Category: STORY

NBC CHAMPIONSHIP KUTAMATISHWA LEO, BINGWA KUJULIKANA.

 

LIGI ya NBC Championship inafika tamati leo kwa michezo nane ya mwisho kupigwa kuhitimisha jumla ya michezo 240 ya Ligi hiyo huku Michezo yote ikipigwa kuanzia saa 10:00 alasiri.

Vita ya Ubingwa leo itamtambulisha rasmi bingwa wa NBC Championship msimu 2023/2024 huku Ken Gold ikiwa tayari imekata tiketi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 itahitaji alama moja pekee ili kutangazwa bingwa.

Timu ya Pamba itahitaji kushinda dhidi ya Mbuni na endapo Ken Gold itapoteza mchezo wa leo timu ya Pamba itafanikiwa kuwa bingwa wa NBC Championship msimu huu.

Vita ya kupanda daraja moja kwa moja kwenda Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 itamalizika leo ambapo ni Pamba au Mbeya Kwanza wenye nafasi hiyo, Pamba inahitaji kushinda ili kujihakikishia alama 65 ambazo haziwezi kufikiwa na Mbeya Kwanza huku Mbeya Kwanza inahitaji kushinda na kuiombea Pamba ipoteze ili ipate nafasi hiyo.

Upande wa ufungaji wa mabao bado safari haijafika mwisho ambapo Edger William wa Ken Gold anashika usukani akiwa na mabao 20 huku Boban Bogere wa Biashara United akifuatia kwa karibu akiwa na mabao 19, Oscar Mwajanga wa Mbeya Kwanza na Maulid Shaban wa Mbeya City wanafuatia kila mmoja akiwa na mabao 17, je ni nani kuwa kinara wa Mabao msimu huu ?

DAR ES SALAAM NI KIJANI NA NJANO LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea Aprili 20 kwa mchezo wa ‘Kariakoo Derby’ uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa na kumalizika kwa Yanga kuibuka washindi kwa mabao 2-1 dhidi ya Simba.

Yanga imeshinda michezo yote ya Ligi Kuu ya NBC iliyokutana na mtani wake Simba msimu huu wa 2023/24 baada ya mzunguko wa kwanza kupata ushindi mnono wa mabao 5-1 ugenini.

Mabao ya Stephane Aziz Ki aliyefunga kwa mkwaju wa penati na Joseph Guede yametosha kuipa Yanga ushindi huo huku bao pekee la Simba likifungwa na Fred Michael Koublan.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kuwa mbele ya Simba kwa tofauti ya alama 12 huku Simba ikiwa na mchezo mmoja mkononi.

Ligi hiyo itaendelea leo kwa michezo mitatu ambapo mchezo wa mapema timu ya Tabora United itakuwa mwenyeji wa Geita Gold saa 8:00 mchana, saa 10:00 alasiri Singida Fountain Gate itaialika Mashujaa kwenye uwanja wa CCM Kirumba na mchezo wa mwisho utakuwa kati ya Azam FC na Ihefu kwenye uwanja wa Azam Complex.

‘KARIAKOO DERBY’ INAPIGWA LEO.

 

MCHEZO wa watani wa Jadi ‘Kariakoo Derby’ ndani ya Ligi Kuu ya NBC unachezwa leo saa 11:00 jioni kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mchezo huu ndio ni mkubwa zaidi Tanzania na Afrika mashariki na miongoni mwa ‘Derby’ kubwa zaidi barani Afrika.

Yanga inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 5-1 kwenye mchezo uliopita.

Mwamuzi wa kati kwenye mchezo huu ni Ahmed Arajiga kutoka Manyara, mwamuzi msaidizi namba moja ni Mohamed Mkono kutoka Tanga, mwamuzi msaidizi namba mbili ni Kassim Mpanga kutoka Dar es salaam na mwamuzi wa akiba ni Tatu Malogo kutoka Tanga.

“KARIAKOO DERBY” SIMBA YAJICHIMBIA ZANZIBAR, YANGA IKISALIA DAR.

 

JOTO la kuelekea mchezo wa watani wa jadi kati ya Yanga na Simba likiendelea kupanda timu ya wekundu wa msimbazi Simba wameamua kusafiri hadi visiwani Zanzibar kwa kambi ya maandalizi kuelekea mchezo huo huku Yanga ikisalia Jijini Dar es salaam kujifua kwenye uwanja wa Avic Town Kigamboni.

Simba ina kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo uliopita walipokubali kichapo cha mabao 5-1 mbele ya Yanga katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Mchezo huo wa Watani wa Jadi utapigwa Aprili 20, kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni.

ALLIANCE, DAR CITY ZASALIA FIRST LEAGUE.

 

Michezo miwili ya Mtoano wa kushuka daraja imemalizika kwa timu za Alliance na Dar City kufanikiwa kubaki kwenye First League msimu ujao wa 2024/2025 baada ya matokeo ya jumla.

Timu za Alliance na Dar City zimefuzu baada ya michezo ya jana kumalizika na Dar City kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Alliance na kupita kwa matokeo ya jumla ya mabao 5-0 huku mchezo Kati ya Alliance na African Lyon ukimalizika kwa suluhu na Alliance kuvuka kwa Matokeo ya jumla 1-0.

Michezo ya kwanza ilichezwa Aprili 6, 2024 ambapo African Lyon iliialika Alliance kwenye uwanja wa mabatini na kumalizika kwa suluhu, mchezo mwingine ulizikutanisha Kurugenzi dhidi ya Dar City kwenye uwanja wa CCM Kambarage mkoani shinyanga.