Category: STORY

MBEYA CITY WAKALI WA ‘KUTUPIA’ NBC CHAMPIONSHIP

TIMU ya Mbeya City imeendelea kuongoza kwa kufunga mabao kuliko timu yoyote katika Ligi ya Championship ya NBC licha ya kuwa katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi hiyo.

Mbeya City wamefanikiwa kufunga mabao 58 katika michezo 28 ambayo timu hiyo imecheza huku ikiwa imeruhusu mabao 26 na kukusanya alama 62 ikiwa nafasi ya pili katika msimamo nyuma ya Mtibwa Sugar ambayo imeshapanda Ligi Kuu ya NBC.

Mtibwa Sugar wanafuatia kwa kufunga mabao ikifunga mabao 54 na kuruhusu mabao 16 katika michezo 28 iliyocheza huku ikiwa imekusanya alama 67 na ikiongoza katika msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC.

Geita Gold imefanikiwa kufunga mabao 49 huku ikiruhusu mabao 24 pamoja na kuvuna alama 54 ikiwa nafasi ya nne katika msimamo huku Stand United ikifunga mabao 47 na kuruhusu  mabao 23 wote wakiwa  wamecheza michezo 28 katika Ligi hiyo.

Mbeya Kwanza imefunga mabao 40 baada ya kucheza michezo 28 ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 26 na ikiwa nafasi  ya sita katika mbio za ubingwa wa Ligi hiyo.

YOUNG AFRICANS ‘HAWACHEKESHI’ NDANI YA BOKSI

UTAMU wa Ligi Kuu ya NBC unazidi kukolea ikiwa ni mzunguko wa 27 wa Ligi hiyo huku timu ya Young Africans ikiongoza kwa kufunga mabao mengi ndani ya eneo la boksi (18).

Young Africans imefanikiwa kufunga mabao  55 ndani ya boksi ikiwa ni mabao mengi kufungwa na timu kwenye Ligi Kuu ya NBC.

Simba nayo haina mzaha ikiwa ndani ya boksi ambapo hadi sasa ikifanikiwa kufunga mabao 48  huku Azam ikiwa na mabao 38 kwenye eneo hilo la 18.

Singida Black Stars nayo haina utani iwapo wachezaji wake wakipata mpira ndani ya boksi ikiwa imeshafunga mabao 37 huku Tabora United na Dodoma Jiji zikiwa na mabao 23.

Kwa upande wa Namungo imefanikiwa kufunga mabao 22 na Fountain Gate ikifunga mabao 20 ndani ya eneo hilo la 18.

FEISAL TISHIO LIGI KUU YA NBC

KIUNGO wa Azam Feisal Salum ameendelea kuwa kinara wa kutoa Pasi za mabao katika Ligi Kuu ya NBC  akiwa na Pasi 13  katika mechi  11 alizocheza msimu huu hadi sasa.

Pacome Zouzoa wa Yanga anashika nafasi ya pili akiwa na Pasi 9 huku akifuatiwa na wachezaji  wenzake Maxi Nzengeli wa Yanga na Prince Dube wenye pasi 8 za mabao sawa na kiungo wa Singida Black Stars.

Kiungo Jean Ahoua wa Simba na Stephane Azizi Ki wa Yanga wanafuata wakiwa na Pasi 7 kila mmoja ikisalia mizunguko mitatu msimu kutamatika huku baadhi ya timu zikiwa na michezo ya ‘kiporo’.

 

LIGI KUU YA NBC KUREJEA MEI 2

LIGI Kuu ya NBC, Ligi namba nne kwa ubora barani Afrika  itarejea Mei 2 kwa mchezo kati ya Simba itakayokuwa mwenyeji wa timu ya Mashujaa kutoka mkoani Kigoma.

Mchezo huo utachezwa katika uwanja wa KMC Complex uliopo mkoani Dar es Salaam ikiwa ni mchezo wa mzunguko wa 24 uliosogezwa kutokana na timu ya Simba kuwa na ratiba ya michezo ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Baada ya mchezo huo timu ya Simba itakuwa na kibarua kingine ugenini katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar watakapokutana na timu ya JKT Tanzania waliyoifunga 1-0 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza kwa bao la Jean Ahoua aliefunga kwa mkwaju wa penati dakika za nyongeza.

Mei 8 itaikaribisha timu ya Pamba katika uwanja wa KMC Complex kabla ya kwenda ugenini kuvaana na timu ya KMC kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.

SIMBA YATINGA FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA.

MWAKILISHI pekee wa Ligi Kuu ya NBC kimataifa timu ya Simba imefanikiwa kutinga fainali baada ya kuiondoa timu ya Stellenbosch kutoka Afrika Kusini kwa matokeo ya jumla kwa bao 1-0.

Simba imelazimisha suluhu ugenini kwenye uwanja wa Moses Mabhida na kufanikiwa kufuzu baada ya faida ya ushindi wa 1-0 iliyopata kwenye mchezo wa nyumbani uliopigwa uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Simba imefanikiwa kutinga fainali hiyo ya kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza kwenye historia huku ikiwa timu ya pili kutoka kwenye Ligi Kuu ya NBC kufuzu fainali hiyo ndani ya miaka mitatu ikiungana na Young Africans iliyofanya hivyo mwaka 2023.

Simba itakutana na RS Berkane ya Morocco kwenye fainali hiyo iliyofuzu baada ya kuifunga CS Constantine ya Algeria kwa ushindi wa jumla kwa mabao 4-1.

Simba itaanzia ugenini Morocco Mei 17 huku mchezo wa pili na wa mwisho katika shindano hilo ukitarajiwa kupigwa Mei 25 kwenye uwanja wa Mkapa, Dar.