Author: Loveness Bernard

DODOMA JIJI, PRISONS KUUMANA LEO LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Dodoma Jiji itaikaribisha Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaochezwa leo majira ya saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Mchezo huo ni muhimu kwa timu zote mbili kwani zinapambana kujinasua ‘mkiani’ Dodoma Jiji ikiwa nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kucheza michezo tisa ikishinda mchezo mmoja ,kupata sare minne na kufungwa michezo mitano .

Mchezaji wa Dodoma Jiji Mwana Kibuta

Aidha Dodoma Jiji imeruhusu mabao 10 huku ikifunga mabao matano na kuweza kukusanya alama saba katika michezo hiyo.

Kwa upande wa Tanzania Prisons inashika nafasi 14 katika msimamo ikiwa imecheza michezo saba, ikishinda michezo miwili, sare mbili na kufungwa michezo minne.

Kwa upande wa alama timu hiyo imefanikiwa kukusanya alama saba, ikifunga mabao matatu na kufungwa mabao matano katika michezo hiyo.

PRISONS WABABE WA MBEYA DABI LIGI KUU YA NBC

Mchezaji wa Mbeya City (kushoto) akichuana na mchezaji wa Tanzania Prisons

TIMU ya Tanzania Prisons imeendeleza ubabe wake katika mchezo wa dabi ya Jiji la Mbeya baada ya kuifunga timu ya Mbeya City mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa Uwanja wa KMC mkoani Dar es Salaam jana Oktoba 21.

Mchezo huo ulianza majira ya saa 10:00 alasiri ambapo timu zote zilikuwa zikipambana kupata alama tatu huku mashabiki wa timu zote mbili wakionekana kushangilia kwa bendi na ngoma zilizonogesha mchezo huo.

Mbeya City kinara wa Ligi Kuu ya NBC alianza mchezo kwa kushambulia sana lango la ‘hasimu’ wake huku Tanzania Prisons ikifanya mashambulizi ya kushtukiza na hadi timu zinaenda mapumzikoni hakuna aliyekuwa ametikisa ‘nyavu’ za mwenzake hivyo kuwapa kazi ya ziada makocha wakati wa mapumziko namna bora ya kujipanga kwa ajili ya kipindi cha pili.

Dakika ya 73 kipindi cha pili Tanzania Prisons ilipata bao la kwanza kupitia kwa Jeremiah Juma na dakika moja baadae Haruni Chanongo aliiongezea bao la pili na kufifisha matumaini ya Mbeya City kubakiza alama zote tatu nyumbani.

Tanzania Prisons wakishangilia

Dakika ya 87 Mbeya City ilipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Daniel Lukandamila hivyo mchezo kutamatika kwa Mbeya City kupoteza 1-2 na kuifanya ‘Purple Nation’ kupoteza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu.

Mchezaji wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo kutokana na kiwango kizuri alichokionyesha ikiwa ni pamoja na kuwafungia ‘Wajelajela’ bao na kuonyesha kiwango kizuri akiisaidia timu yake kushinda.

Jeremiah Juma

Matokeo hayo yanaifanya Tanzania Prisons kupanda hadi nafasi ya tano ikiwa na alama sita huku Mbeya City ikiendelea kushikilia ‘usukani’ wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na alama saba.

DIARRA,AHMAD WANG’ARA TUZO ZA SEPTEMBA.

GOLIKIPA wa timu ya Young Africans, Djigui Diarra ameng’ara baada ya kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu ya  NBC msimu wa mwaka 2025/2026, huku Ahmad Ali wa JKT Tanzania, akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.

Diarra alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Anthony Tra Bi wa Singida Black Stars na Mohamed Bakari wa JKT Tanzania alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo miwili ambayo Young Africans ilicheza na kupata ushindi kwa mchezo mmoja dhidi ya Pamba Jiji (3-0) na kupata suluhu ya (0-0) dhidi ya Mbeya City hivyo kutokuruhusu goli kufungwa kwa timu yake.

KOCHA AHMAD ALI

Kwa upande wa Ahmad Ali aliyeingia fainali na Romain Folz wa Young Africans na Miguel Gamondi wa Singida Black Stars, aliiongoza JKT Tanzania kwenye kiwango kizuri katika michezo miwili iliyocheza kwa mwezi huo wa Septemba.

JKT Tanzania ilipata sare ya bao moja dhidi ya Mashujaa wakiwa ugenini, uwanja wa Lake Tanganyika – Kigoma na kupata ushindi wa mabao mawili dhidi ya Coastal Union (1-2) wakiwa kwenye uwanja wa ugenini,Mkwakwani – Tanga

AZAM,JKT

AZAM, JKT HAPATOSHI ISAMUHYO, SIMBA IKIIKARIBISHA NAMUNGO LIGI KUU YA NBC.

MZUNGUKO wa tatu wa Ligi Kuu ya NBC unaendelea leo mkoani Dar es salaam katika viwanja viwili vya Meja Jenerali Isamuhyo na uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika mchezo wa kwanza utakaochezwa Isamuhyo majira ya saa kumi na mbili jioni timu ya JKT Tanzania inayonolewa na kocha Ahmad Ally itakuwa mwenyeji wa Azam iliyo chini ya Florent Ibenge.

JKT Tanzania

JKT inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imekusanya alama nne baada ya kushinda mchezo mmoja dhidi ya Coastal Union na kutoka sare na Mashujaa huku timu ya Azam ikishika nafasi ya tisa baada ya kukusanya alama tatu kwenye mchezo mmoja iliyocheza dhidi ya Mbeya City.

Mchezo wa pili ni kati ya Simba na Namungo utakaopigwa majira ya saa 2:15 usiku ukiwa ni mchezo wa mwisho wa kukamilisha mzunguko wa tatu.

 

Simba SC

 

Simba iliyo chini ya kocha Selemani Matola inashika nafasi ya nane katika msimamo ikikusanya alama tatu katika mchezo wao pekee waliocheza dhidi ya Fountain Gate.

Namungo FC

Namungo ambayo haijapoteza mchezo wowote hadi sasa chini ya kocha Juma Mgunda inakamata nafasi ya tano ikiwa na alama nne baada ya kutoka sare na timu ya Pamba Jiji huku ikiifunga timu ya Tanzania Prisons.

RATIBA YA LIGI KUU YA NBC MSIMU WA 2025/26 YAWEKWA WAZI.

KAIMU Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Ibrahim Mwayela ametangaza rasmi kuanza kwa Ligi Kuu ya NBC msimu 2025/2026 inayotarajiwa kufungua pazia Septemba 17 kwa michezo miwili itachezwa katika viwanja vya KMC, Dar es Salaam na Mkwakwani mkoani Tanga.

Akizungumza na waandishi wa habari Mwayela amesema kuwa maandalizi yote kuelekea kuanza kwa msimu mpya yapo tayari kwa upande wa usimamizi wa ligi Kuu ya NBC Pamoja na vilabu.

“Ligi Kuu ya NBC inarejea rasmi Septemba 17 ambapo siku hiyo kutakuwa na michezo miwili KMC itaikaribisha timu ya Dodoma Jiji katika uwanja wa KMC Complex na Coastal Union itakuwa mwenyeji wa timu ya Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga” amesema Mwayela.

“Maandalizi yapo tayari kwa upande wetu kama Bodi ya Ligi na masuala yote ya usimamizi yapo vizuri huku klabu zote 16 zikiendelea kusajili ili kujiimarisha vema tayari kwa msimu mpya. Ratiba hiyo imezingatia matukio mbalimbali ya soka yaliyopo mbele yetu ikiwemo michuano ya kimataifa na kitaifa” ameongeza Mwayela.

Mwayela amesema pamoja na hayo Ligi yetu inatarajiwa kutatamatika mei 23, 2026 ili kuruhusu wachezaji watakaopata nafasi ya kuitwa na timu zao zitakazofanikiwa kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2026.

“Ligi inatarajiwa kutamatika mei 23 ili kuruhusu wachezaji ambao timu zao za taifa zitafuzu Kombe la Dunia kwenda kujiandaa na michuano hiyo na mchezo wa watani wa jadi kati ya Young Africans na Simba ‘Kariakoo Dabi’ mzunguko wa kwanza utapigwa Disemba 13, 2025 huku mchezo wa marudiano ukipigwa April 4” amesema Mwayela.

Aidha ameongeza kuwa ubora waliouonyesha wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani yaani CHAN umetokana na uimara wa Ligi Kuu ya NBC.