Author: Yahaya Abushehe

MBEYA KWANZA YAIBAMIZA BIASHARA NBC CHAMPIONSHIP IKIENDELEA.

 

LIGI ya NBC Championship imeendelea leo Machi 24, 2024 kwa michezo miwili kuchezwa kwenye mikoa ya Mtwara na Morogoro.

Mkoani Mtwara saa 10:00 alasiri Mbeya Kwanza ikaibamiza Biashara United kwa bao 1-0 kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona, bao pekee la Mbeya Kwanza likifungwa na Magata Charles Dakika ya 90+4 ya mchezo.

Kwa Matokeo haya Mbeya Kwanza inapanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo ikifikisha alama 53 sawa na Biashara United ikizidiwa utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa Biashara ikiwa na 29 huku Mbeya Kwanza ikiwa na 17.

Mchezo mwengine ukazikutanisha Transit Camp dhidi ya Cosmopolitan saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Jamhuri, Morogoro na kumalizika kwa Transit Camp kufungwa 1-2 mbele ya Cosmopolitan.

Mzunguko wa 26 utamatika kesho kwa mchezo Kati ya Green Warriors dhidi ya Pan Africans kwenye uwanja wa Mabatini mkoani Pwani sa 10:00 alasiri.

KENGOLD, PAMBA HAKUNA MBABE NBC CHAMPIONSHIP.

MICHEZO mitatu ya Ligi ya NBC Championship imechezwa leo kwenye viwanja mbalimbali ndani ya mikoa mitatu tofauti.

Mchezo wa mapema zaidi leo ulichezwa mkoani Arusha Kati ya Polisi Tanzania na Mbuni kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kumalizika kwa Polisi kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Mchezo uliosubiriwa kwa hamu zaidi leo Ken Gold dhidi ya Pamba uliopigwa kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya umemalizika kwa sare ya mabao 2-2 hivyo kila timu kugawana alama na kubaki kwenye nafasi zao.

Mchezo mwengine wa saa 10:00 alasiri Kati ya Copco na Mbeya City kwenye uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza umemalizika kwa sare ya mabao 2-2.

KENGOLD, PAMBA HAPATOSHI NBC CHAMPIONSHIP LEO.

 

MZUNGUKO wa 26 wa Ligi ya Championship ya NBC unaendelea tena leo kwa michezo mitatu na itakayorushwa mubashara kupitia chaneli za TV3 na ST BONGO ndani ya king’amuzi cha StarTimes.

Mapema saa 8:00 mchana Polisi Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mbuni kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.

Mchezo unaosubiriwa kwa hamu leo ni kati ya Ken Gold na Pamba utakaopigwa saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.

Mchezo huu unatazamwa sana kutokana na nafasi ya kila timu kwenye msimamo Ken Gold ikiwa nafasi ya kwanza na Pamba ikiwa nafasi ya pili huku timu hizo zikipishana kwa alama tano.

Ken Gold inahitaji ushindi kwenye mchezo Huu ili kuzidi kujikita kileleni na kuendelea kushikilia rekodi yake ya kutopoteza mchezo wowote nyumbani huku Pamba ikihitaji ushindi ili kupunguza utofauti wa alama uliopo.

Mchezo wa mwisho leo utapigwa saa 10:00 alasiri ukizikutanisha Copco dhidi ya Mbeya City kwenye uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza.

YANGA, SIMBA ZAENDELEZA REKODI LIGI KUU YA NBC.

 

TIMU za Yanga na Simba zinashikilia rekodi za kipekee hadi hivi sasa kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu 2023/2024 zinapocheza viwanja vya nyumbani na ugenini kwa timu hizi.

Yanga ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wowote wa nyumbani kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu katika michezo 10 ya nyumbani Kati ya 20 iliyocheza mpaka sasa.

Simba inashikilia rekodi ya kutopoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu 2023/24 kwenye uwanja wa ugenini kwenye michezo 9 iliyocheza ugenini Kati ya 19.

Timu zote mbili Simba na Yanga zimepoteza michezo miwili kila mmoja ambapo Yanga ilipoteza dhidi ya Ihefu kwa mabao 2-1 Highland Estates mkoani Mbeya na 2-1 pia dhidi ya Azam FC kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa huku Simba ikipoteza dhidi ya Yanga 5-1 uwanja wa Benjamin Mkapa na 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons mkoani Morogoro.

KIPRE JR KINARA WA PASI ZA MABAO LIGI KUU YA NBC.

 

JUMLA ya mabao 364 yameshafungwa hadi hivi sasa kwenye Ligi Kuu ya NBC huku jumla ya wachezaji 137 wakihusika kwenye kuyatengeneza mabao hayo.

Kipre JR ndiye kinara wa kutoa pasi za mabao akifanya hivyo mara nane kwenye mabao 47 ya Azam FC msimu huu.

Kouassi Yao na Stephane Aziz Ki wanafuatia kila mmoja akitoa pasi saba za mabao na kuwa na jumla ya pasi 14 za mabao kwenye mabao 49 ya Yanga msimu huu.

Clatous Chama wa Simba, Feisal Salum wa Azam, Impiri Mbombo wa Tabora, Rahimu Shomari na Awesu Awesu wa KMC wanafuatia kila mmoja akitoa pasi 5 za mabao.