Author: Loveness Bernard

VIWANJA VIWILI KUWAKA MOTO LIGI KUU YA NBC LEO.

LIGI Kuu ya NBC leo itaendelea mkoani Dar es Salaam katika viwanja viwili ambapo timu ya Simba itakuwa mwenyeji wa Mashujaa katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo majira ya saa 10:00 alasiri huku timu ya Azam ikiwaalika TRA katika uwanja wa Azam Complex Chamazi saa 1:00 usiku.

Simba ipo nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imecheza michezo sita, ikishinda michezo minne, sare moja na kufungwa mchezo mmoja huku ikikusanya alama 13.

Mchezaji wa Azam, Zidane Sereri

Mashujaa ipo nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikicheza michezo 10, ikishinda michezo mitatu, sare nne na kufungwa michezo mitatu huku ikikusanya alama 13.

Kwa upande wa timu ya Azam imecheza michezo saba hadi sasa bila kupoteza ikishinda michezo mitatu na sare nne na kufanikiwa kukusanya alama 13 katika michezo hiyo.

Timu ya TRA United ipo nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imecheza michezo nane, ikishinda michezo mitatu, sare tatu na kufungwa michezo miwili huku ikikusanya alama 12.

DUKE,PEDRO WANG’ARA TUZO ZA DISEMBA

MCHEZAJI Duke Abuya wa Klabu ya Young Africans, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Disemba wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2025/26, huku Pedro Goncalves pia wa Young Africans akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa Ligi hiyo kwa mwezi huo.

Duke alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiisaidia timu yake kushinda michezo miwili iliyocheza mwezi huo, pamoja na kuhusika katika mabao mawili kwa dakika 180 za michezo hiyo.

Mchezaji huyo aliwashinda Nassor Saadun wa Azam na Prince Dube wa Young Africans alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa upande wa Pedro aliyeingia fainali katika mchakato huo na Florent Ibenge wa Azam na Etienne Ndairagije wa TRA United, aliiongoza timu yake kushinda michezo miwili na kupaa kutoka nafasi ya nne hadi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo. Young Africans ilizifunga Fountain Gate (2-0), na Coastal Union (0-1).

Wakati huohuo Meneja wa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Said Mpuche, amechaguliwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Disemba kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

Mchezaji wa Transit Camp Adam Uledi

Katika hatua nyingine mchezaji wa Transit Camp, Adam Uledi, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Disemba wa Ligi ya Championship ya NBC 2025/26, huku Shadrack Nsajigwa pia wa Transit Camp akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Uledi aliyeingia fainali katika mchakato huo na Obrey Chirwa wa Kagera Sugar na Boniface Mwanjonde wa Mbeya Kwanza, alionesha kiwango chenye mwendelezo ikiwa ni pamoja na kucheza dakika 450 za michezo mitano aliyocheza.

Kwa upande wa Nsajigwa aliyeingia fainali na Juma Kaseja wa Kagera Sugar na Zuberi Katwila wa Geita Gold aliiwezesha timu yake kushinda michezo yote mitano iliyocheza mwezi huo.

DODOMA JIJI, PRISONS KUUMANA LEO LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Dodoma Jiji itaikaribisha Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaochezwa leo majira ya saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Mchezo huo ni muhimu kwa timu zote mbili kwani zinapambana kujinasua ‘mkiani’ Dodoma Jiji ikiwa nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kucheza michezo tisa ikishinda mchezo mmoja ,kupata sare minne na kufungwa michezo mitano .

Mchezaji wa Dodoma Jiji Mwana Kibuta

Aidha Dodoma Jiji imeruhusu mabao 10 huku ikifunga mabao matano na kuweza kukusanya alama saba katika michezo hiyo.

Kwa upande wa Tanzania Prisons inashika nafasi 14 katika msimamo ikiwa imecheza michezo saba, ikishinda michezo miwili, sare mbili na kufungwa michezo minne.

Kwa upande wa alama timu hiyo imefanikiwa kukusanya alama saba, ikifunga mabao matatu na kufungwa mabao matano katika michezo hiyo.

PRISONS WABABE WA MBEYA DABI LIGI KUU YA NBC

Mchezaji wa Mbeya City (kushoto) akichuana na mchezaji wa Tanzania Prisons

TIMU ya Tanzania Prisons imeendeleza ubabe wake katika mchezo wa dabi ya Jiji la Mbeya baada ya kuifunga timu ya Mbeya City mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa Uwanja wa KMC mkoani Dar es Salaam jana Oktoba 21.

Mchezo huo ulianza majira ya saa 10:00 alasiri ambapo timu zote zilikuwa zikipambana kupata alama tatu huku mashabiki wa timu zote mbili wakionekana kushangilia kwa bendi na ngoma zilizonogesha mchezo huo.

Mbeya City kinara wa Ligi Kuu ya NBC alianza mchezo kwa kushambulia sana lango la ‘hasimu’ wake huku Tanzania Prisons ikifanya mashambulizi ya kushtukiza na hadi timu zinaenda mapumzikoni hakuna aliyekuwa ametikisa ‘nyavu’ za mwenzake hivyo kuwapa kazi ya ziada makocha wakati wa mapumziko namna bora ya kujipanga kwa ajili ya kipindi cha pili.

Dakika ya 73 kipindi cha pili Tanzania Prisons ilipata bao la kwanza kupitia kwa Jeremiah Juma na dakika moja baadae Haruni Chanongo aliiongezea bao la pili na kufifisha matumaini ya Mbeya City kubakiza alama zote tatu nyumbani.

Tanzania Prisons wakishangilia

Dakika ya 87 Mbeya City ilipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Daniel Lukandamila hivyo mchezo kutamatika kwa Mbeya City kupoteza 1-2 na kuifanya ‘Purple Nation’ kupoteza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu.

Mchezaji wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo kutokana na kiwango kizuri alichokionyesha ikiwa ni pamoja na kuwafungia ‘Wajelajela’ bao na kuonyesha kiwango kizuri akiisaidia timu yake kushinda.

Jeremiah Juma

Matokeo hayo yanaifanya Tanzania Prisons kupanda hadi nafasi ya tano ikiwa na alama sita huku Mbeya City ikiendelea kushikilia ‘usukani’ wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na alama saba.

DIARRA,AHMAD WANG’ARA TUZO ZA SEPTEMBA.

GOLIKIPA wa timu ya Young Africans, Djigui Diarra ameng’ara baada ya kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu ya  NBC msimu wa mwaka 2025/2026, huku Ahmad Ali wa JKT Tanzania, akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.

Diarra alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Anthony Tra Bi wa Singida Black Stars na Mohamed Bakari wa JKT Tanzania alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo miwili ambayo Young Africans ilicheza na kupata ushindi kwa mchezo mmoja dhidi ya Pamba Jiji (3-0) na kupata suluhu ya (0-0) dhidi ya Mbeya City hivyo kutokuruhusu goli kufungwa kwa timu yake.

KOCHA AHMAD ALI

Kwa upande wa Ahmad Ali aliyeingia fainali na Romain Folz wa Young Africans na Miguel Gamondi wa Singida Black Stars, aliiongoza JKT Tanzania kwenye kiwango kizuri katika michezo miwili iliyocheza kwa mwezi huo wa Septemba.

JKT Tanzania ilipata sare ya bao moja dhidi ya Mashujaa wakiwa ugenini, uwanja wa Lake Tanganyika – Kigoma na kupata ushindi wa mabao mawili dhidi ya Coastal Union (1-2) wakiwa kwenye uwanja wa ugenini,Mkwakwani – Tanga