Author: Honest Mwanitega

IHEFU, TANZANIA PRISONS KUKIWASHA LIGI KUU YA NBC.

TIMU za Ihefu na Tanzania Prisons zinashuka uwanjani leo kwenye mchezo pekee wa Ligi Kuu ya NBC utakaochezwa kwenye uwanja wa Highland Estates, Mbeya saa 10:00 alasiri.

Ihefu inashuka uwanjani ikiwa haijashinda katika michezo saba iliyopita ikikusanya alama tisa na kushika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Tanzania Prisons inaingia uwanjani ikiwa imeshinda mchezo uliopita nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji kwa bao 1-0 na kukusanya alama 10 huku ikishika nafasi ya 13 kwenye msimamo.

GEITA YATAMBA, KAGERA IKIBANWA LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Geita Gold ya mkoani Geita imepata ushindi katika uwanja wa nyumbani wa Nyankumbu kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu baada ya kuifunga JKT Tanzania ya Dar es salaam bao 1-0.

Huu ni ushindi wa pili kwa Geita msimu huu unaowafanya kufikisha alama 10 katika nafasi ya 10 ikipoteza michezo minne na kutoa sare minne.

Kagera imeshindwa kutamba nyumbani dhidi ya KMC baada ya kulazimishwa sare ya bao moja kwenye uwanja wa nyumbani Kaitaba mkoani Kagera.

Bao namba 10 kwa KMC msimu huu lililofungwa na Waziri Junior kwenye mchezo wa leo limeifanya KMC kusalia nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na alama 16 huku bao la Kagera likifungwa na Deus Bukenya na kuwafanya Kagera kukaa nafasi ya saba ikiwa na alama 13.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena kesho Novemba 23, Tanzania Prisons ikiikaribisha Coastal union kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya saa 10:00 alasiri huku Namungo ikiwa mwenyeji wa Ihefu kwenye uwanja wa Majaliwa, Lindi saa 1:00 usiku.

YANGA YAIADHIBU SIMBA LIGI KUU YA NBC.

MABAO 5-1 walioshinda Yanga dhidi ya Simba yametosha kuwabakiza kileleni mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya NBC kwa alama 21 baada ya kucheza mechi tisa.

Mabao yaliyofungwa na Kennedy Musonda, Maxi Nzengeli aliyefunga mawili, Ki Aziz na Pacome Zouzoua yameifanya Simba kuruhusu mabao 10 huku wakifunga 17.

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha jumla ya mabao 25 kwenye michezo 9 waliyocheza mpaka sasa.

Yanga wamesalia kileleni mwa msimamo wakiwaacha wapinzani wao Simba na pointi zao 18 huku Simba wakiwa wamecheza mechi saba .

AZIZ KI KINARA WA MABAO LIGI KUU YA NBC.

MCHEZAJI Stephane Aziz Ki wa Yanga amemshusha Jean Baleke wa Simba kwenye msimamo wa vinara wa mabao baada ya kufunga mabao matatu (Hat-trick) dhidi ya timu ya Azam.

Mabao matatu aliyofunga Ki yote kwa mguu wa kushoto yamemfanya kufikisha mabao sita na kumzidi Baleke mwenye matano na Feisal Salum wa Azam mwenye mabao manne.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha alama 15 sawa na timu ya Simba na kupanda nafasi ya kwanza kwa tofauti ya mabao manne.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena Oktoba 25 kwa michezo mitatu, JKT Tanzania dhidi ya Tabora United kwenye uwanja wa Azam Complex saa 16:00, Coastal Union na Mashujaa saa 12:30 kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga na mchezo wa mwisho utachezwa uwanja wa Jamhuri saa 21:00 kati ya Dodoma Jiji na Kagera Sugar.

‘KIVUMBI’ DAR ES SALAAM DERBY LIGI KUU NBC.

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo ikikutanisha ‘miamba’ wawili wa soka kutoka mkoa wa Dar timu ya Yanga dhidi ya Azam kwenye uwanja wa Mkapa, Dar utakaochezwa saa 12:30 jioni.

Yanga ndiye kinara wa kufunga mabao mpaka sasa (15) huku akiruhusu mabao mawili sawa na Azam.

Azam imeshinda michezo minne mpaka sasa na kutoa sare mmoja ikiwa haijapoteza mchezo wowote huku Yanga ikishinda minne na kupoteza mmoja.

Yanga imeshinda michezo mitano huku Azam ikishinda mitatu na sare tatu zimepatikana miamba hiyo ilipokutana kwenye michezo 10 iliyopita.