Category: STORY

MZIZE,DUBE HAWASHIKIKI LIGI KUU NBC

WASHAMBULIAJI wa Yanga Prince Dube na Clement Mzize wameongeza kasi katika mbio za ufungaji bora baada ya kufung mabao mawili kila mmoja katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya KenGold mchezo uliochezwa leo katika uwanja wa KMC.

Licha ya Kocha Mkuu wa Yanga Saed Ramovic kuaga jana ikiwa ni saa chache kuelekea mechi yao dhidi ya KenGold Yanga imefanikiwa kufunga mabao 6-1 .

Prince Dube ndio alifungua ukurasa wa mabao ikiwa ni dakika ya pili ya mchezo huo kabla ya Mzize  kufunga baola pili dakika ya sita ya mchezo huo huku Pacome Zouzuoa akiongeza bao la tatu dakika ya 39 dakika  nne mbele Mzize alirudi tena na kufunga bao la nne huku Dube akiongeza bao la tano dakika ya 43 y mchezo huo na kuwafanya Yanga kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 5-0.

Kipindi cha pili kilianza huku Yanga wakionekana kuzidi kulisakama lango la kenGold  licha ya timu zote kufanya mabadiliko ya wachezaji  ambapo Yanga dakika ya 85 Duke Abuya aliongeza bao la 6 kwa  timu yake.

KenGold walipata bao la kujifutia machozi kupitia mchezaji wake Seleman Rashid baada ya kupiga mpira mrefu ambao ulimshinda kipa wa Yanga Djigui Diarra hivyo mchezo kutamatika kwa 6-1.

Mshambuliaji wa Yanga Prince Dube alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.

Ligi Kuu itaendelea kesho kwa michezo minne ambapo Dodoma Jiji watawakaribisha Pamba,Tanzania Prisons dhidi ya Mashujaa,Fountain Gate wakiwakaribisha Simba na Azam watacheza na KMC .

CHIKOLA AWALIZA NAMUNGO LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC imeendelea leo mkoani Tabora kwa mchezo uliozikutanisha  timu ya Tabora United dhidi ya  timu ya Namungo  katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

Mchezo huo uliochezwa majira ya saa nane mchana  ulianza kwa kasi tangu mwanzo kwani dakika ya nne ya mchezo huo mchezaji wa Namungo, Jacob Massawe aliweka mpira wavuni mwa Tabora United.

Offen Chikola ndio alirejesha matumaini ya Tabora United katika dakika ya 32 ya mchezo huo ambapo alifunga bao na hivyo kuifanya mechi kwenda mapumziko wakiwa sare ya 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo dakika ya 52 mshambuliaji wa Tabora Heritier Makambo aliiongezea bao la pili timu yake na kufanya ubao kusomeka 2-1 pasi ya mwisho ikiwa imetolewa na Offen Chikola.

Mchezo ulitamatika kwa timu ya Tabora kubeba alama zote tatu mhimu za mchezo huo na mchezaji wao Offen Chikola akitangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.

TRANSIT YASHINDWA KUIZUIA STAND NBC CHAMPONSHIP.

LIGI ya NBC ya Championship imeendelea kwa mchezo mmoja uliopigwa uwanja wa Mabatini, Pwani kati ya Transit Camp ya Dar iliyochezea ‘kichapo’ cha mabao 3-0 kutoka kwa Stand United ya Shinyanga.

Mchezo ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu huku Stand ikitangulia kupata bao mapema lililoipa uongozi hadi kipindi cha kwanza kwanza kinamalizika likifungwa kwa mkwaju wa penati kupitia kwa Kigi Makasi.

Kipindi cha pili Stand ilijihakikishia ushindi kwa mabao mawili yaliyofungwa na Seleman Seif na Omar Issa na kuifanya Stand kumaliza mchezo huo kwa kukusanya alama zote tatu na bila kuruhusu wavu wao kuguswa.

Matokeo hayo yanaifanya Stand kupaa hadi nafasi ya nne ya msimamo wa ligi ya NBC ya Championship baada ya kukusanya jumla ya alama 35 nyuma ya vinara Mtibwa Sugar wanaoshikilia usukani wa ligi hiyo wakifuatiwa na Geita Gold na Mbeya City.

MBIO ZA UFUNGAJI BORA ZAPAMBA MOTO LIGI KUU YA NBC.

MZUNGUKO wa 16 umekamilika kwa timu zote za Ligi Kuu ya NBC huku vita ya kuwania ufungaji bora ikizidi kushika kasi na Elvis Rupia akiendelea kushikilia usukani wa kinyang’anyiro hicho.

Rupia anaongoza baada ya kupachika mabao nane hadi sasa na kuisaidia timu yake kufikisha alama 30 na kukaa nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Clement Mzize wa Yanga, Jean Ahoua na Leonel Ateba wa Simba wanafuatia wakiwa na mabao saba kila mmoja huku Ateba akifunga penati nne na Ahoua akifunga tatu.

Selemani Mwalimu aliyekuwa Fountain Gate na kusajiliwa na ‘Miamba’ ya soka nchini Morocco Wydad Casablanca amefunga mabao sita sawa na Pacome Zouzoua wa Yanga.

Prince Dube wa Yanga, Edger William wa Fountain Gate na Peter Lwasa wa Kagera Sugar wanafunga msimamo huo wa vinara wa mabao wakiwa na mabao matano kila mmoja.

MZUNGUKO WA 17 NBC CHAMPIONSHIP KUKAMILIKA LEO.

MZUNGUKO wa 17 wa Ligi ya Championship ya NBC unatamatika leo kwa mchezo kati ya Transit Camp ya Dar es salaam na Stand United ya Shinyanga saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Mabatini Mkoani Pwani.

Transit Camp ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikiwa na alama 10 sawa na Kiluvya iliyo nafasi ya 14 zikitofautiana kwenye mabao ya kufunga na kufungwa huku Stand United ikiwa nafasi ya nne (4) na alama 32.

Mpaka sasa Mtibwa Sugar inaongoza kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikiwa na alama 44 kwenye michezo 17 wakati Biashara United ikishika nafasi ya mwisho ikiwa na alama nne (4) pekee kwenye michezo 17