Category: STORY

TRA, SIMBA, AZAM ZAGAWA ‘VICHAPO’ LIGI KUU YA NBC.

BAADA ya kuifunga Fountain Gate mabao 4-1 ugenini timu ya TRA imeshinda mchezo wa pili mfululizo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuifunga Namungo mabao 2-0 katika uwanja wa Black Rhino uliopo wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Mabao ya Chamou Karaboue na Joseph Akandwanaho yalitosha kuwapa furaha ‘walipa kodi’ huku yakipeleka huzuni na vilio kwa ‘Wauaji wa kusini’ wenyeji wa mkoa wa Lindi..

Chamou aliyesajiliwa na TRA akitokea kwa ‘wababe’ wa Kariakoo timu ya Simba alifunga bao lake la kwanza kwa timu yake huku akipokea pasi ya mwisho kutoka kwa Valentin Nouma aliyekuwa Simba pia ndiye aliyeibuka mchezaji bora wa mchezo huo akiisaidia kupata alama tatu bila kuruhusu bao.

Mkoani Singida kwenye uwanja wa Airtel Stadium timu ya Singida Black Stars ilishindwa kutamba nyumbani ikikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Simba na kupoteza mchezo wa pili mfululizo nyumbani baada ya kufungwa 3-0 na Young Africans.

Anicet Oura alikuwa wa kwanza kufungua akaunti ya mabao kwa ‘Mnyama’ akitumia vizuri pasi ya kichwa kutoka kwa Allasane Kante bao ambalo lilifutika dakika chache kabla ya mapumziko baada ya Ndumumwe Mossi kuisawazishia Singida.

Dakika tano kabla ya dakika 90 kukamilika Elie Mpanzu aliyeingia akitokea benchi alitumia vizuri pasi ya mchezaji bora wa mchezo huo Clatous Chama na kuiandikia Simba bao la pili lililohakikisha alama tatu muhimu kwa ‘Mnyama’ zilizomfanya kufikisha alama 27 na kutia kambi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Mchezo wa mwisho ulishuhudia ‘matajiri wa chamazi’ timu ya Azam ikiishushia kipigo timu ya Dodoma jiji kwa mabao 3-0 kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma na kupaa hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Mchezo huo ulioshuhudia kiungo Feisal Salum akifunga bao moja na kutoa pasi ya bao baada ya kurejea uwanjani akitoka kutumikia adhabu aliyopewa baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Pamba Jiji.

Mabao mengine yalifungwa na mchezaji wa zamani wa Dodoma Zidane Sereri aliyekuwa mwiba mkali kwa ‘walima zabibu’ na kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mchezo huo akiingia kambani mara mbili.

MICHEZO MITATU KUPIGWA LEO LIGI KUU YA NBC

Ligi Kuu ya NBC inaendelea kutimua vumbi leo, Machi 11, 2026, ambapo jumla ya michezo mitatu itapigwa katika mikoa ya Arusha, Singida na Dodoma, huku timu mbalimbali zikiingia uwanjani kusaka alama muhimu katika mbio za msimamo wa ligi.

Mchezo wa mapema utapigwa katika Uwanja wa Black Rhino, Karatu mkoani Arusha, ambapo TRA United itakuwa mwenyeji wa Namungo FC. TRA United inaingia kwenye pambano hilo ikiwa na alama 16 baada ya kucheza michezo 13 ya ligi hadi sasa.

Kwa upande wa Namungo FC, inayofundishwa na Kocha Juma Mgunda, inaingia katika mchezo huo ikiwa katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC, ikiwa imekusanya alama 21 baada ya kucheza michezo 16.

Mkoani Singida,mashabiki watashuhudia pambano jingine la kusisimua litakalowakutanisha Singida Black Stars dhidi ya Simba SC katika Uwanja wa Airtel, kuanzia majira ya saa 10:15 jioni.

Singida Black Stars inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi yake iliyopita kwa mabao 3-0 dhidi ya Young Africans. Kwa upande wake Simba SC inaingia kwenye mchezo huo ikiwa imetoka kupata sare ya bila kufungana dhidi ya Young Africans katika mchezo wake wa mwisho wa ligi.

Mchezo wa mwisho wa leo utapigwa katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, ambapo Dodoma Jiji itamenyana na Azam FC kuanzia saa 1:15 usiku.

Mara ya mwisho timu hizi mbili kukutana kwenye Ligi Kuu ya NBC ilikuwa Mei 13, 2025 katika Uwanja wa Azam Complex, ambapo Azam FC iliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0.

Mashabiki wa soka wanaweza kufuatilia michezo yote ya leo mubashara kupitia king’amuzi cha Azam TV kwenye chaneli ya Azam Sports 1 HD, au kusikiliza matangazo ya moja kwa moja kupitia TBC FM.

SINGIDA YATAKATA, PAMBA IKIBANWA NYUMBANI LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI Kuu ya NBC imeendeleza burudani ya aina yake huku mashabiki wakishuhudia ushindi mwembamba wa bao moja kwa Singida Black Stars dhidi ya Coastal na sare ya kusisimua ya mabao 2-2 kwa Pamba Jiji dhidi ya Azam FC.

Katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa airtel mkoani singida, Singida Black Stars waliikaribisha Coastal union na iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union huku shujaa wa mchezo huo akiwa mshambuliaji Joseph Guede aliyefunga bao pekee dakika ya 72 kwa umakini mkubwa akimalizia shambulizi lililowapa furaha mashabiki wa Singida.

Coastal walijitahidi kusaka bao la kusawazisha lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Singida ulihakikisha wanatoka bila alama wala bao.

Wakati huo huo jijini Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba saa kumi kamili jioni kulishuhudiwa pambano kali kati ya Pamba Jiji FC na Azam lililomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Pamba Jiji walianza kuonyesha makali kwa bao la Himid Mao aliyejifunga dakika ya 45 kabla ya John Nakibinge kuongeza la pili dakika ya 48.

Hata hivyo Azam hawakukata tamaa wakarejea kwa nguvu kupitia Jean Ngita dakika ya 56 na baadaye Feisal Salum kufunga kwa penalti dakika ya 59 na kuifanya mechi kuwa ya kusisimua hadi dakika ya mwisho.

Mchezo huo ulishuhudia Feisal akionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea mchezaji wa Pamba rafu mbaya na hivyo feisal kukosa mchezo unaofuata wa Dar es Salaam derby utakaoikutanisha Azam dhidi ya Young Africans.

Kwa matokeo hayo, Singida Black Stars wanaondoka na alama tatu muhimu, huku Azam na Pamba Jiji wakigawana alama mojamoja.

Derby

DERBY YA KIHISTORIA YA LIGI KUU YA NBC KUPIGWA ZANZIBAR LEO.

Tulihesabu miezi, tukahesabu wiki, tukahesabu siku na sasa tunahesabu masaa kuelekea mchezo mkubwa wa Kariakoo Derby kati ya Young Africans SC na Simba SC utakaopigwa katika dimba la Amaan, visiwani Zanzibar kwenye mpambano wa kusisimua utakaochezwa kuanzia majira ya saa 2:15 usiku leo Machi Mosi.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu ya NBC kwa Kariakoo Derby kuchezwa visiwani Zanzibar huku likiwa tukio la kipekee linaloandika ukurasa mpya wa soka la Tanzania, Swali linalobaki ni moja tu nani ataanza kuandika historia hiyo kwa ushindi?

Young Africans SC wanaingia katika pambano hili wakiwa kileleni na alama 28 baada ya michezo 10 wakishinda michezo tisa na kutoka sare mchezo mmoja pekee huku Safu yao ya ushambuliaji ikiwa moto wa kuotea mbali, wakifunga jumla ya mabao 28 idadi kubwa kuliko timu yoyote hadi sasa.

Siyo hilo tu, bali pia wameonyesha uimara wa kipekee katika safu ya ulinzi kwa kuruhusu mabao mawili pekee, rekodi bora zaidi msimu huu.

Lakini kwa upande wa Simba SC, ‘Wekundu wa Msimbazi’ wamejikusanyia alama 23 katika michezo 10 na wakishinda michezo saba, wakipoteza mmoja na kutoka sare mmoja, wakifunga mabao 18, wanashika nafasi ya pili kwa ufungaji nyuma ya watani zao na safu yao ya ulinzi pia imeonyesha uthabiti kwa kuruhusu mabao manne pekee, wakibaki miongoni mwa timu zenye safu imara zaidi ya ulinzi.

Hadi sasa, ni Young Africans SC na Azam FC pekee ambao hawajapoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu. Je, Simba SC wataweza kuivunja rekodi hiyo na kuandika sura mpya ya Derby ya kwanza visiwani Zanzibar?

Leo usiku, historia itaandikwa. Swali ni itaandikwa kwa wino wa nani ‘Wananchi’ Young Africans au ‘wekundu wa Msimbazi’ Simba SC ?

Tukune Amaan Stadium saa 2:15 usiku tuzishuhudie ladha za Ligi namba 6 kwa ubora barani Afrika na 54 Duniani, Ligi Kuu ya NBC.

SIMBA YAILIZA PRISONS LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Simba imeipa maumivu timu ya Tanzania Prisons baada ya kuifunga mabao 0-2 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Mchezo huo uliokuwa muhimu kwa timu zote ambapo Prisons ikitafuta nafasi ya kujitoka katika eneo la hatari huku Simba ikiwa katika harakati za kujiimarisha na kusogea juu zaidi kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

 

Dakika 19 zilimtosha mshambuliaji wa Simba Seleman Mwalimu kufungua ukurasa wa mabao wa mchezo huo huku beki wa timu hiyo Rushine De Reuck akifunga bao la pili dakika ya 45 ya mchezo huo kwa mkwaju wa penati hivyo Simba kwenda mapumziko ikiongoza 0-2.

Kipindi cha pili timu ya Prisons iliamua kucheza kwa kujilinda zaidi ili kutokuruhusu mabao mengine jambo ambalo lilifanikiwa na kwa upande wa Simba wakilinda ushindi wao na kuhakikisha pia wanaondoka na hati safi ambapo pia walifanilisha adhma yao.

Dakika 90 za mchezo huo zilifika tamati na beki wa Simba Rushine De Reuck alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo akiisaidia timu yake kubeba alama zote 3.