Category: STORY

MBEYA KWANZA, MBUNI ZAPETA NBC CHAMPIONSHIP.

TIMU za Mbeya Kwanza na Mbuni zimecheza michezo minne ya Ligi ya NBC Championship bila kupoteza baada ya kila moja kupata ushindi leo.

Mbeya Kwanza inayotumia uwanja wa Nangwanda Sijaona imeifunga Kengold ya Mbeya kwa bao moja kwenye mchezo uliochezwa mapema saa 8:00 mchana.

Mbuni imepata ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Cosmopolitan kwenye uwanja wa Uhuru na kuifanya Cosmo iliyotwaa ubingwa wa First League msimu uliopita kucheza michezo minne bila kupata ushindi.

Mbeya Kwanza imepanda mpaka nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi ya NBC Championship ikifikisha alama 10 sawa na Mbuni huki Mbeya Kwanza akiongoza kwa tofauti ya mabao mawili.

Mchezo mwingine ulipigwa uwanja wa Jamhuri, Morogoro na kushuhudiwa Ruvu Shooting ikifungwa bao moja na Mbeya City na kuifanya Ruvu kuwa timu pekee ambayo haijapata alama msimu huu ikifungwa michezo yote na kushika nafasi ya 16 katika msimamo wa ligi hiyo.

TMA KINARA NBC CHAMPIONSHIP.

TIMU ya TMA FC ya Arusha imeendeleza mwanzo mzuri wa Ligi ya Championship ya NBC kwa ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Pan African ya Dar .

TMA imecheza mchezo wa nne mfululizo bila kupoteza ikifikisha alama nane na kuongoza msimamo wa Ligi ya Championship huku ikiwa mojawapo ya timu zilizopanda daraja msimu huu.

Mkoani Mara timu ya Biashara United imeshindwa kutumia vizuri uwanja wa nyumbani na kulazimishwa sare ya bao moja dhidi ya Pamba ya Mwanza.

Ligi hiyo itaendelea tena Septemba 30 kwa michezo mitatu kati ya Stand United na Copco saa 8:00 mchana kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga huku Transit Camp ikicheza na Polisi Tanzania kwenye uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Green Warriors dhidi ya FGA Talents kwenye uwanja wa Uhuru, Dar michezo itakayochezwa saa 10:00 alasiri.

LIGI KUU YA NBC YAENDELEA COASTAL, JKT ZABANWA NYUMBANI.

 

LIGI Kuu ya NBC imeendelea leo kwa michezo miwili, JKT Tanzania wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani CCM Kambarage mkoani Shinyanga wametoka sare ya bao moja na Kagera Sugar.

Bao la JKT lilifungwa na Danny Lyanga Dakika ya 90+6 kwa mkwaju wa penati huku bao la Kagera Sugar likifungwa na Gasper Mwaipasi dakika ya 90+8.

Ukiwa mchezo wao wa kwanza katika uwanja wa Nyumbani Mkwakwani, Coastal Union imetoka suluhu dhidi ya Tabora United.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena kesho Septemba 30 kwa michezo miwili, Geita Gold watawaalika KMC huku Namungo wakicheza na Mashujaa.

COASTAL, JKT KUANZA NYUMBANI LEO LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI Kuu ya NBC inarejea leo Septemba 29 kwa michezo miwili kuchezwa kwenye mikoa ya Tanga na Shinyanga.

JKT Tanzania watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar katika uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga saa 10 alasiri huku ukiwa mchezo wa kwanza wa JKT Tanzania kucheza nyumbani tangu kupanda Ligi Kuu ya NBC msimu huu wa 2023/2024.

Coastal Union itacheza kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga saa 1:00 usiku dhidi ya Tabora United huku Coastal ikiwa haijapata ushindi wowote msimu huu.

MASHUJAA, YANGA MILANGO MIGUMU

TIMU ya Mashujaa ya mkoani Kigoma na Yanga ya Dar zimetimiza michezo mitatu ya Ligi Kuu ya NBC bila kuruhusu bao lolote.

Yanga imecheza michezo mitatu nyumbani ikikusanya alama zote tisa na kuongoza msimamo wa ligi pasipo kuruhusu bao huku ikifunga mabao 11 ambapo tisa kati ya hayo yamefungwa kipindi cha pili.

Mashujaa iliyopanda daraja baada ya kuiondoa Mbeya City ya Mbeya kwenye michezo ya mtoano imeendelea kuonesha ubabe ikicheza michezo mitatu kwenye uwanja wa nyumbani bila kupoteza wala kufungwa bao huku ikiwa na alama saba katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi