BAADA ya timu za KenGold, JKT Tanzania na Dodoma Jiji kuchukua alama tatu baada ya kushinda michezo yao hapo jana Ligi Kuu ya NBC inatarajiwa kuendelea tena leo kwa michezo mitatu itakayopigwa viwanja vitatu tofauti.
Mkoani Arusha timu ya Coastal Union iliyopoteza mchezo wake uliopita dhidi ya Pamba Jiji itakuwa mwenyeji wa Azam kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid saa 10:00 alasiri.
Azam inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mchezo uliopita nyumbani dhidi ya Mashujaa kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Zidane Sereri na Yoro Diaby.
Mkoani Kigoma timu ya Mashujaa iliyopoteza mchezo wake uliopita ugenini itakuwa mwenyeji wa timu ya Pamba Jiji ambayo imeshinda michezo mitatu mfululizo iliyopita bila kuruhusu bao katika michezo hiyo.
Mchezo wa mwisho utazikutanisha timu za Namungo itakayokuwa mwenyeji wa simba saa 12:30 jioni kwenye uwanja wa Mjaliwa, Lindi.
Timu ya Namungo inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusalia kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu ujao huku Simba ikihataji ushindi ili kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa msimu huu.