Category: STORY

SINGIDA BLACK STARS YAPAA KILELENI MSIMAMO WA LIGI KUU YA NBC.

SINGIDA Black Stars imepanda kileleni mwa Msimamo wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026 baada ya kuibuka na ushindi wa bao moja dhidi ya Mashujaa kwenye uwanja wa KMC.

Bao pekee la Singida BS limefungwa na mchezaji Elvis Rupia raia wa Kenya dakika ya 45+5 ya mchezo.

Singida Black Stars
Singida Black Stars

Ushindi huo unaifanya Singida BS kufikisha alama sita baada ya michezo miwili huku ikiwa haijaruhusu bao.

Mchezo wa pili ulipigwa saa 10:15 alasiri mkoani Mbeya uliozikutanisha Mbeya City dhidi ya Young Africans kwenye uwanja wa Sokoine na kumalizika kwa Suluhu.

Mbeya City Vs Young Africans
Mbeya City Vs Young Africans

Mchezaji Baraka Filemon  wa Mbeya City alitajwa Kama Mchezaji Bora wa mchezo huo kutokana na mchango mkubwa aliotoa kwa timu yake kwenye mchezo huo.

YOUNG AFRICANS,AZAM ZAANZA KIBABE LIGI KUU YA NBC.

TIMU za Young Africans na Azam zimeanza vyema msimu wa 2025/2026 baada ya kuibuka na ushindi kwenye michezo yao ya kwanza kwenye Ligi Kuu ya NBC iliyochezwa jana Septemba 24, kwenye viwanja vya Benjamin Mkapa na Azam Complex, Dar es Salaam.

Mchezo wa kwanza saa 1:00 usiku uliishuhudia Young Africans ikiikaribisha Pamba Jiji kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Mabao ya Young Africans yalifungwa na Lassine Kouma dakika ya 45+4, Bao la pili lilifungwa na mchezaji Maxi Nzengeli dakika ya 63 ya mchezo huku bao la tatu likifungwa na Mudathir Yahya Dakika ya 90+3.

Lassine Kouma - Young Africans
Lassine Kouma – Mchezaji Young Africans

Maxi Nzengeli Nzengeli Alitajwa kama mchezaji bora wa mchezo kutokana na kiwango bora alichoonesha kwenye mchezo huo.

Saa 3:00 usiku Azam FC ilkuwa mwenyeji wa Mbeya City kwenye uwanja wa Azam Complex na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Nassor Saadun ndiye aliyefungua ukurasa wa mabao kwa Azam FC kwenye dakika ya 32 ya mchezo akimalizia krosi safi iliyopigwa na mchezaji Abdul Suleimani ‘Sopu’

Bao la pili la Azam Lilifungwa na  dakika ya 46 ya mchezo akimalizia kazi kubwa iliyofanywa na mchezaji mpya wa kikosi hicho Baraket Hmidi.

Baraket Hmidi - Mchezaji Azam FC
Baraket Hmidi – Mchezaji Azam FC

Ikiwa huo ndio mchezo wake wa kwanza wa kwenye Ligi Kuu ya NBC Baraket Hmidi wa Azam FC Alitajwa kama mcheza bora wa mchezo.

COASTAL UNION YASHINDWA KUFURUKUTA IKIWA NYUMBANI

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa mchezo mmoja kati ya Coastal union na JKT Tanzania kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kushuhudia Coastal Union ikishindwa kutamba baada ya kufungwa mabao 1-2.

Mchezo ulianza kwa kasi na ilikuwa Coastal Union iliyokuwa ya kwanza kuandika bao dakika ya 21 kwa shuti kali la mchezaji Athumani Makambo.

Bao hilo lilidumu kwa dakika 14 pekee kabla ya Saleh Karabaka kuisawazishia JKT baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mohamed Bakari.

Kipindi cha pili JKT ilibadilisha mchezo na dakika ya 67 kuongeza bao la pili lililofungwa na Mohamed Bakari aliyekuwa na siku nzuri ‘kazini’ baada ya makosa ya kiulinzi yaliyofanywa na mabeki wa Coastal Union.

