Category: STORY

TRANSIT YAFUKUZA ‘MWIZI’ KIMYA, BIGMAN, GEITA HAKUNA MBABE NBC CHAMPIONSHIP.

TIMU ya Transit Camp imerejea katika matokeo ya ushindi baada ya kuifunga KenGold bao moja kwenye uwanja wa nyumbani na kufanikiwa kusalia na alama zote tatu.

Mchezo huo uliopigwa uwanja wa TFF Center Kigamboni ulishuhudia Adam Uledi wa Transit Camp akiibuka shujaa kwa kuifungia Transit bao pekee kipindi cha pili kwa mkwaju wa penati huku likiwa bao la 11 kwake akiendelea kuongoza kwenye vinara wa mabao katika ligi ya Championship ya NBC.

Ushindi huo unaifanya Transit kufikisha alama 33 na kupanda hadi nafasi ya tatu ya msimamo ikiwa nyuma ya kinara wa ligi hiyo Geita Gold kwa alama nne pekee.

Mkoani Lindi kwenye uwanja wa Ilulu timu ya Bigman ilikuwa mwenyeji wa Geita Gold na kushuhudia mchezo huo ukikamilika kwa timu hizo kutoka sare ya bao moja.

Geita inayoongoza msimamo wa ligi hiyo kwa alama 37 imeshindwa kukusanya alama zote nyumbani kwa Bigman ambayo imeizidi alama 17 huku timu hiyo (Bigman) ikishika nafasi ya saba kwenye msimamo.

Hii ni sare ya pili mfululizo kwa timu ya Bigman kwenye uwanja wa nyumbani baada ya mchezo uliopita kulazimishwa sare na timu ya African Sports kutoka Tanga.

ILULU, KIGAMBONI KINAWAKA LEO NBC CHAMPIONSHIP.

LIGI ya Championship ya NBC inatarajiwa kuendelea leo kwa mzunguko wa 15 huku viwanja vya Ilulu, Lindi na TFF Center Kigamboni vikitarajiwa kutimua vumbi leo.

Bigman ya Lindi itakuwa mwenyeji wa Geita Gold inayoshika usukani wa Ligi ya Championship ya NBC kwenye uwanja wa Ilulu huku timu ya Bigman ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kulazimishwa sare kwenye uwanja huo na timu ya African Sports katika mchezo uliopita.

Hadi sasa timu ya Bigman imepoteza michezo mitano ya ligi hiyo na inakutana na Geita Gold ambayo haijapoteza mchezo wowote hadi sasa huku ikitoka sare michezo mitatu pekee.

Kwenye uwanja wa TFF Center Kigamboni timu ya Transit Camp itakuwa mwenyeji wa ‘wababe’ kutoka mbeya timu ya Kengold iliyoshiriki Ligi Kuu ya NBC msimu uliopita.

Transit Camp iliyopoteza mchezo uliopita kwa kipigo kikali cha mabao 3-0 dhidi ya Mbuni ugenini itashuka uwanjani kupambana na Kengold iliyopoteza pia ugenini kwa mabao 2-1 dhidi ya B19 inayoshika nafasi ya 13 kwenye msimamo huku ikiifanya B19 kufikisha ushindi wa pili msimu huu.

Transit Camp inahitaji kushinda mchezo wa leo ili kuweka hai matumaini ya kupanda daraja na kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu ujao ikishika nafasi ya nne kwenye msimamo hadi sasa nyuma ya vinara Geita Gold, Kagera Sugar na Mbeya Kwanza.

 

Ratiba ya Ligi Kuu ya NBC 2025/2026

LIGI KUU YA NBC KUREJEA LEO.

BAADA ya kusimama kwa takribani wiki tano Ligi Kuu ya NBC inatarajiwa kurejea leo Januari 16 kwa mchezo utakaopigwa kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma kati ya timu ya Dodoma jiji itakayokuwa mwenyeji wa Singida Black Stars.

