Category: STORY

PAMBA, SINGIDA KUKIWASHA MWANZA, COASTAL KUJIULIZA LIGI KUU YA NBC.

BAADA ya KMC kupata ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC jana dhidi ya KenGold kwa bao moja huku Kagera Sugar ikitoka suluhu na JKT Tanzania leo ligi hiyo inaendelea kwa michezo miwili.

Mapema saa 8:00 mchana timu ya Pamba ya Mwanza itakuwa mwenyeji wa Singida BS kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Pamba haijaruhusu bao mpaka sasa huku ikitoa suluhu kwenye michezo yake mitatu iliyocheza dhidi ya Prisons, Dodoma Jiji na Azam FC huku timu ya Singida ikishinda michezo yote mitatu iliyocheza na KenGold, Kagera Sugar na KMC.

Saa 10:15 alasiri Coastal Union ambayo haijapata ushindi wowote msimu huu itakuwa uwanja wa nyumbani Azam Complex dhidi ya Namungo iliyopoteza michezo yote ya Ligi Kuu ya NBC hadi sasa.

COASTAL KUJIULIZA KWA MASHUJAA LEO KWENYE LIGI KUU YA NBC.

BAADA ya Singida Black Stars na Dodoma Jiji kutamba kwenye uwanja wa nyumbani jana kwa ushindi jana timu ya Coastal Union leo itakuwa mwenyeji wa Mashujaa kuzisaka alama tatu muhimu.

Coastal iliyochagua kutumia uwanja wa KMC uliopo Dar kama uwanja wa nyumbani kwenye mchezo huu itacheza huku ikipambana kupata ushindi wa kwanza msimu huu dhidi ya Mashujaa ambayo haijapoteza mchezo wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu.

Coastal ilipata sare ya bao moja kwenye mchezo wake uliopita dhidi ya KMC baada ya Maabad Maabad kusawazisha dakika za mwisho kwa mkwaju wa penati.

Mashujaa ni miongoni mwa timu saba za Ligi Kuu ya NBC ambazo bado hazijaruhusu bao lolote msimu huu ikiungana na timu za Simba, Yanga, Pamba Jiji, Azam, Tanzania Prisons na JKT Tanzania.

‘KIVUMBI’ CHA LIGI KUU YA NBC KUENDELEA.

BAADA ya Tabora United na Fountain Gate kupata ushindi hapo jana Ligi Kuu ya NBC inaendelea tena leo kwa michezo miwili itakayopigwa mikoa miwili tofauti.

Saa 10:00 alasiri timu ya Singida BS ya Singida itakuwa mwenyeji wa KMC ya Dar kwenye uwanja wa Liti, Singida.

Singida imeshinda michezo yote miwili ya kwanza msimu huu iliyocheza ugenini na leo itaikaribisha KMC kwenye mchezo wa kwanza katika uwanja wa nyumbani.

Mchezo wa pili utachezwa saa 10:00 alasiri kama mchezo wa awali kati ya timu ya Dodoma Jiji na Namungo ya Lindi kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara.

Timu zote mbili hazijapata ushindi kwenye mchezo wowote wa Ligi Kuu ya NBC hadi sasa na hivyo kufanya mchezo huu kuwa na ushindani mkubwa.

TABORA UTD, FOUNTAIN GATE ZATAKATA NYUMBANI LIGI KUU YA NBC.

 

MICHEZO miwili ya Ligi Kuu ya NBC imechezwa Septemba 11 katika mikoa ya Tabora na Manyara na kushuhudia timu mwenyeji wa mikoa hiyo Tabora UTD na Fountain Gate zikitakata.

Mchezo wa mapema saa 8:00 mchana Tabora UTD iliialika Kagera Sugar kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora na kumalizika kwa Tabora kushinda kwa bao 1 likifungwa kwa mkwaju wa penati na Asiegbu Shedrack.

Saa 10:00 jioni katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa Mkoani Manyara Fountain Gate ikaibamiza Kengold kwa mabao 2-1.

Kengold ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Joshua Ibrahim dakika ya 8 huku bao la kusawazisha la Fountain Gate likifungwa na Kassim Abdallah dakika ya 45, Selemani Mwalimu akafunga ukarasa wa mabao kwenye mchezo huo akifunga bao la pili na la ushindi kwa Fountain Gate.

Kwa matokeo hayo timu ya Tabora United imekwea mpaka nafasi ya nne baada ya kufikisha alama sita huku Fountain ikipanda hadi nafasi ya tatu ikiwa na alama sita zikitofautiana kwa mabao ya kufunga

LIGI KUU YA NBC KUENDELEA LEO.

LIGI Kuu ya NBC inatarajiwa kuendelea leo kwa michezo miwili baada ya kusimama kwa takribani siku 13 kupisha michezo ya kimataifa.

Mchezo wa kwanza utachezwa saa 8:00 mchana kati ya timu ya Tabora United itakayokuwa nyumbani kuikaribisha Kagera Sugar kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora ukiwa mchezo wa kwanza wa Tabora kwenye uwanja wa nyumbani.

Mchezo wa mwisho utapigwa saa 10:15 alasiri kati ya Fountain Gate na KenGold kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo mkoani Manyara wilaya ya Babati.

Huu ni mchezo wa kwanza kwa timu ya Fountain kucheza nyumbani ukiwa pia mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC kuchezwa mkoani Manyara kwenye wilaya ya Babati.