Category: STORY

Saa 72

TAARIFA YA KAMATI YA SAA 72

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Desemba 15, 2025 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

Ligi Kuu ya NBC

Mechi Namba 032:  Singida BS FC 1-3 TRA United FC

Mchezaji Khalid Aucho wa klabu ya Singida BS ya mkoani Singida amefungiwa michezo mitano (5) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kufanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga na kumsukuma mchezaji Adam Adam wa klabu ya TRA United wakati wa mchezo tajwa hapo juu.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Alex Pancras kutoka Dar es Salaam amepewa Onyo Kali kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua stahiki kwa kitendo cha ukiukwaji wa sheria za mpira kilichofanywa na mchezaji Khalid Aucho.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.6) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.

Mechi Namba 031: Simba SC 0-2 Azam FC

Mchezaji Jonathan Sowah wa klabu ya Simba ya mkoani Dar es Salaam amefungiwa michezo mitano (5) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kufanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga kiwiko mchezaji Himid Mao wa klabu ya Azam wakati wa mchezo tajwa hapo juu.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mchezaji Allasane Kante wa klabu ya Simba ya mkoani Dar es Salaam amefungiwa michezo mitano (5) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kufanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga teke kwa makusudi mchezaji Feisal Salum wa klabu ya Azam wakati wa mchezo tajwa hapo juu.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.

Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Abdallah Mwinyimkuu kutoka Singida ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano (5) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua kwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria za mpira vilivyofanywa na wachezaji Jonathan Sowah na Allasane Kante katika mchezo huo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.6) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.

Mechi Namba 046:  Coastal Union FC 0-1 Young Africans SC

Klabu ya Young Africans ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la shabiki wake kuruka uzio na kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch), ambapo shabiki huyo alionekana kufika hadi kwenye goli la timu ya Coastal Union na kuinama kama Ishara ya kutafuta, kuchukua ama kuweka kitu.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

MUHIMU

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inazikumbusha klabu zake kuendelea kusisitiza umuhimu wa mchezo wa kiungwana na tabia njema mchezoni kwa wachezaji, viongozi na mashabiki wake. Ukumbusho huu unakuja kufuatia mfululizo wa matukio ya wachezaji kufanya vitendo visivyo vya kiuanamichezo kwa wachezaji wenzao ikiwemo kupiga.

Pamoja na kuhatarisha usalama wa wachezaji, matukio hayo pia yamekuwa yakileta taswira mbaya kwa Ligi yetu jambo ambalo linaweza kushusha hadhi yake na kwamba licha ya adhabu kali ambazo zimekuwa zikitolewa kwa wachezaji husika, bado matukio hayo yameonekana kuendelea viwanjani.

Ligi ya Championship ya NBC

Mechi Namba 061:  African Sports Club 0-2 Transit Camp FC

Klabu ya Transit Camp ya mkoani Dar es Salaam imetozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kuwakilishwa na maofisa wanne (4) badala ya watano (5) kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM) kuelekea mchezo tajwa hapo juu kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:2(2.1) ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

First League

Mechi Namba 7A: Alliance FC vs Biashara United

Klabu ya Alliance ya mkoani Mwanza imepewa ushindi wa mabao matatu (3) na pointi tatu (3) katika mchezo tajwa hapo juu, huku Biashara United ikipoteza mchezo huo kwa mujibu wa Kanuni ya 17:31 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Biashara United ilisababisha mchezo huo kuvunjwa katika dakika ya 67 baada ya wachezaji wawili (2) wa timu hiyo iliyoanza mchezo ikiwa na wachezaji wanane (8) tu, kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo hivyo kufanya timu hiyo kusalia na wacheza sita (6) pekee ambao hawawezi kufanya mchezo uendelee kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:30 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 10A: Pan African FC vs Moro Kids FC

Klabu ya Pan African ya mkoani Dar es Salaam imepoteza mchezo tajwa hapo juu na timu ya Moro Kids imepewa ushindi wa mabao matatu (3) na alama tatu (3) kwa kosa la Pan African kushindwa kuandaa mchezo huo kikamilifu, jambo lililosababisha mchezo huo kushindwa kufanyika kwa mujibu wa Kanuni.

Pan African ilishindwa kupeleka uwanjani gari maalum la kubebea wagonjwa (Ambulance) kama ilivyoelekezwa kwenye Kanuni ya 17:7 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo, hata baada ya kupita dakika 30 za kusubiri kwa mujibu wa kanuni.

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 17:7 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo na Kanuni ya 32:1 ya First League kuhusu Kuvuruga Mchezo.

Nassor Idrissa

NASSOR IDRISSA MWENYEKITI MPYA BODI YA LIGI.

NASSOR Idrissa ‘Father’ amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) baada  ya kupata kura saba (7) dhidi ya kura sita (6) za mpinzani wake CPA Hosea Lugano kwenye uchaguzi uliofanyika jana Novemba 29, 2025 katika Hotel ya Golden Tulip, Masaki Jijini Dar Es Salaam.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Nassor alisisitiza chini ya utawala wake atahakikisha haki inapatikana kwa kila timu bila kujali ukubwa wa timu, hususani maamuzi yanayotolewa ndani ya Dakika 90 za mchezo.

Katika Hatua nyengine Hassan Muhsini Mwenyekiti wa Coastal Union amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ambapo katika nafasi hiyo hakuwa na mpinzani hivyo kupitishwa kwa kura ya ndio wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).

