Author: Yahaya Abushehe

NYAVU ZAO HAZIGUSWI NBC CHAMPIONSHIP.

 

MABAO 519 yamefungwa mpaka sasa kwenye mizunguko 27 sawa na michezo 216 ya Ligi ya NBC Championship msimu huu.

Mlinda mlango wa Ken Gold Castor Mhagama anaongoza kwa kucheza michezo mingi bila kuruhusu bao akifanya hivyo kwenye michezo 16.

Mlinda mlango wa TMA Yusuf Abdul anafuatia akicheza michezo 15 bila kuruhusu bao lolote huku Robert Mapigano wa Biashara United akiwa na michezo 10 bila kuruhusu bao .

Jeremia Kisubi wa Mbeya City na Rahim Sheikh wa Mbeya Kwanza wanafuatia kila mmoja akiwa na michezo nane bila kuruhusu bao.

Ruvu Shooting ndio timu iliyo ruhusu mabao mengi ikiruhusu jumla ya mabao 57 kwenye michezo 27 iliyocheza mpaka sasa.

TUKUTANE FIRST LEAGUE NANE BORA.

 

HATUA ya kwanza ya Ligi ya First League iliyokuwa na jumla ya timu 16 kwenye makundi mawili ya timu nane imemalizika jana Machi 31 na kupata jumla ya timu nane zitakazokwenda kutafuta washindi wa kwenda ligi ya NBC Championship .

Timu zilizofanikiwa kuingia hatua hiyo ni African Sports, Kiluvya, Nyumbu na Malimao kutoka kundi A wakati timu za Mapinduzi, Rhino Rangers, Tanesco na Mwadui zikifuzu kutoka kundi B.

Timu za Tunduru kutoka kundi A na TRA kutoka kundi B zimejihakikishia nafasi ya kubakia First League msimu ujao kwa kushika nafasi ya tano kwenye makundi yao.

Timu zitakazocheza mtoano wa kushuka daraja (Relegation Play off) ni Dar City na African Lyon kutoka kundi A huku Kundi B ikikiwakilishwa na Alliance na Kurugenzi.

Timu zilizoshuka Daraja ni Lipuli ya Iringa iliyokuwa kundi A na Kasulu United ya Kigoma iliyokuwa Kundi B.

MBIVU NA MBICHI KUJULIKANA LEO FIRST LEAGUE.

 

JUMLA ya michezo Saba ya First League kundi A na B itapigwa leo Machi 31, 2024 kuhitimisha ratiba ya First League awamu ya kwanza msimu wa 2023/2024.

Kundi A timu za African Sports, Kiluvya, Nyumbu na Malimao tayari zimefuzu kwenda kwenye hatua ya nane bora huku mvutano ukisalia kwenye timu itakayobaki First League msimu wa 2024/2025 kati ya timu zitakazo cheza mtoano wa kushuka daraja timu hizo zikiwa ni Tunduru Korosho, Dar City na African Lyon.

Kundi B mpaka sasa hakuna timu yoyote iliyofanikiwa kutinga hatua ya nane bora (Top 8) huku timu tano pekee zikiwa na nafasi ya kufanya hivyo, Timu hizo ni TRA, Mapinduzi, Rhino Rangers, Tanesco na Mwadui zikiwa timu nne pekee kutoka kundi hili zenye nafasi ya kufuzu hatua ya nane bora .

Timu za Alliance na Kurugenzi zitacheza hatua ya mtoano wa kushuka daraja huku timu ya Kasulu ikiwa tayari imeshashuka daraja.

MICHEZO MIWILI KUHITIMISHA MZUNGUKO WA 27 NBC CHAMPIONSHIP LEO.

 

MZUNGUKO wa 27 Ligi ya NBC Championship unahitimishwa leo kwa michezo miwili kuchezwa kwenye mikoa ya Shinyanga na Morogoro.

Mkoani Shinyanga Stand United itaialika Green Warriors kwenye uwanja wa CCM Kambarage saa 8:00 mchana.

Stand United na Green Warriors zinapambana kutoka katika mstari wa kucheza mtoano wa kushuka daraja hivyo kufanya mchezo wa leo kuwa wa muhimu kwa pamde zote mbili.

Stand United ipo nafasi ya 11 na alama 30 kwenye michezo 26 iliyocheza huku Green Warriors ikiwa nafasi ya 12 na alama 27 kwenye michezo 26.

Mkoani Morogoro Transit Camp itaialika Biashara United kwenye uwanja wa Jamhuri saa 10:00 alasiri.

Transit Camp ipo nafasi mbaya kwenye msimamo ikiwa nafasi ya 13 na alama zake 23 kwenye michezo 26 huku Biashara ikihitaji ushindi ili kuzidi kuweka hai mbio za kuwania kupanda Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 ikiwa na alama 53 kwenye michezo 26 mpaka sasa.

KEN GOLD KINARA WA USHINDI NBC CHAMPIONSHIP.

 

MICHEZO 208 imechezwa ndani ya Ligi ya NBC Championship sawa na michezo 26 kwa kila timu huku jumla ya mabao 490 yakifungwa mpaka sasa.

Ken Gold kinara wa Ligi ya NBC Championship ndio timu iliyoshinda michezo mingi mpaka sasa ikishinda 18 huku ikifunga mabao 44 na kufungwa 15.

Pamba, Biashara na Mbeya Kwanza zinafuatia kila mmoja ikishinda michezo 16 Kati ya 26 iliyocheza mpaka sasa.

Pamba inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 55 huku Biashara United na Mbeya Kwanza zikifuatia kila mmoja ikiwa na alama 53 zikitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa Biashara ikiwa na tofauti ya mabao 29 huku Mbeya Kwanza ikiwa na 17.

Ruvu Shooting ndio timu iliyoshinda michezo michache zaidi ikifanya hivyo mara mbili pekee kwenye michezo 26 iliyocheza mpaka sasa huku ikishika nafasi ya mwisho kwenye Ligi ya NBC Championship.