Author: Loveness Bernard

CAMARA MKALI WA ‘HATI SAFI’ LIGI KUU YA NBC.

GOLIKIPA wa timu ya Simba, Moussa Camara ameendeleza moto wake wa kuongoza kwa kuwa na hati safi nyingi kuliko magolikipa wengine wa timu za Ligi Kuu ya NBC akiwa hajaruhusu bao kwenye michezo 16 akiwa kwenye msimu wa kwanza ndani ya Simba.

Camara mpaka sasa amecheza michezo 24 sawa na dakika 2160 huku timu yake ya Simba ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo nyuma ya Young Africans inayoshikilia usukani.

Golikipa wa Young Africans,Djigui Diarra anafuatia akiwa amecheza dakika 1819 katika michezo 20 ya Ligi Kuu ya NBC amefanikiwa kukusanya hati safi 14.

Patrick Munthali wa timu ya Mashujaa kutoka Kigoma anashika nafasi ya tatu akiwa amefanikiwa kukusanya hati safi 12 huku Mohamed Mustapha wa timu ya Azam akishika nafasi ya nne na hati safi 10.

Nafasi ya tano inashikiliwa na Yona Amos wa Pamba Jiji aliyefanikiwa kukusanya hati safi tisa huku Yakoub Suleiman wa JKT Tanzania amekusanya hati nane akishika nafasi ya sita.

Metacha Mnata wa Singida Black Stars na Ngaleka Katembua wa Dodoma Jiji wanafunga orodha wakifanikiwa kukusanya hati safi saba kila mmoja.

AHOUA MKALI WA ‘KUCHEKA NA NYAVU’ LIGI KUU YA NBC.

KIUNGO wa timu ya Simba Jean Ahoua ameendelea kujiimarisha kwenye mbio za ufungaji bora baada ya kufikisha mabao 15 ikiwa ni msimu wake wa kwanza tangu ajiunge na timu hiyo kwenye Ligi Kuu ya NBC.

Ahoua amefanikiwa kufunga mabao hayo akiwa amecheza mechi 24 kwa jumla ya dakika 1773 katika Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025.

Clement Mzize wa Young Africans anafuata akiwa amefanikiwa kufunga mabao 13 huku mchezaji mwenzake Prince Dube wa timu hiyo akifanikiwa kucheka na nyavu za wapinzani wao mara 12 sawa na Leonel Ateba wa Simba.

Steven Mukwala wa Simba na Jonathan Sowah wa Singida Black Stars wamefanikiwa kufunga mabao 11 kila mmoja huku Elvis Rupia wa Singida Black Stars akitupia nyavuni mabao 10.

SIMBA ‘YAIBAMIZA’ KMC LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC imeendelea leo kwa mchezo mmoja uliochezwa uwanja wa KMC Complex, mkoani Dar es Salaam kati ya KMC ikiikaribisha timu ya Simba na kushuhudia ‘Mnyama’ akishinda 1-2 ugenini.

Mchezo huo ulianza majira ya saa kumi alasiri kwa timu zote kuwa na ari ya kuzitaka alama tatu muhimu KMC ikitaka kujihakikishia nafasi ya kusalia Ligi Kuu ya NBC msimu ujao huku Simba ikijiimarisha kwenye mbio za ubingwa.

Dakika nane ziliitosha timu ya KMC kufungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Rashid Chambo kabla ya timu ya Simba kusawazika kupitia mshambuliaji wake Steven Mukwala dakika ya 15 ya mchezo na dakika 46 aliongeza bao la pili hivyo mchezo kumalizika kwa 1-2.

Simba imefikisha alama 69 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikifunga mabao 62 na kuruhusu mabao 11 katika michezo 26 ambayo timu hiyo imecheza huku KMC ikiwa nafasi ya 11 na alama 30 ikifunga mabao 23 na kuruhusu mabao 41 katika michezo 27 ambayo timu hiyo imeshacheza.

MTIBWA SUGAR MABINGWA LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC 2024/2025.

TIMU ya Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2024/2025.

Mtibwa Sugar kwenye mchezo wake wa mwisho hii Leo dhidi ya Kiluvya iliyochezwa kwenye uwanja wa Manungu Complex imefanikiwa kuibuka na kushinda wa mabao 2-0 myaliyofungwa na Raizin Hafidh dakika ya 36 na 46 ya mchezo huo.

Baada ya ushindi huo Mtibwa Sugar inafikisha alama 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote inayoshiriki Ligi ya Championship ya NBC.

Mtibwa Sugar ambayo ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu ya NBC msimu uliopita imefanikiwa kufunga mabao 58 huku ikifungwa mabao 18 hivyo kujihakikisha nafasi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026.

AHOUA HASHIKIKI, SIMBA IKIWASHA MOTO LIGI KUU YA NBC

UTAMU wa Ligi namba nne kwa ubora barani Afrika unazidi kukolea timu ya Simba ikiichapa timu ya Pamba Jiji kutoka jijini Mwanza mabao 5-1.

Mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa KMC uliopo Mwenge mkoani Dar es Salaam ulishuhudia kiungo wa timu ya Simba Jean Ahoua akifunga Mabao matatu (Hat-Trick).

ilimchukua dakika 16 kufungua ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penati kabla ya kurejea wavuni tena dakika ya 37 hivyo kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiongoza 2-0 dhidi ya Pamba Jiji.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Ahoua aliongeza bao la tatu hivyo kukamilisha hat-trick dakika ya 48 ya mchezo na mshambuliaji Leonel Ateba aliongeza mabao mawili kwa timu yake ikiwa ni dakika ya 80 na 82 ya mchezo huo huku mchezaji wa Pamba Jiji.

Mathew Momanyi alifunga bao la kufutia machozi kwa timu yake ya Pamba dakika ya 86 hivyo mchezo huo kumalizika 5-1.

Ushindi huo unaifanya timu ya Simba kufikisha alama 66 ikiendelea kusalia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu huku Jean Ahoua akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.