Category: STORY

TABORA YATAMBA NYUMBANI, AZAM YAPANDA KILELENI LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Tabora United imeendelea na wimbi la matokeo mazuri ikicheza uwanja wa nyumbani baada ya Leo kuifunga Dodoma Jiji mabao 2-1 katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

Tabora imekusanya jumla ya alama nane na kushika nafasi ya tano huku ikiwa timu ya tatu kwa kufunga mabao mengi kwenye uwanja wa nyumbani (matano) sawa na timu ya Azam.

Timu ya Azam imepanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuifunga Coastal Union bao 1-0 kwenye uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.

Bao pekee na la ushindi la Azam limefungwa na Feisal Salum dakika 44 ya mchezo.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa michezo miwili Kati ya KMC na Ihefu saa 10 alasiri katika uwanja wa Uhuru, Dar huku mchezo wa pili utazikutanisha Geita Gold dhidi ya Yanga saa 10:00 alasiri katika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza.

SIMBA YAKAA KILELENI, SINGIDA IKITAMBA LIGI KUU NBC.

TIMU ya Simba imeshinda mchezo wa nne mfululizo wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu na kukaa nafasi ya kwanza kwenye msimamo baada ya kuifunga Tanzania Prisons ya Mbeya mabao 3-1 kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mabao ya Clatous Chama, John Bocco na Saidi Ntibazonkiza yameifanya Prisons iliyokuwa ya Kwanza kupata bao kupitia kwa Edwin Balua kupoteza mchezo wa tatu msimu huu unaowaweka nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Singida Big Stars imepata ushindi wa kwanza msimu huu ikicheza uwanja wa Manungu, Morogoro ugenini baada ya kuifunga Mtibwa Sugar bao 1-0.

Bao la Singida limefungwa na Elvis Rupia na kuifanya Singida kufikisha alama tano na kupanda mpaka nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa michezo miwili kati ya Tabora United na Dodoma Jiji saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora huku mchezo wa pili ukiwa Coastal Union dhidi ya Azam Fc kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga saa 1:00 usiku.

WASHINDI TUZO ZA MWEZI SEPTEMBA LIGI KUU YA NBC.

KAMATI ya tuzo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemtangaza mchezaji wa timu ya KMC ya Dar Waziri Junior kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya NBC kwa mwezi Septemba akiwashinda Jean Baleke wa Simba na John Nakibinge wa Tabora United.

Waziri ameifungia timu yake mabao mawili na kuisaidia kushinda michezo miwili ya mwezi Septemba dhidi ya JKT Tanzania na Geita Gold.

Kamati hiyo pia imemtangaza kocha wa KMC Abdihamid Moalin kuwa kocha bora wa mwezi baada ya kushinda michezo yote miwili KMC waliyocheza kwa mwezi Septemba.

Moalin amewashinda Roberto Oliveira wa Simba na Abdallah Mohamed wa Mashujaa baada ya kukusanya alama sita na kupanda kutoka nafasi ya 14 mpaka ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Aidha kamati imemtangaza meneja uwanja wa Azam Complex Amir Juma kuwa meneja bora wa uwanja kwa mwezi Septemba.

 

 

 

VITA YA WABABE WA NBC CHAMPIONSHIP NDANI YA LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI Kuu ya NBC itaendelea leo kwa michezo miwili kwenye mikoa ya Shinyanga na Dodoma.

Wababe wawili wa ligi ya NBC Championship msimu uliopita JKT Tanzania na Mashujaa wanakutana kwa mara ya kwanza ndani ya Ligi Kuu ya NBC katika uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga saa 10:00 alasiri.

JKT Tanzania imeshinda mchezo mmoja huku ikifungwa michezo miwili na kupata sare mchezo mmoja na Mashujaa ikianza vizuri msimu bila kufungwa mchezo na wala kuruhusu bao na ikishinda michezo miwili na kupata sare michezo miwili.

Dodoma Jiji watakuwa wenyeji wa Azam FC katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma saa 1:OO usiku katika mchezo wa pili leo.

Azam imeshinda michezo yote mitatu ya Ligi Kuu NBC msimu huu ikiwa na alama tisa katika nafasi ya tatu huku Dodoma ikishinda mchezo mmoja, sare moja na kufungwa moja ikiwa na alama nne huku ikishika nafasi ya saba kwenye msimamo.