Author: Yahaya Abushehe

KAGERA SUGAR, YANGA HAKUNA MBABE.

 

LIGI KUU ya NBC imerejea leo kwa mchezo mmoja uliopigwa kati ya kagera Sugar na Yanga katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera na kumalizika kwa suluhu.

Kwa matokeo haya Kagera Sugar inapanda kwa nafasi moja kutoka 14 hadi 13 baada ya kufikisha alama 14 kwenye michezo 14 huku Yanga ikiendelea kusalia nafasi ya 2 ikiwa na alama 31 kwenye michezo 12.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa mchezo mmoja kati ya Mashujaa na Simba kwenye uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

LADHA ZA LIGI KUU YA NBC KUREJEA LEO.

 

LIGIKUU ya NBC inarejea leo Februari 2 baada ya kusimama kwa takribani siku 40 kupisha fainali za mataifa ya Afrika.

Mchezo mmoja utapigwa leo Kagera Sugar ikiikaribisha Yanga kwenye uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera saa 10:00 alasiri.

Kagera Sugar inaingia kwenye huu mchezo ikiwa nafasi ya 14 kwenye msimamo baada ya kukusanya alama 13 kwenye michezo 13 huku Yanga ikiwa nafasi ya pili baada ya kujikusanyia alama 30 kwenye michezo 11.

Kagera inashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wake uliopita wa Ligi Kuu ya NBC kwa mabao 4-0 dhidi ya Azam nyumbani huku Yanga ikishinda mchezo wake uliopita kwa bao 1 lililofungwa na Stephane Aziz Ki dhidi ya Tabora United ugenini.

MBEYA, ARUSHA NBC CHAMPIONSHIP ‘KINAWAKA’ LEO.

 

MICHEZO miwili ya Ligi ya NBC Championship inachezwa leo kwenye mikoa ya Mbeya na Arusha katika muendelezo wa mzunguko wa 19.

Mkoani Mbeya KenGold vinara wa NBC Championship itawakabili Mbeya Kwanza inayoshika nafasi ya tano kwenye msimamo saa 8:00 mchana kwenye uwanja wa Sokoine.

Mkoani Arusha TMA inayoshika nafasi ya sita na alama 34 itakuwa mwenyeji wa Pan Africans inayoshika nafasi ya 14 ikiwa na alama 15 katika mchezo utakaochezwa saa 10 alasiri kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Michezo yote miwili itakuwa mubashara kwenye chaneli ya TV3 inayopatikana kwenye king’amuzi cha Startimes.

MICHEZO MITATU NBC CHAMPIONSHIP KUPIGWA LEO.

 

LIGI ya NBC Championship inarejea leo Januari 26 kwa michezo mitatu ya mzunguko wa 19 kuchezwa kwenye mikoa mitatu
tofauti.

Mapema saa 8:00 mchana Copco itawaalika Stand United kwenye uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza, Copco inashika nafasi ya 15 kwenye msimamo ikicheza jumla ya michezo 18 na kupata alama 13 huku Stand United ikishika nafasi ya tisa ikicheza jumla ya michezo 18 ikiwa na alama 22.

Mchezo wa pili utazikutanisha FGA Talents dhidi ya Green Warriors saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Mkoani Arusha Mbuni itakuwa mwenyeji wa Cosmopolitan saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Mechi zote zitakuwa mubashara kupitia chaneli za TV3 na ST BONGO zinazopatikana kwenye king’amuzi cha Startimes.

HAWA HAPA VINARA WA MABAO NBC CHAMPIONSHIP.

 

Jumla ya mabao 329 yameshafungwa katika michezo 144 sawa na mizunguko 18 ya Ligi ya NBC Championship mpaka kufikia sasa.

Edger William wa KenGold ndiye kinara wa upachikaji mabao ndani ya Ligi ya NBC Championship akifunga mabao 15 huku timu yake ikifunga mabao 32.

Boban Bogere wa Biashara United ndiye anayefuatia akifunga mabao 13 kwenye mabao 32 yaliyofungwa na timu yake.

Ramadhani kapera aliyekuwa Mbeya Kwanza kabla ya kutimkia Geita Gold inayoshiriki Ligi Kuu ya NBC na Salim Aiyee aliyekuwa timu ya Mbuni kabla ya kujiunga na Coastal Union ya Ligi Kuu ya NBC wanafuata kila mmoja akifunga mabao 9.