Author: Yahaya Abushehe

‘KARIAKOO DERBY’ INAPIGWA LEO.

 

MCHEZO wa watani wa Jadi ‘Kariakoo Derby’ ndani ya Ligi Kuu ya NBC unachezwa leo saa 11:00 jioni kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mchezo huu ndio ni mkubwa zaidi Tanzania na Afrika mashariki na miongoni mwa ‘Derby’ kubwa zaidi barani Afrika.

Yanga inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 5-1 kwenye mchezo uliopita.

Mwamuzi wa kati kwenye mchezo huu ni Ahmed Arajiga kutoka Manyara, mwamuzi msaidizi namba moja ni Mohamed Mkono kutoka Tanga, mwamuzi msaidizi namba mbili ni Kassim Mpanga kutoka Dar es salaam na mwamuzi wa akiba ni Tatu Malogo kutoka Tanga.

“KARIAKOO DERBY” SIMBA YAJICHIMBIA ZANZIBAR, YANGA IKISALIA DAR.

 

JOTO la kuelekea mchezo wa watani wa jadi kati ya Yanga na Simba likiendelea kupanda timu ya wekundu wa msimbazi Simba wameamua kusafiri hadi visiwani Zanzibar kwa kambi ya maandalizi kuelekea mchezo huo huku Yanga ikisalia Jijini Dar es salaam kujifua kwenye uwanja wa Avic Town Kigamboni.

Simba ina kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo uliopita walipokubali kichapo cha mabao 5-1 mbele ya Yanga katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Mchezo huo wa Watani wa Jadi utapigwa Aprili 20, kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni.

ALLIANCE, DAR CITY ZASALIA FIRST LEAGUE.

 

Michezo miwili ya Mtoano wa kushuka daraja imemalizika kwa timu za Alliance na Dar City kufanikiwa kubaki kwenye First League msimu ujao wa 2024/2025 baada ya matokeo ya jumla.

Timu za Alliance na Dar City zimefuzu baada ya michezo ya jana kumalizika na Dar City kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Alliance na kupita kwa matokeo ya jumla ya mabao 5-0 huku mchezo Kati ya Alliance na African Lyon ukimalizika kwa suluhu na Alliance kuvuka kwa Matokeo ya jumla 1-0.

Michezo ya kwanza ilichezwa Aprili 6, 2024 ambapo African Lyon iliialika Alliance kwenye uwanja wa mabatini na kumalizika kwa suluhu, mchezo mwingine ulizikutanisha Kurugenzi dhidi ya Dar City kwenye uwanja wa CCM Kambarage mkoani shinyanga.

MZUNGUKO WA 28 NBC CHAMPIONSHIP KUPIGWA LEO.

 

MZUNGUKO wa 28 wa Ligi ya NBC Championship utapigwa leo Aprili 13 kwa michezo nane kuchezwa kwenye mikoa Saba tofauti majira ya saa 10:00 alasiri.

Mkoani Mwanza michezo miwili itapigwa Copco itakuwa mwenyeji wa Polisi Tanzania kwenye uwanja wa CCM Kirumba huku Pamba ikiwa mwenyeji wa FGA Talents kwenye uwanja wa Nyamagana.

Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Mbuni kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya huku Stand United ikicheza dhidi ya Transit Camp kwenye uwanja CCM Kambarage mkoani Shinyanga na Cosmopolitan itaialika Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Mabatini, Pwani.

Michezo mitatu ya timu zilizo ndani ya nne bora kwenye msimamo wa Ligi ya NBC Championship inabeba hisia za watu wengi kutokana na kila timu kuwa na nafasi ya kupanda Ligi Kuu ya NBC.

Michezo hiyo ni Mbeya Kwanza dhidi ya Pan African kwenye uwanja wa Nangwanda mkoani Mtwara, Biashara United dhidi ya Green warriors kwenye uwanja wa Karume mkoani Mara na TMA dhidi ya KenGold kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.

Michezo yote itachezwa saa 10:00 alasiri na baadhi ya michezo kurushwa mubashara kupitia chaneli za TV3, ST Bongo, TV3 YouTube na ST Bongo Youtube.

KARIAKOO DERBY KUPIGWA 20 APRILI

 

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imepanga upya tarehe ya mchezo namba 180 wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2023/2024 kati ya Yanga na Simba maarufu kama ‘Kariakoo Derby’.

Mchezo huo ambao haukupangiwa tarehe kwenye ratiba iliyofanyiwa maboresho Februari 2024, sasa utachezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Aprili 20, 2024 kuanzia saa 11:00 jioni.

Klabu za Yanga na Simba pamoja na wadau wengine wa Ligi Kuu ya NBC wamepewa taarifa hiyo kuhusiana na mchezo huo na maandalizi yake yanaanza mara moja ili kuhakikisha unafanyika katika kiwango cha juu kinachoendana na hadhi ya michezo mikubwa ya Ligi ya sita kwa ubora barani Afrika.