Category: STORY

MZIZE

TANZANIA YAANDIKA HISTORIA MPYA CHAN.

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imefanikiwa kufuzu hatua ya Robo Fainali ya michuano ya CHAN2024 inayoendelea katika nchi za Kenya, Tanzania na Uganda na kuwa nchi ya kwanza kujihakikishia kucheza hatua hiyo ya Robo Fainali.

Stars imefika hatua hiyo baada ya jana Agosti 9, kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Madagascar hivyo kujikusanyia alama tisa (9) baada ya kushinda michezo yote mitatu iliyocheza kwenye kundi lake.

Mabao yote ya Stars yalifungwa na Clement Mzize dakika ya pili na ya 21, hii ni kwa mara ya kwanza Clement Mzize anaifungia Timu ya Taifa ya Tanzania kwenye mchezo wa kimashindano.

Na hii ni mara ya kwanza kwa Timu ya Taifa ya Tanzania kufuzu hatua ya Robo Fainali tangu kuanzishwa kwa mashindano haya ya CHAN.

TANZANIA YAANZA NA USHINDI CHAN 2024.

TANZANIA YAANZA NA USHINDI CHAN 2024.

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imeanza vyema michuano ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza Ligi za ndani CHAN 2024 kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Timu ya Taifa ya Burkina Faso.

Mabao ya Stars yalifungwa na Abdul Suleimani anaekipiga kwenye timu ya Azam ya Dar es Salaam kwa mkwaju wa penati huku la pili likifungwa na Mohammed Hussein aliyemaliza mkataba wake na timu ya Simba akimaliza kazi safi iliyofanywa na Iddy Selemani (Nado) wa Azam.

Mchezo huo ulitanguliwa na Shamra shamra za ufunguzi wa michuano hiyo ambao kwa upande wa burudani ziliongozwa na msanii wa Bongo Fleva Raymond Mwakyusa maarufu Kama ‘Rayvanny’.

Timu ya Tanzania inaundwa na ‘mastaa’ mbalimbali wanaocheza Ligi za ndani ikiwemo Ligi Kuu ya NBC na Ligi ya Championship ya NBC.

Tanzania itarejea tena uwanjani Jumatano ya Agosti 6, saa 2:00 usiku ikiivaa timu ya Taifa ya Mauritania.

BODI YA LIGI KUU TANZANIA (TPLB) KUPOKEA MAONI YA MABORESHO YA KANUNI ZA LIGI

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) inaujulisha umma kuwa leo Julai 11, 2025 imeanza rasmi kupokea maoni ya maboresho ya Kanuni za Ligi kuelekea msimu wa 2025/2026.

Zoezi hilo la kupokea maoni litafanyika kwa kipindi cha majuma matatu ambapo litafungwarasmi Agosti 1, 2025.

Maoni ya maboresho ya kanuni yawasilishwe TPLB kwa kupitia njia zifuatazo;

i. Barua pepe – maoni@ligikuu.co.tz

ii. Ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) – +255 758 500 222

iii. Kuwasilisha kwa mkono katika ofisi za Bodi ya Ligi Kuu Tanzania zilizopo ghorofa

ya 14 kwenye jengo la NSSF (Mafao House), Ilala Dar es Salaam.

Bodi inawaomba wadau wote wa Ligi Kuu ya NBC, Ligi ya Championship ya NBC, First League na mpira wa miguu kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika zoezi hili muhimu kwa maendeleo ya Ligi zetu kwa kuchangia maoni yatakayosaidia kuboresha kanuni zake.

Wadau wanakumbushwa kuwa kanuni bora ndio msingi wa kupatikana kwa ligi bora na maendeleo ya mpira wa miguu kwa ujumla hivyo ushiriki katika zoezi hili ni jambo la muhimu sana.

STAND UNITED, FOUNTAIN GATE NI VITA YA KUCHEZA LIGI KUU YA NBC.

 

HATUA ya mtoano wa nani kusalia ama kupanda Ligi Kuu ya NBC inaendelea kesho kwa mchezo mmoja kati ya Stand United ya mkoani Shinyanga itakayokuwa mwenyeji wa timu ya Fountain Gate kwenye uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.

Mchezo huo utakaopigwa saa kumi alasiri utakuwa muhimu kwa timu zote ili kujihakikishia kucheza kwenye ligi namba nne kwa ubora barani Afrika.

Stand United ambao msimu wa 2024/2025 imecheza Ligi ya championship ya NBC inapaswa kupata ushindi wa matokeo ya jumla ya michezo ya nyumbani na ugenini ili kupanda Daraja huku timu ya Fountain Gate nayo ikipaswa kufanya hivyo ili kuhakikisha inabaki Ligi Kuu ya NBC msimu ujao.

Stand imepata nafasi ya kucheza hatua ya mtoano baada ya kuitoa timu ya Geita Gold kwa matokeo ya jumla huku Fountain ikicheza baada ya kupoteza kwenye matokeo ya jumla dhidi ya Tanzania Prisons.

Tatu Malogo kutoka Tanga ndiye mwamuzi atakaesimamia mchezo huo wa kwanza akisaidiwa na Hamdan Said kutoka Mtwara, Zawadi Yusuph kutoka Dar es Salaam na Shija Shurugwai kutoka mkoani Shinyanga.

PRISONS UHAKIKA LIGI KUU NBC 2025/26.

TIMU ya Tanzania Prisons imefanikiwa kusalia Ligi Kuu ya NBC baada ya kuifunga timu ya Fountain Gate 3-1 katika mchezo uliochezwa uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.

Ilimchukua dakika saba mchezaji wa Tanzania Prisons,Beno Ngasa kufungua ukurasa wa mabao huku mchezaji wa Fountain Gate Laurian Makame akisawazisha dakika ya 27 kabla ya Ezekiel Mwashilindi kuiongezea Prisons bao dakika ya 45 hivyo maafande hao Kwenda mapumziko wakiongoza 2-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo dakika ya 47 ya mchezo huo mchezaji wa Prisons Oscar Mwajanga aliongeza bao la tatu kwa timu hiyo na matokeo yakisalia hivyo mpaka mwisho wa mchezo .

Tanzania Prisons wamesalia Ligi Kuu ya NBC kwa uwiano wa mabao 4-2 katika michezo yote miwili ambayo timu hiyo na Fountain Gate zimecheza.