Category: STORY

DODOMA JIJI YASHINDWA KUTAMBA NYUMBANI.

TIMU ya Dodoma Jiji imepoteza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kurejea kutoka kwenye mapumziko mafupi kwa bao moja kutoka kwa Pamba Jiji ya mkoani Mwanza.

Mchezo huo uliokutanisha timu zilizopo chini ya manispaa za jiji ulipigwa kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma na kushuhudia bao lililofungwa kipindi cha kwanza na Mathew Tigisi likiizamisha Dodoma nyumbani.

Huu ni mchezo wa tatu kwa timu ya Pamba kushinda kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu huku ikishinda miwili ugenini na mmoja pekee ikishinda kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Dodoma imepoteza mchezo wa nane msimu huu idadi sawa na timu ya Pamba jiji huku Dodoma ikisalia nafasi ya tisa na alama 19 nne zaidi ya timu ya Pamba iliyofikisha alama 15 na kushika nafasi ya 14.

PRISONS YAIDUWAZA MASHUJAA LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Tanzania Prisons imerejea vema kwenye Ligi Kuu ya NBC baada ya kuifunga Mashujaa mabao 2-1 kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mabao ya Prisons yalifungwa na Beno Ngassa mdogo wa nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania Mrisho Ngassa na Meshack Mwamita aliyefunga bao la ushindi kipindi cha pili huku bao la kufutia machozi kwa mashujaa likifungwa Seif Karihe kwa mkwaju wa penati.

Ukiwa mchezo wa kwanza kwa kocha mpya wa Prisons Amani Josiah kwenye Ligi Kuu ya NBC Prisons imesalia nafasi ya 13 ikifikisha alama 17 sawa na Namungo huku Prisons ikizidiwa kwa mabao ya kufunga.

Matokeo hayo yanaifanya timu ya Mashujaa kusalia nafasi ya saba ikiwa na alama 19 sawa na timu za JKT, Dodoma Jiji na KMC huku mashujaa ikiwa juu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

FOUNTAIN GATE,SIMBA WATOSHANA NGUVU LIGI KUU NBC.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea jana  mkoani Manyara ambapo  timu ya Fountain Gate Iliwakaribisha timu ya Simba katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa majira ya saa kumi alasiri.

Mchezo huo ulianza kwa kasi ambapo timu zote zilionekana kushambuliana kwa kasi kubwa  huku kila timu ikionyesha nia ya kuzitaka  alama tatu muhimu za mchezo huo jambo lilipolekea kwenda mapumziko wakiwa hawajafungana .

Kipindi cha pili kilianza ambapo dakika ya  57 mshambuliaji wa Simba, Leonel Ateba alifunga bao la  kwanza kwa timu yake   hivyo Simba kuwa mbele kwa  0-1.

Dakika ya 74 winga wa Simba Ladack Chasambi alijifunga goli  baada ya kupiga mpira  nyuma na golikipa wa Simba Moussa Camara  kushindwa kuumudu  ukaingia  nyavuni hivyo ubao kusomeka 1-1 mpaka mchezo huo unatamatika.

Simba ilifanikiwa kuvuna alama moja ugenini na kufikisha alama 44  wakiwa nafasi ya pili ya msimamo wakiwa wamefunga mabao 35 na kufungwa 6 katika mechi 17 ilizocheza mpaka sasa.

 

MTIBWA WABABE WA NAMBA NBC CHAMPIONSHIP MPAKA SASA.

JUMLA ya Michezo 136 kati ya 240 imeshachezwa kwenye Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2024/2025 na kushuhudia jumla ya mabao 297 yakifungwa kwenye michezo hiyo huku Mtibwa Sugar ikiwa kinara kwa kufunga mabao mengi.

Mtibwa imefunga jumla ya mabao 31 kwenye michezo 17 mengi zaidi kuliko timu yeyote kwenye Ligi ya Championship ya NBC hadi sasa huku ikiruhusu kufungwa mabao saba pekee machache zaidi kuliko timu yeyote kwenye Ligi hiyo.

Mtibwa inaongoza msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikiwa na alama 44 baada ya michezo 17 ikishinda michezo 14 ikipata sare michezo miwili na kufungwa mchezo mmoja pekee.

 

LIGI KUU YA NBC

LIGI KUU YA NBC KUCHEZWA VIWANJA VINNE LEO.

LIGI Kuu ya NBC inaendelea kwa mzunguko wa 17 huku mechi nne zikichezwa katika viwanja mbalimbali nchini kuanzia majira ya saa nane mchana.

Mchezo wa kwanza utachezwa saa nane mchana katika  uwanja wa Jamhuri Dodoma ambapo Dodoma Jiji watawakaribisha Pamba Jiji kutoka jijini Mwanza .

Sambamba na mchezo huo Tanzania Prisons “wajelajela” watawakaribisha timu ya Mashujaa “Wana mapigo na mwendo” katika uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya  muda ikiwa ni saa nane mchana.

Mchezo  wa tatu  kwa siku ya leo ni timu ya Fountain Gate watawakaribisha  timu ya Simba katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati Mkoani Manyara saa kumi alasiri.

Mkoani Dar es Salaam wenyeji wa  uwanja wa Chamazi  timu ya Azam watawakaribisha timu ya KMC “Kinoboys” katika mchezo utakaochezwa saa moja jioni.