Pia Japhet Makau Rais wa Fountain Gatena Gilbert Nkolonko Mwenyekiti wa Mbeya City wamechaguliwa kuwa wajumbe wawakilishi wa klabu za Ligi Kuu ya NBC huku Ahmed Gao wa Bigman na John Ndumbaro wa Mbeya City wakichaguliwa kuwa wajumbe wawakilishi wa klabu za Ligi ya Championship ya NBC wakati huohuo Azim Khan wa Dar City akichaguliwa kuwa mjumbe muwakilishi wa klabu za First League.

kagera sugar kupindua meza

KAGERA SUGAR KUPINDUA MSIMAMO LEO ?

Kagera Sugar inashuka Dimbani hii leo Novemba 22 kuwakabili Polisi Tanzania kwenye muendelezo wa Ligi ya Championship ya NBC 2025/2026 mchezo utakao chezwa kwenye uwanja wa Kaitaba kuanzia saa 10:00 alasiri.

Kagera Sugar inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikiwa na alama 13 sawa na Geita Gold inayoshika nafasi ya kwanza wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kwa upande wa Polisi Tanzania ina jumla ya Alama 10 baaada ya michezo mitano ya Ligi ya Championship ya NBC ikishinda michezo mitatu, kufungwa mmoja na kutoka sare mchezo mmoja.

UShindi kwenye mchezo wa leo unaweza kuwapeleka ‘Wana Nkurukumbi’ Kagera Sugar kwenye kilele cha Ligi ya Championship ya NBC ikiwa mpinzani wake wa Karibu Geita Gold akipata matokeo mengine tofauti na ushindi.

Mkoani Tanga African Sports itaikaribisha Geita Gold kinara wa Ligi ya Championship ya NBC kwenye uwanja wa Mkwakwani mchezo utakaoanza saa 10:00 alasiri, Mchezo huu utarushwa Mubashara ‘Live’ kupitia FIFA+.

HAWA HAPA WAKALI WA ‘GUU’ LA KULIA KWENYE LIGI KUU YA NBC.

WAKALI wa kutumia mguu wa kulia katika kufunga mabao ndani ya Ligi Kuu ya NBC wanazidi kuongezeka kadri Ligi inavyozidi kuendelea ikiwa ni mzunguko wa sita wa Ligi .

Maxi Nzengeli mchezaji anaecheza eneo la kiungo katika timu ya Young Africans amefanikiwa kuifungia mabao mawili timu yake akitumia ufundi wa mguu wake wa kulia na kuwa tishio kwa mabeki wa timu pinzani.

Peter Lwasa kiungo mshambuliaji anaekipiga kwenye timu ya Pamba Jiji nae amekuwa hodari na mguu wake wa kulia kwa kuifungia mabao mawili timu yake ndani ya msimu huu.

Mshambuliaji wa timu Mashujaa Mundhir Vuai aliyeanza msimu kwa kiwango bora ameingia pia kwenye orodha hiyo akiwa ameshatupia mabao mawili kwa ufundi wa mguu wake wa kulia.

Coastal Union nao wanatamba na mshambuliaji wao Athuman Makambo ambaye aliwika akiwa mfungaji bora wa Ligi ya Vijana akiwa na Mtibwa Sugar amefanikiwa kufunga mabao mawili kwa ‘guu’ lake wa kulia.

‘Kino Boys’ timu ya KMC inawakilishwa na Darueshi Saliboko ambaye amefunga mabao mawili kwa mguu wake wa kulia huku moja ya bao hilo likiwa bao la kwanza la msimu wa 2025/2026.

Mkongwe Vitalis Mayanga wa timu ya Mbeya City anazidi kuwafundisha vijana kuwa mguu wake wa kulia bado upo vizuri akifanikiwa kufunga mabao mawili ndani ya msimu huu.

Andy Boyeli ambaye jina lake halikuimbwa sana wakati wa usajili wake ni mshambuliaji wa timu ya Young Africans ambaye hadi sasa amefanikiwa kutikisa nyavu za wapinzani mara mbili kwa mguu wake wa kulia akifunga yote kwenye mchezo dhidi ya KMC.

NANI KUSHIKA USUKANI WA KILELE CHA MSIMAMO WA LIGI KUU YA NBC LEO ?

 

LIGI KUU ya NBC inarejea Leo Novemba 8 kwa michezo miwili kupigwa kwenye mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam baada ya kusimama kwa muda kwasababu ya changamoto za kiuendeshaji zilizotokana na sababu za kiusalama na Miongozo yake.

Mkoani Mwanza Pamba Jiji itaialika Singida Black Stars saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Pamba inashika nafasi ya pili (2) kwenye Msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikijikusanyia alama 8 kwenye michezo mitano huku Singida BS ikiwa nafasi ya nane (8) na alama zake sita baada ya michezo miwili.

‘Wazee wa kichapo cha Kizalendo’ JKT Tanzania itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye uwanja wa Mej. Jen Isamuhyo saa 1:00 Usiku. Huu ni mchezo wa tatu wa Ligi Kuu ya NBC kuchezwa usiku katika uwanja huo.

JKT Tanzania inaingia kwenye mchezo huu ikiwa imefunga mabao Saba na kuruhusu mabao sita kwenye michezo yake mitano iliyocheza, sawa na kusema imefunga na kuruhusu bao katika kila mchezo wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu wa 2025/2026 huku Simba ikifunga mabao sita na kutoruhusu bao lolote kwenye michezo miwili iliyocheza.

Alama tatu kwa kila timu kwenye michezo ya Leo zinaweza ipa timu yoyote nafasi ya kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026.