LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa mchezo mmoja uliochezwa katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma na kushuhudia Mtibwa sugar ikifanikiwa kuondoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City.
Mtibwa Sugar ilianza mchezo kwa kasi na dhamira ya kutafuta ushindi mapema na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 27 baada ya George Chota kufunga bao la kwanza kwa shuti lililomshinda kipa wa Mbeya City Beno Kakolanya na kuwapa wenyeji uongozi wa 1-0.
Mbeya City haikukata tamaa na dakika ya 45+2 Eliud Ambokile aliisawazishia Mbeya City bao baada ya kutumia vyema krosi ya beki wa kulia Maranyingi na kufanya matokeo kuwa 1-1 hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa kutoka Mtibwa Sugar wakitafuta bao la ushindi na dakika ya 63 Said Mkopi aliibuka shujaa baada ya kufunga bao la pili kwa ustadi mkubwa lililowarejesha Mtibwa Sugar mbele na matokeo kuwa 2-1.
Mbeya City ilijaribu kurejea mchezoni kwa kuongeza kasi ya mashambulizi lakini safu ya ulinzi ya Mtibwa Sugar ilisimama imara hadi filimbi ya mwisho na kuhakikisha wanachukua alama tatu muhimu huku timu hiyo ikipanda hadi nafasi ya 4 kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakifikisha na alama 14.