Author: Honest Mwanitega

Ratiba ya Ligi Kuu ya NBC 2025/2026

VIWANJA NANE KAZINI LEO LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC inatimua ‘vumbi’ leo kwenye viwanja nane tofauti ikiwa ni michezo ya kukamilisha mzunguko wa 30 wa ligi hiyo msimu wa 2024/25.

Macho na masikio yatakuwa zaidi kwa ‘Vigogo’ wa ligi hiyo timu za Yanga na Simba zilizopishana alama moja pekee huku timu hizo zikiwa nyumbani kwenye michezo yao ya leo.

Young Africans inayoongoza ligi hiyo itakuwa nyumbani kwenye uwanja wa New Amaan, Zanzibar kuwaalika Dodoma Jiji ya Dodoma huku ‘watani’ zao Simba wakiwa uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kuwaalika Kagera Sugar iliyoshuka daraja hadi sasa.

‘Maafande’ wa timu ya Mashujaa watakuwa nyumbani kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma kuwaalika wenzao wa JKT Tanzania huku timu ya Pamba Jiji ya halmashauri ya Jiji la Mwanza ikiwa mwenyeji wa KMC inayomilikiwa na manispaa ya Kinondoni kwenye uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Singida Black Stars itakuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Liti, Singida kuwakaribisha Tanzania Prisons ya Mbeya inayopambana kujitoa kwenye nafasi ya kucheza hatua ya mtoano huku Ken Gold ikiwa ugenini kwenye uwanja wa Majaliwa, Lindi kurusha ‘karata’ yake ya mwisho ya Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Namungo baada ya kushuka daraja msimu huu ikiwa timu ya mwisho kwenye msimamo wa ligi hiyo.

‘Matajiri wa Chamazi’ timu ya Azam FC baada ya kuichapa Tabora United mabao 5-0 nyumbani, itakuwa ugenini leo kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa dhidi ya Fountain Gate na mchezo wa mwisho utakuwa kati ya Coastal Union ambayo haijapoteza mchezo tangu kurejea kwenye uwanja wake wa Mkwakwani ikiikaribisha Tabora United.

Michezo yote itapigwa kuanzia saa 10:00 alasiri na kurushwa mbashara kwenye stesheni za Azam.

COASTAL UNION YAGEUZA MKWAKWANI ‘MACHINJIONI’ LIGI KUU YA NBC.

‘WAGOSI wa kaya’ timu ya Coastal Union imefanikiwa kupanda ushindi wa tatu mfululizo kwenye uwanja wake wa Mkwakwani tangu kukamilika marekebisho yake baada ya kuifunga timu ya Fountain Gate 1-0.

Lucas Kikoti ndiye aliyepeleka furaha kwa wakazi wa mkoa wa Tanga akifunga kwa mkwaju wa penati uliopatikana kipindi cha pili.

Tangu uwanja huo urejeshwe kwenye matumizi Coastal imezifunga timu za Singida Black Stars kwa mabao 2-1, Ken Gold 2-1 na ushindi wa jana unakamilisha mchezo wa tatu mfululizo wakitumia uwanja huo wakiwa hawajapoteza wala kutoa sare.

Coastal imefikisha alama 34 na kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26 huku ikisalia na mchezo mmoja kukamilisha msimu.

Bakari Msimu wa Coastal Union aliibuka mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kuonyesha kiwango bora zaidi ya wachezaji wenzake.

‘MAAFANDE’ WASHINDWA KUTAMBA KWA ‘WANANCHI’ LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Tanzania Prisons imeshindwa kuonyesha ubabe ikicheza uwanja wa nyumbani wa Sokoine, Mbeya baada ya kukubali kipigo cha mabao 0-5 kutoka kwa Young Africans.

Ilimchukua dakika 31 Mudathir Yahya kuiandikia Young Africans bao la kuongoza kabla ya dakika tatu baadae Clatous Chama kuongeza msumari wa pili na kuwafanya ‘Wananchi’ kwenda mapumziko wakiongoza mabao 0-2.

Dakika 11 baada ya kipindi cha pili kuanza Pacome Zouzoua aliongeza ‘chuma’ cha tatu huku dakika nne baadae Israel Mwenda akaongeza la nne kwa kichwa baada ya kuunganisha mpira wa krosi ya Chadrack Boka na dakika ya 75 Pacome aliingia kambani tena na kukamilisha karamu ya mabao kwa Young Africans.

‘Wananchi’ wameendelea kujikita kileleni baada ya ushindi huo wakifikisha alama 76 huku wakiwa wamefunga mabao 76 wakifuatiwa na timu ya Simba yenye alama 75 wakifunga mabao 68 huku timu hizo zikisalia na michezo miwili kutamatisha msimu wa Ligi Kuu ya NBC.

Pacome Zouzoua aliibuka nyota wa mchezo na kukabidhiwa tuzo ya mchezaji bora wa mechi akifunga mabao mawili na kuisaidia timu yake kupata alama tatu.

PAZIA LA NBC CHAMPIONSHIP KUFUNGWA LEO.

KILELE cha ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2024/25 kinatarajiwa kufikiwa leo kwa mchezo wa kukabidhi ubingwa kati ya Mtibwa Sugar na Mbeya City utakaopigwa leo kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam saa 2:00 usiku.

Ligi hiyo ilifika tamati Mei 11, kwa michezo nane kupigwa na Mtibwa Sugar kumaliza bingwa na kupanda daraja akifikisha jumla ya alama 71 huku Mbeya City ikimaliza nafasi ya pili na kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26 sambamba na Mtibwa.

Mtibwa Sugar imerejea Ligi Kuu ya NBC ikiwa ni msimu mmoja pekee tangu kushuka daraja huku Mbeya City ikitumia misimu miwili kurejea ligi hiyo.

Mchezo wa leo utarushwa mubashara TV3 na utakuwa sambamba na sherehe za kukabidhi ubingwa kwa timu ya Mtibwa Sugar baada ya kumaliza nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi ya Championship ya NBC.

TABORA, KMC KUFUNGA MZUNGUKO WA 28 LIGI KUU YA NBC.

MZUNGUKO wa 28 unatarajiwa kukamilika leo kwa mchezo mmoja utakaozikutanisha timu za Tabora United kutoka mkoani Tabora dhidi ya KMC ya Dar es Salaam saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

KMC itashuka ugenini ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wake uliopita dhidi ya Simba kwa mabao 1-2 kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Hadi sasa ikicheza viwanja vya ugenini KMC imeshinda mchezo mmoja pekee, kufungwa michezo saba huku ikitoka sare minne na kukusanya alama saba pekee.

Tabora inashuka uwanjani ikiwa haijafanikiwa kupata ushindi kwenye michezo mitano mfululizo ya Ligi Kuu ya NBC na mara ya mwisho kushinda ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji kwa bao moja lililofungwa na Offen Chikola kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.