Dodoma Jiji iliyoanza vibaya msimu huu imeshinda mchezo mmoja pekee wa Ligi Kuu ya NBC kwenye michezo nane iliyocheza huku ikishika nafasi ya 15 kwenye msimamo itaikaribisha Singida Black Stars inayoshika nafasi ya 15 ikishinda michezo miwili baada ya kucheza mitano.

Singida Black Stars inashuka uwanjani leo chini ya kocha mpya David Ouma baada ya kubadilisha majukumu ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho Miguel Gamondi mwenye nafasi mpya ya Mkurugenzi wa ufundi katika timu hiyo.

Hadi sasa usukani wa Ligi Kuu ya NBC unashikiliwa na timu ya JKT Tanzania yenye alama 17 huku timu ya KMC ikishika nafasi ya mwisho (16) ikikusanya alama nne pekee huku ikiwa imeshinda mchezo mmoja sawa na Dodoma Jiji inayoshika nafasi ya 15.

Mchezo wa leo utapigwa kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma saa 1:00 usiku na ndio mchezo pekee wa Ligi Kuu ya NBC utakaopigwa leo na utarushwa mbashara kwenye chaneli ya Azam Sports.

 

YOUNG AFRICANS YAANZA KIBABE 2026.

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya NBC timu ya Young Africans imeanza mwaka 2026 kibabe kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga timu ya Azam FC kwa mikwaju ya penati 5-4.

Mechi hiyo iliyokuwa na upinzani mkali ilishuhudia timu hizo zikitoka suluhu ndani ya dakika 90 huku mchezaji wa Young Africans Pacome Zouzoua wa Young Africans akikosa mkwaju wa penati na Cheickna Diakite wa Azam akishindwa kumaliza mchezo baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu.

Young Africans inayoshika nafasi ya pili kwenye maimamo wa Ligi Kuu ya NBC imekuwa timu ya kwanza kushinda kombe kwa mwaka 2026 ikishinda kwa wachezaji wake wote watano kufunga mikwaju yao huku Landry Zouzou akikosa penati yake.

Young Africans imeifunga Azam fainali ya pili mfululizo kwenye ardhi ya visiwa vya Zanzibar baada ya kufanya hivyo kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho iliyopigwa uwanja wa Amaan Complex msimu wa 2024/25 kwa mikwaju ya penati.

 

 

NBC CHAMPIONSHIP YANOGA.

IKIKAMILISHA mizunguko 14 Ligi ya Championship ya NBC imeendelea kuleta msisimko zaidi kutokana na ushindani wa timu zikipambana kupanda Ligi Kuu ya NBC huku nyingine zikipambana kusalia kwenye ligi hiyo kwa msimu unaofuata.

Utamu wa ligi hiyo upo zaidi kwenye nafasi ya kwanza na ya pili ambapo timu ya Geita Gold inashikilia usukani na Kagera Sugar ikishika nafasi ya pili huku timu hizo zikilingana alama (36), mabao ya kufunga (27), na mabao ya kufungwa (6).

Timu hizo zimeshacheza mchezo wao wa mzunguko wa kwanza ambapo zilitoka sare ya bao moja kwenye uwanja wa Nyankumbu, Geita ambapo timu ya Geita Gold ilikuwa mwenyeji.

Timu hizo za kutoka kanda ya ziwa hadi sasa ndio timu pekee kwenye ligi hiyo ambazo hazijapoteza mchezo wowote.

Timu za Hausung na Barberian zinashika nafasi mbili za chini zinazotoa timu za kushuka daraja zikikusanya alama saba kila mmoja huku timu hizo zikiwa zimepanda daraja na kushiriki ligi hiyo kwa mara ya kwanza msimu huu.

Timu ya B19 ndio timu iliyofungwa mabao mengi hadi sasa ikifungwa (27) ikiwa imeshinda michezo miwili pekee sawa na timu za Hausung na African Sports.

Timu ya Barberian inayoshika nafasi ya mwisho ndio timu iliyoshinda michezo michache msimu huu ikishinda mmoja pekee huku ikifanikiwa kufunga mabao nane pekee.