Author: Yahaya Abushehe

TABORA YATAMBA NYUMBANI, AZAM YAPANDA KILELENI LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Tabora United imeendelea na wimbi la matokeo mazuri ikicheza uwanja wa nyumbani baada ya Leo kuifunga Dodoma Jiji mabao 2-1 katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

Tabora imekusanya jumla ya alama nane na kushika nafasi ya tano huku ikiwa timu ya tatu kwa kufunga mabao mengi kwenye uwanja wa nyumbani (matano) sawa na timu ya Azam.

Timu ya Azam imepanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuifunga Coastal Union bao 1-0 kwenye uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.

Bao pekee na la ushindi la Azam limefungwa na Feisal Salum dakika 44 ya mchezo.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa michezo miwili Kati ya KMC na Ihefu saa 10 alasiri katika uwanja wa Uhuru, Dar huku mchezo wa pili utazikutanisha Geita Gold dhidi ya Yanga saa 10:00 alasiri katika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza.

VITA YA WABABE WA NBC CHAMPIONSHIP NDANI YA LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI Kuu ya NBC itaendelea leo kwa michezo miwili kwenye mikoa ya Shinyanga na Dodoma.

Wababe wawili wa ligi ya NBC Championship msimu uliopita JKT Tanzania na Mashujaa wanakutana kwa mara ya kwanza ndani ya Ligi Kuu ya NBC katika uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga saa 10:00 alasiri.

JKT Tanzania imeshinda mchezo mmoja huku ikifungwa michezo miwili na kupata sare mchezo mmoja na Mashujaa ikianza vizuri msimu bila kufungwa mchezo na wala kuruhusu bao na ikishinda michezo miwili na kupata sare michezo miwili.

Dodoma Jiji watakuwa wenyeji wa Azam FC katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma saa 1:OO usiku katika mchezo wa pili leo.

Azam imeshinda michezo yote mitatu ya Ligi Kuu NBC msimu huu ikiwa na alama tisa katika nafasi ya tatu huku Dodoma ikishinda mchezo mmoja, sare moja na kufungwa moja ikiwa na alama nne huku ikishika nafasi ya saba kwenye msimamo.

LIGI KUU YA NBC YAENDELEA COASTAL, JKT ZABANWA NYUMBANI.

 

LIGI Kuu ya NBC imeendelea leo kwa michezo miwili, JKT Tanzania wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani CCM Kambarage mkoani Shinyanga wametoka sare ya bao moja na Kagera Sugar.

Bao la JKT lilifungwa na Danny Lyanga Dakika ya 90+6 kwa mkwaju wa penati huku bao la Kagera Sugar likifungwa na Gasper Mwaipasi dakika ya 90+8.

Ukiwa mchezo wao wa kwanza katika uwanja wa Nyumbani Mkwakwani, Coastal Union imetoka suluhu dhidi ya Tabora United.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena kesho Septemba 30 kwa michezo miwili, Geita Gold watawaalika KMC huku Namungo wakicheza na Mashujaa.

COASTAL, JKT KUANZA NYUMBANI LEO LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI Kuu ya NBC inarejea leo Septemba 29 kwa michezo miwili kuchezwa kwenye mikoa ya Tanga na Shinyanga.

JKT Tanzania watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar katika uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga saa 10 alasiri huku ukiwa mchezo wa kwanza wa JKT Tanzania kucheza nyumbani tangu kupanda Ligi Kuu ya NBC msimu huu wa 2023/2024.

Coastal Union itacheza kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga saa 1:00 usiku dhidi ya Tabora United huku Coastal ikiwa haijapata ushindi wowote msimu huu.

SIMBA, AZAM HAZIKAMATIKI

Ligi Kuu ya NBC imeendelea leo Septemba 21 kwa michezo miwili kuchezwa katika viwanja viwili na kushuhudiwa Simba wakiifunga Coastal Union ya Tanga mabao 3-0 kwenye uwanja wao wa nyumbani Uhuru mkoani Dar es salaam.

Mabao yote matatu ya Simba yamefungwa na mchezaji Jean Baleke huku akiingia katika rekodi ya kuwa mchezaji wa pili kufunga mabao matatu kwenye mchezo mmoja ‘Hat-trick’ katika Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2023/2024 sambamba na Feisal Salum aliyefunga idadi hiyo ya mabao dhidi ya Tabora United.

Azam FC waliwaalika Singida BS katika uwanja wa Azam Complex na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 yaliyofungwa na Cheikh Sidibe na Iddi Selemani ‘Nado’ huku la Singida BS likifungwa na Marouf Tchakei.

Ligi hiyo itaendelea tena Septemba 29 kwa michezo miwili kuchezwa Kati ya JKT Tanzania na Kagera Sugar wakati mchezo wa pili Coastal Union watawaalika Tabora United.