Author: Honest Mwanitega

WAMECHEZA DAKIKA NYINGI NBC CHAMPIONSHIP.

UKISALIA mchezo mmoja pekee Ligi ya Championship ya NBC kutamatika Mchezaji wa Mtibwa Sugar Oscar Masai anashikilia rekodi ya kucheza dakika nyingi zaidi kwenye ligi hiyo hadi sasa.

Oscar amecheza dakika 2627 hadi sasa huku akiwa ameisaidia Mtibwa kurejea kwenye Ligi Kuu ya NBC na endapo timu yake itashinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya Kiluvya itakuwa bingwa mpya wa Ligi ya Championship ya NBC.

Andrew William wa Stand United ya Shinyanga anashika nafasi ya pili kwa kucheza dakika nyingi akiwa nazo 2614 huku timu yake ikiwa nafasi ya tatu ya msimamo na ikitarajiwa kuchezo michezo ya mtoano kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26.

Evart Joseph wa African Sports ya Tanga anashika nafasi ya tatu akiwa na dakika 2580 huku timu yake ikishika nafasi ya 15 ikiwa kwenye mstari wa kushuka daraja na endapo African Sports itapoteza mchezo wake wa mwisho dhidi ya Transit Camp nyumbani itakuwa imeshuka daraja rasmi na kushiriki Ligi ya First League msimu wa 2025/26.

ISAMUHYO CHANGAMOTO KWA ‘VIGOGO’ LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC inatarajiwa kutimua vumbi leo Mei 5, kwa mchezo mmoja kati ya JKT Tanzania na Simba utakaopigwa kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam huku uwanja huo ukiwa sehemu ngumu kupata matokeo ya ushindi kwa timu kubwa za Ligi Kuu ya NBC.

JKT yenye ‘maskani’ yake Mbweni, Dar es Salaam imecheza uwanja wake wa nyumbani dhidi ya Young Africans na Azam bila kupoteza mchezo kwenye msimu huu wa 2024/25.

Michezo yote miwili dhidi ya timu hizo JKT haijaruhusu bao lolote kwani michezo hiyo ilimalizika kwa suluhu huku golikipa wa timu hiyo Yakoub Suleiman akimaliza michezo hiyo kwa kukusanya (hati safi) mbili.

JKT leo itakuwa mwenyeji wa ‘Kigogo’ mwingine wa Ligi Kuu ya NBC aliyefanikiwa kufuzu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika timu ya Simba kwenye uwanja huo wa Meja Jenerali Isamuhyo katika mchezo utakaopigwa saa 10:00 alasiri.

SIMBA YATINGA FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA.

MWAKILISHI pekee wa Ligi Kuu ya NBC kimataifa timu ya Simba imefanikiwa kutinga fainali baada ya kuiondoa timu ya Stellenbosch kutoka Afrika Kusini kwa matokeo ya jumla kwa bao 1-0.

Simba imelazimisha suluhu ugenini kwenye uwanja wa Moses Mabhida na kufanikiwa kufuzu baada ya faida ya ushindi wa 1-0 iliyopata kwenye mchezo wa nyumbani uliopigwa uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Simba imefanikiwa kutinga fainali hiyo ya kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza kwenye historia huku ikiwa timu ya pili kutoka kwenye Ligi Kuu ya NBC kufuzu fainali hiyo ndani ya miaka mitatu ikiungana na Young Africans iliyofanya hivyo mwaka 2023.

Simba itakutana na RS Berkane ya Morocco kwenye fainali hiyo iliyofuzu baada ya kuifunga CS Constantine ya Algeria kwa ushindi wa jumla kwa mabao 4-1.

Simba itaanzia ugenini Morocco Mei 17 huku mchezo wa pili na wa mwisho katika shindano hilo ukitarajiwa kupigwa Mei 25 kwenye uwanja wa Mkapa, Dar.

MZIZE NI MOTO WA KUOTEA MBALI LIGI KUU YA NBC.

MCHEZAJI wa Young Africans raia wa Tanzania Clement Mzize ameendelea kuwa ‘Mwiba’ kwa mabeki wa timu pinzani baada ya kufanikiwa kufunga jumla ya mabao 13 hadi sasa kwenye Ligi Kuu ya NBC.

Mzize amefunga idadi hiyo ya mabao huku timu yake ikisalia na michezo minne kutamatika kwa msimu wa 2024/25.

Prince Dube wa Young Africans na Jean Ahoua wa Simba wanafuata nyuma ya Mzize wakifunga mabao 12 kila mmoja huku Ahoua akifunga mikwaju ya penati mitano hadi sasa na kuwa kinara wa kufunga mabao kwa penati.

Jonathan Sowah anafuatia akifunga jumla ya mabao 11 huku akiwa amecheza michezo tisa pekee baada ya kujiunga na timu yake kwenye dirisha dogo la usajili.

Elvis Rupia wa timu ya singida Black Stars anafuata nyuma ya mshambuliaji mwenzake wa timu ya Singida Jonaathan Sowah akiwa na mabao kumi.

KENGOLD YAAGA RASMI LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya KenGold imekuwa timu ya kwanza kuaga Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/25 na kushuka daraja baada ya kupoteza jana kwa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

KenGold iliyokuwa bingwa wa Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2023/24 na kufanikiwa kupanda ligi kuu imedumu kwa msimu mmoja pekee na kurejea tena kwenye ligi ya Championship.

Hadi sasa mabingwa hao waliopita wa Championship wameshinda michezo mitatu pekee ya Ligi Kuu ya NBC wakifungwa 17, huku wakitoka sare michezo saba na kukusanya alama 16 pekee huku ikisalia michezo mitatu kukamilika kwa msimu.

KenGold hadi sasa imeruhusu mabao 50 na kufunga 22 huku ikiwa timu ya pili kuruhusu mabao mengi nyuma ya Fountain Gate ya Manyara iliyofungwa mabao 51 hadi sasa.