Category: STORY

NI VITA YA KUBAKI NA KUPANDA FIRST LEAGUE LEO.

Michezo ya mtoano (PlayOff) ya kubaki na kupanda First League inachezwa leo Mei 8 ikikutanisha timu mbili kutoka First League ambazo ni Tunduru Korosho ya Ruvuma na Copco ya Mwanza pamoja na timu mbili kutoka kwenye Fainali za mabingwa wa mikoa ambazo ni Cargo ya Dar es Salaam na Kajuna ya Kigoma.

Mechi ya kwanza itakutanisha timu ya Cargo dhidi ya Tunduru Korosho saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa TFF Center Kigamboni uliopo Dar.

Mechi ya pili itakutanisha timu ya Kajuna dhidi ya Copco kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma huku mchezo huo ukitarajiwa kupigwa saa 10:00 alasiri.

Ikumbukwe timu mbili kutoka First league ni zile zilizopoteza michezo ya Mtoano wa kushuka daraja (Relegation Playoffs) na kupata nafasi ya kupambania kubakia kwenye Ligi hiyo kwa msimu ujao.

Timu mbili kutoka Fainali za mabingwa wa mikoa ni zile zilizotolewa kwenye Nusu Fainali na kushika nafasi ya tatu na ya nne kwenye fainali hizo.

SIMCHIMBA HASHIKIKI LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC

 

IKIWA imesalia mechi moja pekee kwa kila timu ya Ligi ya Championship ya NBC ufungaji wa mabao umeendelea kushika kasi huku mchezaji wa Geita Gold ya mkoani Geita Andrew Simchimba akiendelea kuongoza akiwa na mabao 18 katika mechi 22 alizocheza.

Nafasi ya pili inashikiliwa na mchezaji Abdulaziz Shahame wa TMA ya mkoani Arusha akiwa na mabao 17 huku timu yake ikishika nafasi ya sita baada ya kukusanya alama 50.

Mchezaji Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro anashika nafasi ya tatu akiwa amefunga mabao 16 huku timu yake ikiwa imekata tiketi ya kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26.

Nafasi ya nne ipo kwa mchezaji Ambokile Eliud wa Mbeya City ya mkoani Mbeya akiwa na mabao 11 huku akiisaidia timu yake kurejea tena kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu ujao.

Yusuph Mhilu wa timu ya Geita Gold anafunga ‘Mkeka’ akishika nafasi ya tano na mabao 10 huku Geita ikishika nafasi ya nne na ikitarajiwa kucheza michezo ya mtoano kuwania kucheza Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26.

HAYA HAPA MABORESHO RATIBA YA LIGI KUU YA NBC

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imefanya maboresho ya ratiba ya Ligi Kuu ya NBC kuanzia mzunguko wa 28 hadi 30 ikiwa ni ratiba ya kukamilisha msimu wa 2024/2025.

Michezo nane ya mzunguko wa 28 inataarajiwa kuchezwa kuanzia mei 12 hadi mei 14 huu timu ya Simba ikicheza dhidi ya Singida Black Stars mei 28 ikiwa ni baada ya mchezo wao wa Fainali ya Kombe la Shirikisho.

Michezo yote nane ya mzunguko wa 29 wa Ligi Kuu ya NBC itachezwa June 18 saa 10:00 alasiri na michezo ya mzunguko wa 30 itapigwa June 22 ambayo itakuwa siku ya kuhitimisha msimu wa 2024/2025.

WAMECHEZA DAKIKA NYINGI NBC CHAMPIONSHIP.

UKISALIA mchezo mmoja pekee Ligi ya Championship ya NBC kutamatika Mchezaji wa Mtibwa Sugar Oscar Masai anashikilia rekodi ya kucheza dakika nyingi zaidi kwenye ligi hiyo hadi sasa.

Oscar amecheza dakika 2627 hadi sasa huku akiwa ameisaidia Mtibwa kurejea kwenye Ligi Kuu ya NBC na endapo timu yake itashinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya Kiluvya itakuwa bingwa mpya wa Ligi ya Championship ya NBC.

Andrew William wa Stand United ya Shinyanga anashika nafasi ya pili kwa kucheza dakika nyingi akiwa nazo 2614 huku timu yake ikiwa nafasi ya tatu ya msimamo na ikitarajiwa kuchezo michezo ya mtoano kushiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025/26.

Evart Joseph wa African Sports ya Tanga anashika nafasi ya tatu akiwa na dakika 2580 huku timu yake ikishika nafasi ya 15 ikiwa kwenye mstari wa kushuka daraja na endapo African Sports itapoteza mchezo wake wa mwisho dhidi ya Transit Camp nyumbani itakuwa imeshuka daraja rasmi na kushiriki Ligi ya First League msimu wa 2025/26.

NGOMA AWALIZA JKT LIGI KUU YA NBC

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa mchezo mmoja ulioikutanisha timu ya JKT Tanzania na timu ya Simba katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo majira ya saa kumi jioni ulioshuhudia Simba ikishinda kwa bao moja.

Iliwachukua dakika 45 Simba kuandika bao kupitia kwa kiungo wake Fabrice Ngoma baada ya kupokea pasi kutoka kwa mshambuliaji Steven Mukwala na kuifanya Simba kwenda mapumziko ikiwa inaongoza bao moja.

Kipindi cha pili kilianza ambapo JKT Tanzania walijitahidi kulisaka lango la Simba bila kupata bao na hadi mchezo unatamatika ‘Mnyama’ alikuwa mbele kwa bao la Ngoma.

Simba ilifanikiwa kubeba alama zote tatu na kufikisha alama 63 katika michezo 25 iliyocheza huku ikiendelea kusalia katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC