Author: Loveness Bernard

HAPATOSHI NBC CHAMPIONSHIP

Ligi ya NBC Championship inazidi kushika kasi ambapo mizunguko tisa imeshachezwa mpaka sasa kwa timu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo ambayo kila timu imeonekana ikipambana kuhakikisha inapanda daraja msimu ujao.

Mtibwa Sugar ndio wanaongoza msimamo wakiwa na alama 20 wakiwa wamefunga mabao 15 na kufungwa manne sambamba na Geita Gold wakiwa na alama 20 huku wakiwa wamefunga mabao 11 na kuruhusu manne.

Timu za TMA,Songea United,Mbeya City na Stand United kila moja imevuna alama 18 huku TMA wakifunga mabao 15 na kuruhusu nane, Songea wamefunga 12 na kuruhusu saba, Mbeya City imefunga mabao 15 ikiruhusu 11 na Stand United imefunga nane ikiruhusu mabao saba.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena Novemba 22 kwa michezo miwili, Transit Camp itakuwa mwenyeji wa Mbeya Kwanza huku timu ya BigMan itaikaribisha Kiluvya kwenye mchezo wa pili.

“UGUMU WA LIGI KUU YA NBC UNATUPA CHACHU KUPAMBANA ZAIDI” ANTONY MLIGO.

MCHEZAJI wa Namungo Anthony Mligo amesema kuwa ubora wa Ligi Kuu ya NBC umefanya ligi hiyo kuwa ngumu kutokana na kila timu kupambana kuhakikisha inapata matokeo ya ushindi.

Akizungumza wakati wa siku ya kuongea na vyombo vya Habari kwa timu ya Namungo, Mligo amesema kuwa Ligi ya NBC imekuwa ngumu na hili linajidhihirisha ubora wake kutokana na ubora uliosababishwa na ligi hiyo kupanda viwango vya ubora barani Afrika.

“Timu nyingi zipo vizuri kwa sababu zina wachezaji wazuri ndio maana ushindani ni mkubwa hivyo sisi tunaendelea kupambana japokuwa hali yetu sio nzuri “Amesema Mligo.

“Sisi kama wachezaji tunaendelea kujituma na tusikate tamaa kwani Kocha anajua nini anatakiwa kutupatia ili tuweze kurejesha ubora wetu na kuifanya timu yetu irudi kuwa imara zaidi’’ Aliongeza.

Aidha mchezaji huyo amesema kuwa ushindani wa namba uliopo Namungo unamfanya azidi kupambana zaidi ili aweze kuwa chaguo namba moja la kocha na kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.

“Kwenye kila timu kuna ushindani wa namba hivyo mimi sihofii ushindani bali nachukulia kama chachu yakupambana zaidi ili niweze kuzidi kupata nafasi ya kucheza kwani mchezaji anaecheza nae nafasi moja ni mzuri pia.

Tukio ambalo mchezaji huyo hawezi kulisahau amesema ni wakati akianza kucheza alipata timu ya Ligi daraja la pili Zanzibar akaenda kucheza lakini ukata wa timu hiyo ulimfanya afyeke majani katika eneo la Fumba ili aweze kupata nauli ya kurudi nyumbani Pamoja na pesa ya kujikimu.

“Nilipohitimu kidato cha nne nilimwomba Mama aniruhusu niende nikacheze Zanzibar ligi daraja la pili kwa bahati mbaya timu hiyo ilikuwa na ukata ilinilazimu kuacha mpira nikajikuta nafyeka majani ili niweze kupata mahitaji yangu na pesa ya nauli ya kurudi nyumbani Tanga mpaka sasa sijawahi kumwambia Mama kilichonikuta kwani alijua nilikuwa nacheza huko” Alisema Mligo.

SIMBA, AZAM TIMU ZILIZORUHUSU MABAO MACHACHE LIGI KUU NBC

Ligi Kuu ya NBC inaendelea kushika kasi ambapo mpaka sasa mizunguko 9, 10 na 11 kwa baadhi ya tmu imeshachezwa.

Timu za Simba na Azam ndio timu pekee zilizoruhusu mabao machache mpaka sasa ambapo kila moja imeruhusu mabao matatu tu.

