Category: STORY

MTIBWA YAENDELEA KUSOTA LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Mtibwa Sugar imeendelea kusota bila kupata ushindi katika Ligi Kuu ya NBC kwa kushindwa kutamba kwenye uwanja wa Manungu, Morogoro baada ya kupoteza kwa mabao 0-2 dhidi ya Kagera Sugar.

Mabao yaliyofungwa na Ally Nassoro na Said Omary yameifanya mtibwa kusalia nafasi ya mwisho ikiwa haijafanikiwa kushinda mchezo wowote msimu huu.

Mtibwa imefungwa mabao 12 mpaka sasa huku ikiwa timu iliyofungwa mabao mengi baada ya kucheza michezo sita.

Ligi hiyo itaendelea tena Oktoba 21 kwa michezo mitatu kati ya Geita Gold na Dodoma saa 8:00 mchana kwenye uwanja wa Nyankumbu, Geita na Ihefu dhidi ya Coastal Union saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Highland estates, Mbeya huku katika uwanja wa Majaliwa, Lindi saa 1:00 usiku timu ya Namungo itakuwa mwenyeji wa Singida BS.

WAKALI WA NAMBA LIGI KUU YA NBC.

IKIELEKEA kuanza kwa mzunguko wa sita Ligi Kuu ya NBC tayari imeshuhudia mabao 89 huku 54 yakifungwa kwa mguu wa kulia, 27 mguu wa kushoto huku nane yakifungwa kwa kichwa.

Jean Baleke wa Simba amefunga mabao matano na kuwa kinara akifuatiwa na Feisal Salum wa Azam mwenye mabao manne huku Pacome Zouzoua, Aziz Ki, Maxi Nzengeli wa Yanga na Matheo Anthony wa Mtibwa Sugar wakifuatia na mabao matatu kila mmoja.

Idrisu Abdulai wa Azam na Djigui Diarra wa Yanga ndio makipa pekee waliofanikiwa kumaliza michezo mitatu bila kuruhusu bao lolote mpaka mzunguko wa tano kutamatika.

Yao Kouassi wa Yanga ndio kinara wa kutoa pasi zilizozaa mabao (tatu) huku akiwa na bao moja alilofunga dhidi ya JKT Tanzania kwenye uwanja wa Azam Complex.

Simba ndio timu ya kwanza kushinda michezo mitano mfululizo huku ikiongoza msimamo wa Ligi Kuu ya NBC kwa alama 15.

UCHAGUZI MDOGO BODI YA LIGI KUU TANZANIA RASMI DISEMBA 9.

Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Imetangaza uchaguzi mdogo wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania utakaofanyika Disemba 9, 2023 Jijini Dar es Salaam.

Nafasi zinazogombewa ni Mjumbe mwakilishi wa Klabu za Ligi Kuu ya NBC na Mjumbe mwakilishi wa Klabu za NBC Championship huku Mgombea lazima awe Rais au Mwenyekiti wa Klabu.

Fomu za uchaguzi zitatolewa kuanzia Oktoba 13 hadi 17 katika Ofisi za TFF na tovuti ya TFF na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Gharama za fomu ni Sh.100,000 (Laki moja) za kitanzania.

@election press TPLB

election calendar TPLB 2023

Fomu No. 1 ya uchaguzi TPLB

 

SIMBA HAIJAPATA MBABE LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Simba imeanza msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2023/24 kibabe ikiwa haijafungwa wala kutoa sare mchezo wowote mpaka mzunguko wa tano kukamilika.

Simba imeshinda michezo miwili nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji kwa mabao 2-0 na Coastal Union mabao 3-0 huku ikishinda michezo mitatu ya ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar mabao 2-4, 1-3 dhidi ya Tanzania Prisons, 1-2 dhidi ya Singida BS.

Simba inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya NBC huku ikishika nafasi ya pili kwa kufunga mabao (14) nyuma ya timu ya Yanga yenye mabao (15).

BALEKE AONGOZA MBIO ZA UFUNGAJI LIGI KUU YA NBC.

MBIO za kuwania kiatu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2023/24 zimeendelea kupamba moto huku michezo mitano ikiwa imekamilika kwa kila timu.

Jean Baleke wa Simba ndiye kinara wa ufungaji akiwa na mabao matano huku akifanikiwa kufunga mabao matatu kwenye mchezo mmoja (Hat-Trick) dhidi ya Coastal Union.

Feisal Salum wa Azam anashika nafasi ya pili akiwa na mabao manne huku akiwa amefunga mabao matatu katika mchezo mmoja dhidi ya Tabora United kwenye mchezo wa ufunguzi.

Pacome Zouzoua, Ki Aziz, Maxi Nzengeli wa Yanga na Matheo Anthony wa Mtibwa Sugar wanafuatia nafasi ya tatu wakiwa na mabao matatu kila mmoja.