Category: STORY

NI VITA YA NANI KUBAKI LIGI KUU YA NBC SOKOINE LEO.

MCHEZO wa pili wa hatua ya mtoano kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Fountain Gate unatarajiwa kupigwa leo kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya kutafuta timu itakayosalia kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026.

Huu ni mchezo wa mwisho kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya NBC kukutana msimu huu baada ya kumaliza kwenye nafasi ya 13 na 14 ya msimamo zikiwa nafasi za kucheza michezo ya mtoano.

Mchezo huo wa mkondo wa pili utachezwa leo majira ya saa 10:00 alasiri ambapo mchezo wa kwanza uliochezwa uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara ulimalizika kwa sare ya 1-1.

Mshindi wa mchezo wa leo atakuwa amekata tiketi ya kusalia katika Ligi Kuu ya NBC huku atakayeshindwa atacheza mchezo wa mtoano dhidi ya timu ya Stand United inayoshiriki Ligi ya Championship ya NBC.

YOUNG AFRICANS MABINGWA LIGI KUU YA NBC 2024/2025

PAZIA la Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 limefungwa rasmi jana katika mchezo wa dabi ya Kariakoo ambapo timu ya Young Africans iliibuka na ushindi.

Katika mchezo ulichezwa majira ya saa kumi na moja jioni uwanja wa Benjamin Mkapa timu ya Yanga iliifunga timu ya Simba mabao 2-0 yaliyofungwa na wachezaji Pacome Zouzoa na Clement Mzize kipindi cha pili cha mchezo huo.

Mara baada ya mchezo huo Young Africa ilikabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 na kuweka historia ya kulibeba kombe hilo mara 31 huku timu hiyo ikikusanya alama 82 na mtani wao Simba akibaki nafasi ya pili na alama 78.

timu zote zimekata tiketi kushiriki Ligi ya mabingwa barani Afrika (CAF Champions League) kwa msimu wa 2025/2025 huku Azam na Singida Black Stars wakishiriki Kombe la Shirikisho(CAF Confederation Cup)

NI VITA YA UBINGWA ‘DERBY’ YA KARIAKOO LEO.

 

‘DERBY YA MAAMUZI’ ndivyo unavyoweza kuuita mchezo wa watani wa Jadi ‘Kariakoo Derby’ ndani ya Ligi Kuu ya NBC unachezwa leo saa 11:00 jioni kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam.

Huu ni mchezo wa kufunga Pazia la Ligi Kuu ya NBC kwa msimu wa 2024/2025 lakini pia ndio mchezo utakaotoa Bingwa wa Ligi Kuu ya NBC kwa msimu huu wa 2024/2025.

Young Africans inahitaji alama moja pekee ili kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC kwa msimu huu kwa kuwa itafikisha alama 80 ambazo haziwezi fikiwa na timu nyengine yoyote.

Matokeo ya Ushindi ndio silaha pekee kwa Simba ili kuweza kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC kwa msimu huu wa 2024/2025, hii ni kutokana na utofauti wa alama Kati yake na timu inayoongoza Ligi Young Africans.

Yanga inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo uliopita huku ikiongoza msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na alama 79.

Mwamuzi wa kati kwenye mchezo huu ni Amin Mohammed Amin, mwamuzi msaidizi namba moja ni Mahmoud Ahmed Abo, mwamuzi msaidizi namba mbili Samil Gamal Saad na mwamuzi wa akiba ni Ahmed Mahrous Elghandour wote kutoka Misri.

‘PILATO’ WA DABI YA KARIAKOO HUYU HAPA.

RAIA wa Misri Amin Mohamed Amin ndiye atakayechezesha mchezo wa Young Africans dhidi ya Simba maarufu kama ‘Kariakoo Dabi’ Juni 25 kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Ikiwa Yanga itashinda mchezo huo au kutoa sare ya aina yoyote itaibuka mshindi wa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 na ikiwa Simba itafanikiwa kushinda itaibuka mabingwa wapya wa kombe hilo.

Amin atasaidiwa na Mahmoud El Regal,Samir Gamal Mohamed na Ahmed Mahrous Elghandour wote kutoka nchini Misri huku mtathimini waamuzi akiwa ni Alli Mohamed kutoka nchini Somalia.

Hii ni mara ya kwanza kwa mchezo wa Ligi Kuu ya NBC kusimamiwa na waamuzi wa mchezo kutoka nje ya Tanzania.

Mchezo huo ambao mwenyeji ni timu ya Young Africans yenye alama 79 huku ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Simba yenye alama 78 ikishika nafasi ya pili utapigwa saa kumi na moja jioni.

Ratiba ya Ligi Kuu ya NBC 2025/2026

VIWANJA NANE KAZINI LEO LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC inatimua ‘vumbi’ leo kwenye viwanja nane tofauti ikiwa ni michezo ya kukamilisha mzunguko wa 30 wa ligi hiyo msimu wa 2024/25.

Macho na masikio yatakuwa zaidi kwa ‘Vigogo’ wa ligi hiyo timu za Yanga na Simba zilizopishana alama moja pekee huku timu hizo zikiwa nyumbani kwenye michezo yao ya leo.

Young Africans inayoongoza ligi hiyo itakuwa nyumbani kwenye uwanja wa New Amaan, Zanzibar kuwaalika Dodoma Jiji ya Dodoma huku ‘watani’ zao Simba wakiwa uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kuwaalika Kagera Sugar iliyoshuka daraja hadi sasa.

‘Maafande’ wa timu ya Mashujaa watakuwa nyumbani kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma kuwaalika wenzao wa JKT Tanzania huku timu ya Pamba Jiji ya halmashauri ya Jiji la Mwanza ikiwa mwenyeji wa KMC inayomilikiwa na manispaa ya Kinondoni kwenye uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Singida Black Stars itakuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Liti, Singida kuwakaribisha Tanzania Prisons ya Mbeya inayopambana kujitoa kwenye nafasi ya kucheza hatua ya mtoano huku Ken Gold ikiwa ugenini kwenye uwanja wa Majaliwa, Lindi kurusha ‘karata’ yake ya mwisho ya Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Namungo baada ya kushuka daraja msimu huu ikiwa timu ya mwisho kwenye msimamo wa ligi hiyo.

‘Matajiri wa Chamazi’ timu ya Azam FC baada ya kuichapa Tabora United mabao 5-0 nyumbani, itakuwa ugenini leo kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa dhidi ya Fountain Gate na mchezo wa mwisho utakuwa kati ya Coastal Union ambayo haijapoteza mchezo tangu kurejea kwenye uwanja wake wa Mkwakwani ikiikaribisha Tabora United.

Michezo yote itapigwa kuanzia saa 10:00 alasiri na kurushwa mbashara kwenye stesheni za Azam.