kikanuni hawaruhusiwi kuendelea na mchezo.

Hadi mchezo huo unamalizwa Azam ilikuwa inaongoza kwa mabao 4-0 yaliyofungwa na Prince Dube na Feisal Salum ‘Feitoto’ aliyefunga mabao matatu ‘Hat-trick’.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea kesho kwa mchezo mmoja utakaokutanisha timu za Mtibwa Sugar na Simba utakaochezwa uwanja wa Manungu, Morogoro.

PAZIA LA LIGI KUU YA NBC LAFUNGULIWA

Baada ya siku 76 kupita Ligi Kuu ya NBC imerejea tena kwa michezo mitatu iliyochezwa viwanja vya mikoa mitatu tofauti na kushuhudia mabao matano yakifungwa kwa ujumla.

Elias Maguli amekuwa ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao katika msimu huu wa 2023/24 na kuifanya timu ya Geita Gold kupata ushindi wa bao 1-0 ikiwa ugenini dhidi ya Ihefu kwenye uwanja wa Highland Estates, Mbeya.

JKT Tanzania mabingwa wa Ligi ya Championship msimu uliopita wameanza vyema ugenini kwa kupata alama tatu dhidi ya Namungo kwa ushindi wa bao moja lililofungwa na Martin Kigi kwenye uwanja wa Majaliwa, Lindi.

Dodoma Jiji imefanikiwa kuwa timu pekee iliyopata ushindi leo ikiwa nyumbani baada ya kushinda mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union yaliyofungwa na Raizin Hafidh na Meshack Abraham huku Haji Ugando akiifungia Coastal .

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa michezo miwili kati ya Mashujaa iliyopanda daraja na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma na Azam itakuwa mwenyeji wa Kitayosce iliyopanda daraja kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar.

‘KIVUMBI’ CHA LIGI KUU YA NBC KUANZA LEO.

PAZIA la Ligi kuu ya NBC msimu wa 2023/2024 linafunguliwa rasmi leo Agosti 15 kwa michezo mitatu kuchezwa katika viwanja mbalimbali.

Mchezo wa kwanza wa ufunguzi utazikutanisha Ihefu dhidi ya Geita Gold saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Highland Estate, Mbeya mchezo wa pili utazikutanisha Namungo dhidi ya JKT Tanzania saa 12:30 usiku katika Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Mkoani Lindi na mchezo wa mwisho ni kati ya Dodoma Jiji na Coastal Union saa 3:00 usiku uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Msimu huu mpya wa Ligi Kuu ya NBC unashirikisha jumla ya timu 16 zitacheza jumla ya michezo 30 ‘kila moja’ uwanja wa nyumbani na ugenini na kufanya jumla ya michezo 240 sawa na michezo 120 nyumbani na 120 ugenini kwa timu zote

SIMBA BINGWA MPYA WA NGAO YA JAMII.

Baada ya timu ya Yanga kutwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii kwa miaka miwili mfululizo hatimaye timu ya Simba Leo Agosti 13, 2023 imefanikiwa kushinda mchezo wa fainali na kutwaa ubingwa huo.

Simba wametwaa ubingwa huo kwa kuifunga Yanga Kwa mikwaju ya penati 3-1 ikiwa ni baada ya mchezo huo kumalizika kwa suluhu ndani ya dakika 90.

Golikipa wa Simba Ali Salim ndiye aliyeibuka shujaa wa mchezo baada ya kuokoa penati tatu na kuisaidia timu yake kutwaa ubingwa huo.

Baada ya mchezo huu Ligi Kuu ya NBC inatarajiwa kuanza Agosti 15 kwa michezo kati ya Ihefu na Geita Gold, Namungo na JKT Tanzania, na Dodoma dhidi ya Coastal Union.

NI KARIAKOO ‘DERBY’ FAINALI NGAO YA JAMII.

TIMU ya Simba imefanikiwa kufuzu fainali ya Ngao ya Jamii kwa ushindi wa penati 4-2 dhidi ya Singida Big Stars baada ya kumalizika kwa suluhu ndani ya dakika 90.

Simba itakutana na Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii kwa mara ya tatu mfululizo huku ikiwa imefungwa katika mara zote mbili zilizopita.

Penati zilizofungwa na Luis Miquisone, Saidi Ntibazonkinza, Mzamiru Yassin na Moses Phiri zilitosha kuipeleka Simba fainali na kuifanya Singida kukutana na Azam katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu.

Shindano hilo litatamatika Agosti 13 kwa mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kati ya Azam na Singida huku mchezo wa mwisho ukiwa kati ya Simba na Yanga kutafuta bingwa wa Ngao ya Jamii msimu wa 2023/24.