Category: STORY

LIGI KUU YA NBC KUREJEA FEBRUARI 2.

BAADA ya kusimama kwa takribani siku 40 kupisha mashindano ya Mataifa ya Afrika yanayoendelea nchini Ivory Coast Ligi Kuu ya NBC inarejea tena Februari 2.

Ligi hiyo itarejea kwa mchezo mmoja utakaopigwa saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera kati ya Kagera Sugar na Yanga.

Ligi hiyo namba sita kwa ubora Afrika inarejea baada ya timu ya taifa ya Tanzania kushindwa kufuzu kwenye hatua ya 16 bora na kutolewa kwenye mashindano ya Mataifa ya Afrika.

Ni ‘Mastaa’ watatu pekee waliosalia kwenye mashindano hayo hadi sasa ambao ni Henock Inonga wa timu ya Simba, Stephane Aziz Ki wa Yanga na Djigui Diarra wa Yanga hivyo kuruhusu ligi hiyo kuendelea kwa mujibu wa kanuni.

BIASHARA YAISHUSHA PAMBA, POLISI, TRANSIT HAKUNA MBABE LIGI YA NBC CHAMPIONSHIP.

TIMU ya Bishara United ya Mara imeiduwaza Pamba ya Mwanza baada ya kuifunga bao 1-0 kwenye mchezo uliopigwa uwanja wa Mwadui, Shinyanga.

Pamba iliyokuwa mwenyeji wa mchezo huo imeruhusu bao la dakika ya 87 lililofungwa na Ramadhan Kipalamoto na kuifanya timu hiyo kushuka kutoka nafasi ya pili mpaka ya tatu na kuipisha Biashara iliyokaa nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao ya kufunga.

Mkoani Kilimanjaro timu ya Polisi Tanzania imeshindwa kutamba baada ya kulazishwa sare ya bao moja dhidi ya timu ya Transit Camp ya mkoani Dar es Salaam.

Polisi inakwea hadi nafasi ya nane ikiwa na alama 26 huku Transit ikisalia nafasi ya 13 baada ya kufikisha alama 16.

Ken Gold ya Mbeya inaendelea kushika nafasi ya kwanza ikiwa na alama 43 huku Ruvu Shooting ya Pwani ikisalia nafasi ya 16 na alama tatu ikiwa haijashinda mchezo wowote msimu huu.

MBEYA, ARUSHA NBC CHAMPIONSHIP ‘KINAWAKA’ LEO.

 

MICHEZO miwili ya Ligi ya NBC Championship inachezwa leo kwenye mikoa ya Mbeya na Arusha katika muendelezo wa mzunguko wa 19.

Mkoani Mbeya KenGold vinara wa NBC Championship itawakabili Mbeya Kwanza inayoshika nafasi ya tano kwenye msimamo saa 8:00 mchana kwenye uwanja wa Sokoine.

Mkoani Arusha TMA inayoshika nafasi ya sita na alama 34 itakuwa mwenyeji wa Pan Africans inayoshika nafasi ya 14 ikiwa na alama 15 katika mchezo utakaochezwa saa 10 alasiri kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Michezo yote miwili itakuwa mubashara kwenye chaneli ya TV3 inayopatikana kwenye king’amuzi cha Startimes.

MICHEZO MITATU NBC CHAMPIONSHIP KUPIGWA LEO.

 

LIGI ya NBC Championship inarejea leo Januari 26 kwa michezo mitatu ya mzunguko wa 19 kuchezwa kwenye mikoa mitatu
tofauti.

Mapema saa 8:00 mchana Copco itawaalika Stand United kwenye uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza, Copco inashika nafasi ya 15 kwenye msimamo ikicheza jumla ya michezo 18 na kupata alama 13 huku Stand United ikishika nafasi ya tisa ikicheza jumla ya michezo 18 ikiwa na alama 22.

Mchezo wa pili utazikutanisha FGA Talents dhidi ya Green Warriors saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Mkoani Arusha Mbuni itakuwa mwenyeji wa Cosmopolitan saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Mechi zote zitakuwa mubashara kupitia chaneli za TV3 na ST BONGO zinazopatikana kwenye king’amuzi cha Startimes.

LIGI KUU YA NBC NAMBA SITA KWA UBORA AFRIKA.

SHIRIKISHO la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS) limetoa takwimu za Ligi bora duniani huku Ligi Kuu ya NBC Tanzania ikishika namba 6 barani Afrika.

Shirikisho hilo limetoa takwimu za ligi 100 ikijumuisha Bara la Afrika, Ulaya, Amerika ya Kusini, Amerika Kaskazini, Asia, Australia na Antaktiki huku Ligi Kuu ya NBC ikishika nafasi ya 62 Duniani.

Ligi Kuu ya NBC iliyokuwa nafasi ya tano mwaka jana imeshuka kwa nafasi moja mwaka huu barani Afrika ikiwa nyuma ya Misri, Morocco, Algeria, Tunisia na Afrika ya Kusini.