Katika mchezo huo Ally Msengi wa JKT aliibuka mchezaji bora wa Mchezo huo baada ya kufanya kazi kubwa ya kiulinzi iliyowapa alama tatu ‘maafande’ hao.

LIGI KUU YA NBC YAENDELEA KUSHIKA KASI

 

LIGI kuu ya NBC imeendelea kushika kasi kwa michezo mitatu iliyochezwa kwenye viwanja vya Lake Tanganyika mkoani Kigoma, Tanzanite Kwaraaa mkoani Manyara na Majaliwa mkoani Lindi.

Mchezo wa kwanza uliopigwa saa 8 kamili mchana ulizikutanisha timu za Fountain gate na Mbeya city na kushuhudia Fountain Gate ikipoteza kwa bao moja lililofungwa na Habib Kyombo kwa mkwaju wa penati dakika ya 56.

Mbeya City iliyopanda daraja kutoka ligi ya Championship ya NBC imefanikiwa kuwa miongoni mwa timu tatu zilizokusanya alama tatu katika mzunguko wa kwanza huku mchezaji wa timu hiyo Habib Kyombo akiibuka mchezaji bora wa mchezo huo.

Mchezo wa pili ulipigwa kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma na kushuhudia maafande hao wakitoshana nguvu kwa sare ya bao moja.

Timu zote zilipambana kupata ushindi na alikuwa Mundhir Vuai wa Mashujaa dakika 78 aliyewapa uongozi kabla ya Paul Peter wa JKT kuisawazishia timu yake dakika nane baadae na kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare.

Paul peter aliibuka shujaa wa mchezo huo baada ya kuonyesha mchezo mzuri na kuisawazishia timu yake bao lililoipa alama ugenini.

Mchezo wa tatu ulichezwa saa moja kamili usiku na kushuhudia Namungo ikitoshana nguvu na Pamba jiji ya Mwanza kwa sare ya bao moja.

Dakika 19 zilitosha kwa Pamba jiji kupata bao lililofungwa na Staphan Siwa na hadi mapumziko wageni walikuwa mbele kwa bao hilo.

Namungo walipambana kupata bao la kusawazisha na dakika ya saba ya nyongeza kipindi cha pili Abdulaziz Shahame aliwanyanyua kwenye viti mashabiki wa ‘Wauaji wa Kusini’ kwa bao la kusawazisha na kufanya ubao wa matokeo kusoma sare ya 1-1.

Cyprian Kipenye wa Namungo aliibuka nyota wa mchezo huo baada ya kuonyesha kiwango bora .

KMC, COASTAL ZATAMBA LIGI KUU YA NBC

LIGI Kuu ya NBC msimu wa 2025/2026 imefunguliwa kwa michezo iliyochezwa kwenye viwanja vya KMC Complex mkoani Dar es salaam na Mkwakwani, Tanga na kushuhudia KMC na Coastal Union zikitamba kwa ushindi nyumbani.

Goli pekee la ushindi la KMC lilifungwa na Daruweshi Saliboko dakika ya 56 kipindi cha pili baada ya kipindi cha kwanza kumalizika kwa sare ya bila kufungana.

DARUESHI SALIBOKO - KMC
DARUESHI SALIBOKO – KMC

KMC wamekusanya alama zao tatu za kwanza za msimu wa 2025/26 na kuwa timu ya kwanza kushinda mchezo huku Daruweshi Saliboko akiwa mfungaji wa bao la kwanza la msimu.

Mchezo wa pili ulichezwa mkoani Tanga majira ya saa moja kamili jioni uwanja wa mkwakwani ambapo Coastal union waliwakaribisha Tanzania Prisons.

Kipindi cha kwanza kilitosha kwa Coastal kujihakikishia alama zake tatu kwa bao la kiungo wa zamani wa Azam na Dodoma Jiji Cleophace Mkandala lililodumu hadi mwisho wa mchezo.

Matokeo hayo yanaifanya Coastal union kuungana na KMC na kuwa timu za kwanza kukusanya alama tatu kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu.