Author: Loveness Bernard

CAMARA ‘ANG’ANG’ANIA’ KILELENI HATI SAFI LIGI KUU YA NBC.

GOLIKIPA wa timu ya Simba Moussa Camara ameendeleza ubabe wake kwa kuendelea kukaa kileleni kwa kuwa na hati safi (Cleansheet) nyingi (17) kuliko magolikipa wenzake wa Ligi Kuu ya NBC kwa msimu 2024/2025.

Camara ambaye ni msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu ya NBC amefanikiwa kukusanya hati safi hizo katika michezo 25 ya Ligi Kuu aliyocheza mpaka sasa huku akifanikiwa kuendelea kuwa juu ya msimamo wa hati safi huku Djigui Diarra wa Young Africans akiwa nafasi ya pili baada ya kukusanya hati safi 15.

Patrick Munthali wa Mashujaa anashikilia nafasi ya tatu akiwa na hati safi 12 huku Mohamed Mustapha wa Azam na Yona Amos wa Pamba Jiji wakiwa nazo 10 kila mmoja.

Yakoub Suleiman wa JKT Tanzania nae hayuko mbali akiwa amefanikiwa kukusanya hati safi 8 huku Metacha Mnata wa Singida Black Stars na Ngaleka Katembua wa Dodoma Jiji wakiwa wamefanikiwa kukusanya hati safi 7 kila mmoja huku ikisalia mizunguko miwili kutamatika kwa msimu wa 2024/25.

YOUNG AFRICANS YASHIKILIA ‘USUKANI’ LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC inazidi kushika kasi Iikielekea ukingoni huku timu ya Young Africans ikiendelea ilipoishia baada ya kuichapa Namungo 3-0 kwenye uwanja wa KMC Complex mkoani Dar es Salaam.

Ilimchukua dakika 27 kiungo wa Young Africans Aziz Ki kufungua ukurasa wa mabao na dakika nne baadae mshambuliaji wa timu hiyo raia wa Zimbabwe Prince Dube aliipatia timu yake bao la pili hivyo kwenda mapumziko ikiongoza 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi timu ya Namungo ikionekana kusaka namna ya kupata bao ambapo juhudi zao hazikuzaa matunda na dakika ya 74 mchezaji wa Young Africans Maxi Nzegeli aliipatia timu yake bao la tatu na mpaka dakika 90 zinatimia ubao wa matokeo ulikuwa unasoma 3-0.

Matokeo hayo yanaifanya Young Africans kufikisha alama 73 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu ya NBC huku timu hiyo ikisaliwa na michezo mitatu kuhitimisha Ligi hiyo.

Mchezaji wa Young Africans Maxi Nzegeli alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kutokana na kiwango kizuri alichoonyesha katika mchezo huo akifunga bao na kutoa pasi ya bao la Stephane Aziz Ki.

LIGI KUU NBC KAZINI VIWANJA VINNE LEO.

BAADA ya kupigwa michezo miwili jana Ligi Kuu ya NBC inaendelea leo kwa michezo minne ya mzunguko wa 28 katika viwanja vinne tofauti .

Mchezo wa kwanza utapigwa majira ya saa 8:00 mchana katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni Dar es Salaam ambapo JKT Tanzania itaikaribisha timu ya Fountain Gate kutoka Manyara.

Saa 10:00 alasiri itapigwa michezo miwili ambapo mchezo wa kwanza ni kati ya Young Africans ikiwaalika Namungo katika uwanja wa KMC Complex mkoani Dar es Salaam na KenGold itaikaribisha Pamba Jiji katika uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.

Mchezo wa mwisho utachezwa saa 1:00 usiku ambapo timu ya Azam itakuwa mwenyeji wa timu ya Dodoma Jiji katika uwanja wa Azam Complex, Dar.

KAGERA SUGAR ‘HATIHATI’ KUSHIRIKI LIGI KUU YA NBC MSIMU UJAO.

MATUMAINI ya wapenzi na mashabiki wa timu ya Kagera Sugar kusalia Ligi Kuu ya NBC yamezidi kufifia baada ya kufungwa na timu ya Mashujaa katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera jana kwa bao 1-0.

Timu hiyo imeshacheza michezo 28 ya Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/25 na kufanikiwa kuvuna alama 22 ikifunga mabao 22 na kuruhusu mabao 40 huku ikiwa imebakisha michezo miwili kumaliza msimu.

Aidha timu hiyo endapo ikishinda michezo yote iliyobakia itaweza kufikisha alama 28 ikiwa ni tofauti ya alama moja na Pamba Jiji ambayo ina alama 27 ikifunga mabao 18 na kufungwa mabao 32 huku ikiwa imebaki michezo mitatu mkononi.

Endapo Pamba Jiji itashinda mchezo wa leo dhidi ya KenGold rasmi Kagera Sugar itashuka daraja na kushiriki Ligi ya Championship ya NBC.

PRISONS YATAKATA SOKOINE LIGI KUU YA NBC

LIGI Kuu ya NBC imeendelea mkoani Mbeya ambapo timu ya Tanzania Prisons iliikaribisha timu ya Coastal Union katika uwanja wa Sokoine na kukusanya alama zote tatu baada ya ushindi wa 2-1.

Mchezo huo ulianza saa 10:00 alasiri timu zote zilionyesha ari ya kupambania alama tatu muhimu ili kuweza kujiweka katika mazingira ya kusalia Ligi Kuu ya NBC msimu ujao.

Iliwachukua dakika 27 timu ya Tanzania Prisons kufungua ukurasa wa mabao kupitia mchezaji wao Ezekia Mwashilindi hivyo kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa inaongoza kwa 1-0.

Kipindi cha pili kilianza ambapo Coastal Union walionekana kuliandama zaidi lango la Prisons hata hivyo juhudi zao zilizimwa na mchezaji Beno Ngasa aliyeongeza bao la pili kwa timu yake dakika ya 74.

Dakika ya 89 Coastal Union ilipata bao la kufutia machozi kupitia mchezaji wao Bakari Msimu hivyo mchezo kutamatika kwa matokeo ya 2-1.

Tanzania Prisons ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imevuna alama 30 katika michezo 28 huku Coastal Union ikiwa nafasi ya 9 na alama 31 katika michezo 28 ya Ligi Kuu msimu wa 2024/2025.