Category: STORY

DODOMA, MTIBWA HAKUNA MBABE

Mchezo wa Ligi Kuu ya NBC kati ya Dodoma Jiji na Mtibwa Sugar uliochezwa katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma umemalizika kwa sare ya bao moja.

Bao la Mtibwa Sugar lilifungwa na Abdul Hilary dakika ya 18 huku la Dodoma Jiji likifungwa na Emmanuel Martin dakika ya 38.

Dakika ya 25 mchezo ulilazimika kusimama baada ya golikipa wa Mtibwa Sugar Mohammed Makaka kudondoka ghafla na kuwahishwa hospitali.

akizungumza na Azam Tv baada ya mchezo kumalizika daktari wa Mtibwa Laurence Mushi amesema hali ya Makaka inaendelea vizuri kwasasa kinachosubiriwa ni majibu ya vipimo kujua nini Tatizo.

“Alianguka ghafla pasipokua na mpira wowote wa kugombania, baada ya kumuangalia nikagundua amepoteza fahamu tukamuwahisha hospitali, kwasasa anaendelea vizuri lakini tunasubiri majibu ya vipimo vya hospitali “ alisema Mushi

TABORA UTD YATAMBA

Mkoani Tabora Tanzania Prisons imepoteza mchezo wa pili mfululizo dhidi ya Tabora United kwa mabao 3-1.

Tabora UTD iliyopoteza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Azam kwa mabao 4-0 imepata ushindi huo wa kwanza kwa mabao ya John Ben aliefunga mawili na Erick Okutu huku bao la Prisons likifungwa na Samson Mbangula.

Prisons imeruhusu mabao sita kwenye michezo miwili iliyopita huku wakiwa na alama moja pekee waliyopata suluhu dhidi ya Singida Fountain Gate inayowaweka nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

LADHA YA LIGI KUU YA NBC KUREJEA LEO

BAADA ya siku 15 kupita  kupisha kalenda ya FIFA ya michezo ya kimataifa, Ligi Kuu ya NBC inarejea tena Leo Septemba 15 kwa michezo mitatu kuchezwa kwenye mikoa tofauti.

Mchezo wa mapema utachezwa Saa 8:00 mchana kati ya KMC na JKT Tanzania kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es salaam huku timu zote mbili zikipoteza kwenye michezo yao iliyopita  kwa idadi sawa ya mabao matano.

Mchezo wa pili utachezwa kati ya Tabora United na Tanzania Prisons saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Ali hasssan Mwinyi, Tabora huku ikiwa ni mara ya kwanza kwa Tabora United kucheza katika uwanja wao wa nyumbani baada ya kupanda daraja msimu huu.

Dodoma Jiji watakuwa nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma saa 1:00 usiku huku Mtibwa ikiwa haijashinda mchezo wowote na Dodoma ikipoteza mchezo uliopita kwa mabao 2-0 dhidi ya Simba.

POLISI KUJIULIZA KWA RUVU, PAMBA, PAN KUKIWASHA LEO.

Ligi ya NBC Championship itaendelea leo Septemba 15 kwa michezo miwili kuchezwa kwenye mikoa ya Kilimanjaro na Mwanza.

Polisi Tanzania watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Ushirika, Kilimanjaro saa 8:00 mchana huku mchezo huo ukitarajiwa kutangazwa Mbashara kupitia chaneli ya TV3.

Baaada ya kupata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Cosmopolitan kwenye mchezo wa kwanza Pamba watakuwa uwanja wa Nyamagana, Mwanza saa 10 alasiri kuwaalika Pan Africans waliopata ushindi wa mabao 3-2 katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Copco ugenini.

Jumla ya mabao 25 yamefungwa mpaka sasa kwenye ligi ya NBC Championship katika michezo minane iliyochezwa mzunguko wa kwanza.

 

NBC CHAMPIONSHIP LIVE TV3

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo Septemba 13 wameingia mkataba wa miaka mitatu (3) wa haki za matangazo ya televisheni kwa ligi ya NBC Championship na TV3 wenye thamani ya shilingi Milioni 613 kuanzia msimu wa 2023/2024 mpaka 2025/2026.

Akizungumza wakati wa hafla ya makubaliano hayo Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema wanaishukuru TV3 kwa kuamua kuonyesha Ligi ya NBC Championship na kuwahakikishia hawatojutia udhamini wao.

“Niwahakikishie TV3 hamtojuta kuingia mkataba huu na TFF, katika hili tunaenda sambamba kuhakikisha kwamba viwanja vitakavyotumika kwenye NBC Championship viwe na sifa sawa na vile vya Ligi Kuu” alisema Karia.

Naye Msimamizi wa vipindi wa TV3 Emanuel Skawa amesema TV3 wataonesha zaidi ya mechi 170 kati ya mechi 240 za NBC Championship kutokana sababu mbalimbali.

“Mechi hizo zitaonekana kupitia TV3 na TV3 Sports ambayo tutaizindua hivi karibuni na zinapatikana katika kisimbuzi cha StarTimes” alisema Skawa.

TV3 inapatikana ndani ya kisimbuzi cha StarTimes ambacho kinaonekana zaidi ya nchi saba Afrika (Tanzania, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Zambia, Msumbiji na Afrika Kusini) hivyo kuweka fursa kwa wachezaji wa Ligi hiyo kuweza kujiuza na kuonekana zaidi.