Author: Yahaya Abushehe

YANGA BINGWA LIGI KUU YA NBC.

 

USHINDI wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar umeipa timu ya Yanga ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2023/2024 baada ya kufikisha jumla ya alama 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yeyote .

Huu ni ubingwa wa tatu mfululizo wa Ligi Kuu ya NBC kwa Young Africans tangu msimu wa 2021/2022 hadi msimu huu wa 2023/2024.

Vita ya nafasi ya pili ndio inayoendelea kwasasa Kati ya Azam FC na Simba SC zikiwania kuungana na Yanga kwenye uwakilishi katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Azam ipo nafasi ya pili ikiwa na alama 60 baada ya michezo 27 huku Simba SC ikiwa nafasi ya tatu na alama 57 baada ya michezo 26.

MZIZIMA ‘DERBY’ KUISIMAMISHA DAR ES SALAAM LEO.

 

MCHEZO wa Ligi Kuu ya NBC ‘Derby’ ya Mzizima unapigwa leo kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa saa 12:15 jioni kati ya Azam na Simba.

Mchezo huu unabeba hisia za watu wengi kutokana na nafasi za kila timu kwenye msimamo huku ukiwa ni mchezo wa hatma za timu hizi kwenye nafasi ya kuendelea kupambania ubingwa.

Mchezo wa Mzunguko wa kwanza Simba dhidi ya Azam ulimalizika kwa Sare ya bao 1, bao la Azam likifungwa na Prince Dube huku lile la Simba likifungwa na Clatous Chama.

Kwenye msimamo Azam ipo nafasi ya Pili ikiwa na alama 57 baada ya michezo 25 huku Simba ikiwa nafasi ya Tatu ikiwa na alama 53 kwenye michezo 24 pungufu ya mchezo mmoja nyuma ya Azam.

FIRST LEAGUE NANE BORA KUANZA KUTIMUA VUMBI LEO.

 

MICHUANO ya First League hatua ya Nane Bora inaanza kutimua vumbi leo Mei 2 mkoani Tanga ikishirikisha jumla ya timu nane kutoka mikoa tofauti.

Mchezo wa ufunguzi utazikutanisha African Sports ya Tanga dhidi ya Malimao ya Dar es salaam saa 8:00 mchana katika uwanja wa CCM Mkwakwani ikifuatiwa na mchezo wa saa 10:00 alasiri kati ya Rhino Rangers na Nyumbu.

Timu shiriki ni Nyumbu ya Pwani, African Sports ya Tanga, Kiluvya na Malimao za Dar, Mapinduzi ya Mwanza, Rhino Rangers ya Tabora, Tanesco ya Kilimanjaro na Mwadui ya Shinyanga ambazo zimegawanya kwenye makundi mawili, ya A na B.

Timu mbili za juu kutoka kila kundi zitafuzu moja kwa moja hatua ya nusu fainali huku timu zitakazoingia fainali zitakata tiketi ya kushiriki Ligi ya NBC Championship msimu ujao wa 2024/2025.

Timu mbili zitakazopoteza hatua ya Nusu fainali zinayo nafasi ya kupanda Ligi ya NBC Championship kwa kucheza michezo ya mchujo na timu zilizopoteza mchezo wa mchujo wa Kubaki Ligi ya NBC Championship na mshindi wa jumla kushiriki Ligi ya NBC Championship msimu ujao wa 2024/2025.

KENGOLD BINGWA NBC CHAMPIONSHIP 2023/2024, PAMBA KARIBU LIGI KUU YA NBC.

 

MSIMU wa 2023/2024 Ligi ya NBC Championship umemalizika rasmi kwa KenGold kutawazwa mabingwa wa Ligi hiyo ikifikisha jumla ya alama 70 kwenye michezo 30 ikishinda 21, ikipata sare michezo 7 na kufungwa michezo 2.

Pamba FC imefanikiwa kupanda Ligi Kuu ya NBC moja kwa moja baada ya kushinda mchezo wa leo na kufikisha jumla ya alama 67 ambazo haziwezi fikiwa na timu yeyote inayomfuatia.

Mbeya kwanza na Biashara United watacheza hatua ya mtoano kutafuta timu moja kutoka Ligi ya NBC Championship itakayocheza hatua ya mtoano na timu moja toka Ligi Kuu ya NBC na mshindi wa Jumla kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025.

Timu kutoka Ligi Kuu ya NBC itakayocheza hatua ya mtoano dhidi ya timu ya Ligi ya NBC Championship ni timu itakayopoteza mchezo wa mtoano kati ya timu iliyoshika nafasi ya 13 na 14 ndani ya Ligi Kuu ya NBC.

Timu za Pan African ya Dar es salaam na Ruvu Shooting ya Iringa zimeshuka daraja moja kwa moja na mwakani zitashiriki First League msimu wa 2024/2025.

NBC CHAMPIONSHIP KUTAMATISHWA LEO, BINGWA KUJULIKANA.

 

LIGI ya NBC Championship inafika tamati leo kwa michezo nane ya mwisho kupigwa kuhitimisha jumla ya michezo 240 ya Ligi hiyo huku Michezo yote ikipigwa kuanzia saa 10:00 alasiri.

Vita ya Ubingwa leo itamtambulisha rasmi bingwa wa NBC Championship msimu 2023/2024 huku Ken Gold ikiwa tayari imekata tiketi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 itahitaji alama moja pekee ili kutangazwa bingwa.

Timu ya Pamba itahitaji kushinda dhidi ya Mbuni na endapo Ken Gold itapoteza mchezo wa leo timu ya Pamba itafanikiwa kuwa bingwa wa NBC Championship msimu huu.

Vita ya kupanda daraja moja kwa moja kwenda Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 itamalizika leo ambapo ni Pamba au Mbeya Kwanza wenye nafasi hiyo, Pamba inahitaji kushinda ili kujihakikishia alama 65 ambazo haziwezi kufikiwa na Mbeya Kwanza huku Mbeya Kwanza inahitaji kushinda na kuiombea Pamba ipoteze ili ipate nafasi hiyo.

Upande wa ufungaji wa mabao bado safari haijafika mwisho ambapo Edger William wa Ken Gold anashika usukani akiwa na mabao 20 huku Boban Bogere wa Biashara United akifuatia kwa karibu akiwa na mabao 19, Oscar Mwajanga wa Mbeya Kwanza na Maulid Shaban wa Mbeya City wanafuatia kila mmoja akiwa na mabao 17, je ni nani kuwa kinara wa Mabao msimu huu ?