Simba imeruhusu mabao hayo katika michezo miwili dhidi ya Yanga ikifungwa goli moja na mchezo dhidi ya Coastal Union ambapo ilitoka sare ya bao 2-2.

Kwa upande wa timu ya Azam imeruhusu mabao hayo matatu kwenye michezo miwili dhidi ya KenGold ambapo iliruhusu bao moja huku mchezo ukiisha kwa Azam kushinda 4-1 na mchezo dhidi ya Simba ambapo ilifungwa mabao 2-0.

Yanga na Singida Black Stars ndio wanafuatia kuruhusu mabao machache ambapo mpaka sasa wameruhusu mabao manne tu kwenye Ligi Kuu ya NBC.

Yanga imeruhusu mabao hayo baada ya kufungwa na Azam bao moja lililofungwa na mchezaji Gibril Sillah kisha kufungwa na timu ya Tabora United 1-3.

TCHAKEI MCHEZAJI BORA OKTOBA, TAOUSSI AWABWAGA MOALLIN NA KITAMBI.

Mshambuliaji wa Singida Black Stars Marouf Tchakei amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Oktoba wa Ligi Kuu ya NBC huku Kocha wa Azam Rachid Taoussi akichaguliwa kuwa kocha bora wa mwezi huo.

Tchakei amewashinda Lusajo Mwaikenda wa Azam na Pacome Zouzoua wa Yanga alioingia nao fainali za tuzo hizo baada ya kufunga mabao 3 na kutoa pasi ya mwisho moja katika dakika 360 alizocheza ndani ya mwezi huo.

Singida imeshinda dhidi ya Mashujaa 1-0, Namungo 2-0,Fountain Gate 2-0 na kufungwa 1-0 katika mchezo wao dhidhi ya Yanga.

Aidha Kocha wa Azam Rachid Taoussi amefanikiwa kuwa kocha Bora wa mwezi huo baada ya kuwashinda Abdulhamid Moallin wa KMC na Denis Kitambi wa Singida Black Stars baada ya kushinda michezo mitatu ambayo timu yake ilicheza ndani ya mwezi huo.

Azam walishinda dhidi ya Namungo 1-0, Tanzania Prisons 2-0 na KenGold 4-1 hivyo kupanda kutoka nafasi ya tano hadi ya nne ya msimamo wa ligi hiyo.

Kamati ya Tuzo pia imemchagua Meneja wa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Godwin Israel kuwa Meneja bora kutokana na usimamizi mzuri wa matukio ya michezo na masuala ya miundombinu.

Kwa upande wa Ligi ya NBC Championship kamati imemchagua mchezaji wa Geita Gold Andrew Simchimba kuwa mchezaji bora wa Ligi hiyo baada ya kufunga mabao manne na kutoa pasi ya mwisho moja akiwashinda Adam Oseja wa Geita Gold na Jaffar Maneno wa TMA alioingia nao fainali.

Naye Kocha wa Geita Gold, Amani Josiah amechaguliwa kuwa kocha bora wa ligi hiyo kwa mwezi oktoba ambapo aliiongoza timu yake kushinda michezo minne na kufanikiwa kupanda kutoka nafasi ya tisa mpaka ya kwanza katika msimamo wa ligi hiyo.Bonyeza kiuganishi hapa chini kuona video hiyo WASHINDI WA TUZO ZA MWEZI OKTOBA LIGI KUU YA NBC NA LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC.

MWALIMU KINARA WA TUZO LIGI YA NBC.

Mchezaji wa Fountain Gate Seleman Mwalimu ameendelea kuwa mwiba kwa mabeki wa timu za Ligi Kuu ya NBC kutokana na kufunga mabao sita hivyo kuwa mshambuliaji hatari zaidi awapo langoni mwa mpinzani.

Licha ya kuongoza kwa idadi kubwa ya mabao pia Mwalimu anaongoza kuwa na tuzo nyingi kuliko mchezaji yoyote wa Ligi hiyo baada ya kufikisha tuzo tano.

Mwalimu amefanikiwa kuwa mchezaji bora wa michezo minne tofauti ya Fountain Gate dhidi ya KMC, Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na KenGold.

Aidha Mwalimu alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi septemba hivyo kumfanya kuwa mchezaji mwenye tuzo tano katika Ligi Kuu ya NBC.