Category: STORY

KMC NDANI YA TATU BORA LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI KUU ya NBC imeendelea Leo kwa Mchezo mmoja katika uwanja wa Uhuru, Dar na kushuhudia KMC akiibuka na Ushindi wa Bao moja dhidi ya Mtibwa Sugar, lililowapeleka mpaka nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Bao pekee na la ushindi kwa KMC limefungwa na Ibrahim Elias Dakika ya 15 ya mchezo na kuifanya KMC kufikisha alama 15 na michezo saba mfululizo bila kupoteza.

Ligi hiyo itaendelea kesho kwa michezo mitatu, mapema saa 8:00 Mchana Singida BS watawaalika Ihefu katika uwanja wa Liti mkoani Singida, Mashujaa watawaalika Azam FC saa 10:00 alasiri katika uwanja wa Lake Tanganyika Mkoani Kigoma na Mchezo wa mwisho saa 1:00 usiku Coastal Union watakuwa wenyeji wa Namungo katika uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.

AZIZ KI KINARA WA MABAO LIGI KUU YA NBC.

MCHEZAJI Stephane Aziz Ki wa Yanga amemshusha Jean Baleke wa Simba kwenye msimamo wa vinara wa mabao baada ya kufunga mabao matatu (Hat-trick) dhidi ya timu ya Azam.

Mabao matatu aliyofunga Ki yote kwa mguu wa kushoto yamemfanya kufikisha mabao sita na kumzidi Baleke mwenye matano na Feisal Salum wa Azam mwenye mabao manne.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha alama 15 sawa na timu ya Simba na kupanda nafasi ya kwanza kwa tofauti ya mabao manne.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena Oktoba 25 kwa michezo mitatu, JKT Tanzania dhidi ya Tabora United kwenye uwanja wa Azam Complex saa 16:00, Coastal Union na Mashujaa saa 12:30 kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga na mchezo wa mwisho utachezwa uwanja wa Jamhuri saa 21:00 kati ya Dodoma Jiji na Kagera Sugar.

‘KIVUMBI’ DAR ES SALAAM DERBY LIGI KUU NBC.

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo ikikutanisha ‘miamba’ wawili wa soka kutoka mkoa wa Dar timu ya Yanga dhidi ya Azam kwenye uwanja wa Mkapa, Dar utakaochezwa saa 12:30 jioni.

Yanga ndiye kinara wa kufunga mabao mpaka sasa (15) huku akiruhusu mabao mawili sawa na Azam.

Azam imeshinda michezo minne mpaka sasa na kutoa sare mmoja ikiwa haijapoteza mchezo wowote huku Yanga ikishinda minne na kupoteza mmoja.

Yanga imeshinda michezo mitano huku Azam ikishinda mitatu na sare tatu zimepatikana miamba hiyo ilipokutana kwenye michezo 10 iliyopita.

SINGIDA YATAKATA MAJALIWA LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Singida imepata ushindi wa pili msimu huu baada ya kuifunga Namungo mabao 2-3 kwenye uwanja wa Majaliwa, Lindi.

Namungo haijashinda mchezo wowote wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu ikipata sare mitatu na kupoteza mitatu.

Singida imeshinda michezo miwili idadi sawa na michezo ya kufungwa na kupata sare.

Mabao mawili yaliyofungwa na Marouf Tchakei na moja la Duke Abuya yameifanya Singida kufikisha alama nane na kukwea mpaka nafasi ya sita kwenye msimamo.

HIGHLAND ESTATES, NYANKUMBU HAKUNA MBABE LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Geita Gold imeshindwa kutamba kwenye uwanja wake wa Nyankumbu baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na timu ya Dodoma Jiji.

Geita imepata sare ya pili msimu huu ikipoteza michezo mitatu na kupata ushindi katika mchezo mmoja pekee dhidi ya Ihefu.

Ihefu ya Mbeya imeshindwa kutamba kwenye uwanja wake wa nyumbani Highland Estates baada ya kulazimishwa suluhu na Coastal Union ya Tanga.

Ihefu imepata sare ya kwanza msimu huu sawa na timu za Azam, KMC, Prisons na JKT Tanzania.

Coastal ambayo haijapata ushindi wowote msimu huu imepata sare ya tatu huku pia ikipoteza idadi hiyo ya michezo .