Category: STORY

YOUNG AFRICANS HAIKAMATIKI LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Young Africans imefanikiwa kuifunga timu ya Namungo bao moja kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa kwenye uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.

Mchezo ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa kasi kubwa kuhakikisha wanachukua alama tatu za Ligi Kuu ya NBC ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu.

Dakika 26 zilimtosha mshambuliaji wa Young Africans Laurindo Dilson kufungua ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penati baada ya mchezaji wao Max Nzengeli kufanyiwa madhambi na mchezaji wa Namungo bao lililodumu hadi mwisho wa kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili timu zote zilirejea kwa kasi kubwa Namungo ikijaribu kufanya mashambulizi ya mbali ambayo hata hivyo hayakuweza kuzaa matunda hadi dakika 90 za mchezo huo zinatamatika wageni Young Africans walifanikiwa kubeba alama zote tatu kutoka kwa Namungo. Mchezaji Max Nzengeli wa Young Africans alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Max Nzemgeli akiwa na tuzo yake

AZAM YATAKATA KMC COMPLEX.

TIMU ya Azam imeendeleza ubabe wake dhidi ya timu ya KMC baada ya kuifunga 0-2 katika mchezo uliopigwa leo kwenye uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo timu zote zilikuwa zikiutaka mchezo na zilishambuliana kwa kasi licha ya Azam kuutawala mchezo huo lakini hadi dakika 45 zinatamatika hakuna aliyefanikiwa kuguza nyavu za mwenzake kwa bao.

Akaminko (kushoto) akipambana namchezaji wa KMC

Kipindi cha pili dakika ya 55 ya mchezo mchezaji wa Azam Iddy Seleiman alifungua ukurasa wa mabao wa timu hiyo na kurejea tena kambani dakika ya 64 ya mchezo huo na kufanya Azam kuongoza kwa mabao mawili.

Hadi mwamuzi wa mchezo huo Ramadhani Kayoko anapuliza kipenga cha mwisho matokeo yalisalia 0-2 na kuifanya KMC kuendelea kuburuza ‘mkia’ wa Ligi Kuu ya NBC huku Iddy Selemani akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

SINGIDA YAONGEZA MAUMIVU KWA MTIBWA.

SINGIDA Black Stars imejipata baada ya kuifunga timu ya Mtibwa Sugar mabao 3-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa leo katika uwanja wa Jamhuri Dodoma majira ya saa nane mchana.

Iliwachukua dakika tano pekee Singida kufungua ukurasa wa mabao kupitia mchezaji wao Nduhumwe Mosi na dakika ya 16 Horso Muaku aliiongezea timu hiyo bao la pili hivyo kwenda mapumziko wakiongoza kwa mabao mawili.

Wachezaji wa Singida wakishangilia bao.

Kipindi ca pili timu zote zilikuwa na ari ya kutaka ushindi hasa Mtibwa iliyokuwa nyuma kwa mabao mawili hata hivyo ndoto zao zilizidi kudidimia baada ya Kennedy Juma kuongeza bao la tatu kwa timu ya Singida ikiwa ni dakika ya 58 ya mchezo huo.

Dakika ya 88 Mtibwa ilipata bao la kufutia machozi kupitia mchezaji wao Raizin Haji hivyo kufanya mchezo kumalizika wa 1-3 na Singida kufanikiwa kubeba alama zote tatu ugenini huku mchezaji wa Singida Horso Muaku alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Ladha za NBC

MIKOA SABA KUNOGESHA LADHA ZA NBC CHAMPIONSHIP LEO

Ladha za NBC Championship zinaendelea Leo, Februari 22, 2025, ambapo pazia la mzunguko wa 19 wa Ligi hiyo linafunguliwa rasmi kwa michezo saba itakayochezwa katika mikoa saba tofauti nchini. Kuanzia saa 10:00 alasiri, kila timu ikisaka alama tatu zenye uzito wa dhahabu katika safari ya kutimiza malengo yake.

Mbeya Kwanza vs Transit Camp

Mchezo unaovuta hisia zaidi ni kati ya Mbeya Kwanza na Transit Camp utakaopigwa katika Uwanja wa Airtel, mkoani Singida. Mbeya kwanza inatumia uwanja huo kama uwanja wake wa nyumbani kufuatia kufungiwa kwa Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi.

Mbeya Kwanza inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 40, huku Transit Camp ikifuatia katika nafasi ya nne na alama 36, Ushindi kwa Mbeya Kwanza utaifanya kufikisha alama 43 na kuimarisha nafasi yao katika mbio za kupanda Ligi Kuu ya NBC. Kwa Transit Camp, ushindi utaifanya kufikisha alama 39 na kupunguza kwa kiasi kikubwa pengo dhidi ya wapinzani wao wa moja kwa moja.

Mchezo huo utarushwa mubashara kupitia jukwaa la FIFA+ ukitoa fursa kwa mashabiki kote nchini kushuhudia patashika hiyo.

Vinara Kwenye Jaribio Zito

Geita Gold, vinara wa ligi hadi sasa na timu pekee ambayo haijapoteza mchezo msimu huu, watakuwa ugenini Moshi kuivaa Polisi Tanzania katika Uwanja wa Ushirika. Rekodi yao safi iko hatarini kila wanaposhuka dimbani, na kila mpinzani anatamani kuwa wa kwanza kuwavua ubabe huo. Je Polisi Tanzania watafanikiwa kuivunja rekodi hii ?

Michezo Mingine

Michezo mingine ya mzunguko huu ni:

  • TMA dhidi ya KenGold katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
  • Stand United dhidi ya Hausung katika Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.
  • BigMan dhidi ya Barberian katika Uwanja wa Ilulu, Lindi.
  • B19 wakiwakaribisha Gunners katika Uwanja wa TFF Center, Kigamboni.
  • African Sports dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo utakaokamilisha ratiba ya leo.

Kwa ujumla, mzunguko huu wa 20 unatarajiwa kuongeza ushindani na kuathiri kwa kiasi kikubwa mwenendo wa msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC kadri mbio za kupanda daraja zinavyozidi kushika kasi.

Mabao 325

HUKU NBC CHAMPIONSHIP ‘BOLI’ LINATEMBEA.

Baada ya kuchezwa kwa mizunguko 18 ya Ligi ya Championship ya NBC, jumla ya mabao 325 yamefungwa katika michezo 140 iliyochezwa hadi sasa, hali inayoonesha ushindani mkubwa miongoni mwa timu shiriki.

Mbeya Kwanza wanaongoza kwa ufungaji wa mabao, wakiwa wamefumania nyavu mara 37 huku wakiruhusu mabao 18. Kagera Sugar wanafuatia kwa karibu, wakiwa wamefunga mabao 33 na kuruhusu mabao 10 pekee, wakionesha uimara mkubwa katika safu ya ulinzi.

Vinara wa ligi hiyo kwa sasa, Geita Gold, wana uwiano bora wa mabao (goal difference), Timu hiyo imefunga mabao 32 na kuruhusu mabao nane tu, hivyo kuwa na tofauti ya mabao 24 takwimu inayodhihirisha uimara wao katika ushambuliaji na ulinzi.

Kwa upande mwingine, Barberian wanaoshika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC, ndio timu yenye idadi ndogo zaidi ya mabao ya kufunga, wakiwa wamefunga mabao 10 pekee na kuruhusu mabao 29.

‘Wana Kimanumanu’ African Sports ndio timu iliyoruhusu mabao mengi zaidi hadi sasa, wakiwa wamefungwa mabao 33 katika michezo 18 waliyocheza, huku wao wakifanikiwa kufunga mabao 14.