Category: STORY

ISAMUHYO CHANGAMOTO KWA ‘VIGOGO’ LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC inatarajiwa kutimua vumbi leo Mei 5, kwa mchezo mmoja kati ya JKT Tanzania na Simba utakaopigwa kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam huku uwanja huo ukiwa sehemu ngumu kupata matokeo ya ushindi kwa timu kubwa za Ligi Kuu ya NBC.

JKT yenye ‘maskani’ yake Mbweni, Dar es Salaam imecheza uwanja wake wa nyumbani dhidi ya Young Africans na Azam bila kupoteza mchezo kwenye msimu huu wa 2024/25.

Michezo yote miwili dhidi ya timu hizo JKT haijaruhusu bao lolote kwani michezo hiyo ilimalizika kwa suluhu huku golikipa wa timu hiyo Yakoub Suleiman akimaliza michezo hiyo kwa kukusanya (hati safi) mbili.

JKT leo itakuwa mwenyeji wa ‘Kigogo’ mwingine wa Ligi Kuu ya NBC aliyefanikiwa kufuzu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika timu ya Simba kwenye uwanja huo wa Meja Jenerali Isamuhyo katika mchezo utakaopigwa saa 10:00 alasiri.

JKT KUWAKARIBISHA SIMBA ISAMUHYO LIGI KUU YA NBC

LIGI Kuu ya NBC itaendelea kesho kwa mchezo mmoja ambapo timu ya JKT Tanzania itaikaribisha timu ya Simba katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni mkoani Dar es Salaam  majira ya saa kumi jioni.

Mchezo huo ambao ni mchezo wa mzunguko wa 25 ulishindwa kufanyika hapo awali kutokana na ugumu wa ratiba ya Simba iliyokuwa  na michezo ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

JKT Tanzania ipo nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imefanikiwa kufunga mabao 24 na kuruhusu mabao 24 katika michezo 26 ambayo timu hiyo imeshacheza mpaka sasa huku ikikusanya alama 32.

Simba ipo nafasi ya pili kwenye msimamo  wa Ligi  Kuu ya NBC ikiwa imekusanya alama 60 katika michezo 23 ikifunga mabao 54 na kuruhusu mabao tisa .

SIMBA ‘YATAKATA’ DHIDI YA MASHUJAA LIGI KUU YA NBC

LIGI Kuu ya NBC imeendelea leo kwa mchezo mmoja uliochezwa majira ya saa kumi jioni katika uwanja wa KMC mkoani Dar es Salaam ambapo Simba waliwakaribisha timu ya Mashujaa kutoka mkoani Kigoma.

Mchezo ulianza kwa kasi ambapo kila timu ilionyesha ikitaka kupata alama tatu  ambapo iliwachukua dakika tano timu ya Mashujaa kufungua ukurasa wa mabao kupitia mchezaji wao Jafary Kibaya ambapo mpaka wakati wa kwenda mapumziko matokeo yalikuwa 0-1 licha ya Simba tupambana kusawazisha .

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Simba wakiwa na uchu zaidi wa kufika langoni mwa mpinzani wao licha ya kukutana na upinzani mkali kutoka kwa wachezaji wa timu ya mashujaa ambapo hata hivyo dakika ya 65 ya mchezo huo Leonel Ateba alifungua akaunti ya mabao kwa Simba kupitia mkwaju wa penati na kufanya ubao kusomeka 1-1 na alirejea tena nyavuni kupitia mkwaju wa penati ya pili hivyo kufanya ubao kusomeka 2-1 matokeo yaliyobaki hadi mwisho wa mchezo huo na kuwafanya Simba kubeba alama zote tatu .

 

BIASHARA UNITED YASHUKA FIRST LEAGUE.

TIMU ya Biashara United ya mkoani Mara rasmi imeshuka daraja kutoka Ligi ya Championship ya NBC na msimu ujao 2025/2026 itashiriki ligi ya First League.

Biashara imefikia hatua hiyo baada ya jana Mei 1, kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Geita Gold hivyo kufikisha alama 15 ambazo hata akishinda mchezo wake wa mwisho hazimuondoi katika nafasi ya mwisho ya Ligi ya Championship ya NBC.

Moja ya timu kati ya Transit Camp, Cosmopolitan au African Sports inaweza kuungana na Biashara United kwenye kushuka daraja endapo matokeo yao ya michezo ya mwisho ya Ligi ya Championship ya NBC hayatakuwa mazuri siku ya michezo ya mwisho ya ligi hiyo

 

SIMBA ‘KUKIWASHA’ NA MASHUJAA LEO LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC inarejea rasmi leo ambapo mchezo mmoja utachezwa katika uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge mkoani Dar es Salaam timu ya Simba ikiikaribisha timu ya Mashujaa kutoka mkoani Kigoma.

Mchezo huo utachezwa majira ya saa kumi jioni ikiwa ni mchezo wa kiporo cha mzunguko wa 24 wa Ligi Kuu ya NBC ambao haukuchezwa kutokana na Simba kuwa na michezo ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo wamefanikiwa kufuzu fainali ya michuano hiyo.

Simba ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na alama 57 ikifanikiwa kufunga mabao 52 na kuruhusu mabao 8 ikiwa ni timu iliyoruhusu mabao machache kuliko timu zote ikiwa timu hiyo imeshacheza michezo 22.

Mashujaa ipo nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imefanikiwa  kufunga mabao 26 ikiruhusu mabao 30 katika michezo 26 ambayo timu hiyo imeshacheza.