Category: STORY

MTIBWA YAPANDA RASMI LIGI KUU YA NBC

TIMU ya Mtibwa Sugar imepanda rasmi Ligi Kuu ya NBC ambayo ni Ligi namba nne kwa ubora barani Afrika  wakitokea Ligi ya Championship ya NBC baada ya kufanikiwa kufikisha alama 67 ambazo hakuna timu itaweza kuzifikia  katika michezo 28 abayo timu hiyo imeshacheza mpaka sasa.

Mtibwa ambayo ilishuka daraja msimu uliopita na sasa wamerejea rasmi huku ikiwa imeweka rekodi ya kucheza michezo 14 katika uwanja wao wa nyumbani wa Manungu pasipo kufungwa huku michezo 14 ya ugenini wakishinda saba kupata sare nne na kufungwa michezo mitatu.

Aidha timu hiyo imefanikiwa kufunga mabao 54 kuruhusu mabao 16 katika michezo timu hiyo  iliyocheza huku wakiwa wamebaki na michezo miwili ili kuweza kutamatika kwa Ligi ya Championship ya NBC

SIMCHIMBA KINARA WA MABAO LIGI YA NBC CHAMPIONSHIP

Ikiwa imesalia michezo mitatu ya Ligi ya Championship ya NBC vita ya ufungaji wa mabao ikiendelea kushika kasi baada ya  mchezaji  wa Geita Gold kutoka mkoani Geita,  Andrew  Simchimba, kuongoza  akiwa ameshatupia mabao  18 katika mechi 20 ambazo amecheza akiwa na timu yake hiyo.

Nafasi ya pili ikishikiliwa na mchezaji Raizin Hafidhi wa Mtibwa Sugar  ya mkoani Morogoro akiwa amefanikiwa kufunga mabao 16, sambamba na mchezaji, Abdulaziz Shahame, wa timu ya TMA ya mkoani Arusha  akiwa na mabao 16

Nafasi ya nne ikichukuliwa na mchezaji  Ambokile Eliud wa Mbeya City  ya mkoani Mbeya akiwa na mabao 9 huku Mwani Ally wa timu hiyo pia akiwa na mabao 9 yanayomfanya kuwa nafasi ya tano.

Mzunguko wa 28  wa Ligi ya NBC Championship utaendelea kesho ambapo mechi zote nane za mzunguko huo zitachezwa majira ya saa kumi jioni.

VIWANJA NANE ‘KUWAKA MOTO’ LIGI YA NBC CHAMPIONSHIP KESHO

LIGI ya NBC Champioship inaendelea kushika kasi ikielekea mwishoni  na  hapo kesho michezo nane ya mzunguko wa 28 itachezwa katika viwanja mbalimbali nchini majira ya saa kumi jioni .

Timu ya Cosmopolitan ambayo iko nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC itaikaribisha timu ya Stand United iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Green Warriors iliyopo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi ya Champioship itaikaribisha timu ya Biashara United ambayo ipo nafasi ya mwisho kwenye msimamo mchezo utakaochezwa uwanja wa Azam Complex Dar es Salaam.

Transit Camp  ikiwa kwenye nafasi  ya 14 katika msimamo itaikaribisha timu  ya TMA  iliyopo nafasi ya tano kwenye msimamo mchezo utakaochezwa katika uwanja wa TFF Centre uliopo Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Timu ya Kiluvya iliyopo nafasi ya 12 itaikaribisha timu ya  Mbuni ambayo iko nafasi ya tisa katika mchezo utakaochezwa uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.

Mbeya Kwanza  iliyo nafasi ya sita itachuana  vikali na African Sports iliyo nafasi ya 15 mchezo utakaochezwa uwanja wa Nangwanda Sijaona Mkoani Mtwara.

Timu ya Bigman iliyo nafasi ya saba itawaalika timu ya Mtibwa Sugar inayoongoza Ligi ya Championship ya NBC katika uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

Wachimba madini yaani Geita Gold iliyo nafasi ya nne kwenye msimamo itawakaribisha Mbeya City iliyo nafasi ya pili katika uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita huku Songea United iliyopo nafasi ya nane ikiwakaribisha Polisi Tanzania iliyo nafasi ta 10  katika uwanja wa Majimaji mkoani Songea.

 

 

MZIZE NI MOTO WA KUOTEA MBALI LIGI KUU YA NBC.

MCHEZAJI wa Young Africans raia wa Tanzania Clement Mzize ameendelea kuwa ‘Mwiba’ kwa mabeki wa timu pinzani baada ya kufanikiwa kufunga jumla ya mabao 13 hadi sasa kwenye Ligi Kuu ya NBC.

Mzize amefunga idadi hiyo ya mabao huku timu yake ikisalia na michezo minne kutamatika kwa msimu wa 2024/25.

Prince Dube wa Young Africans na Jean Ahoua wa Simba wanafuata nyuma ya Mzize wakifunga mabao 12 kila mmoja huku Ahoua akifunga mikwaju ya penati mitano hadi sasa na kuwa kinara wa kufunga mabao kwa penati.

Jonathan Sowah anafuatia akifunga jumla ya mabao 11 huku akiwa amecheza michezo tisa pekee baada ya kujiunga na timu yake kwenye dirisha dogo la usajili.

Elvis Rupia wa timu ya singida Black Stars anafuata nyuma ya mshambuliaji mwenzake wa timu ya Singida Jonaathan Sowah akiwa na mabao kumi.

MBEYA CITY WAKALI WA MABAO LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC.

JOTO la nani kwenda Ligi Kuu namba nne kwa ubora barani Afrika Ligi Kuu ya NBC linazidi kupanda huku timu ya Mbeya City ikiongoza kwa upande wa kufunga mabao mengi kuliko timu yoyote katika Ligi ya Championship ya NBC.

Mbeya City wamefanikiwa kufunga mabao 55 katika michezo 27 ambayo timu hiyo imecheza huku ikiwa imeruhusu bao 24 na kukusanya alama 59 ikiwa nafasi ya pili katika msimamo nyuma ya Mtibwa Sugar.

Mtibwa Sugar wanafuatia kwa kufunga mabao ikiwa imefanikiwa kufunga mabao 53 na ikiruhusu mabao 15 katika michezo 27 iliyocheza huku ikiwa imekusanya alama 66 na ikiongoza katika msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC.

Stand United na Geita Gold wote wamefanikiwa kufunga mabao 47 kila timu huku Stand ikiruhusu mabao 23 pamoja na kuvuna alama 58 ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo na Geita Gold ikiruhusu mabao 21 wote wakiwa  wamecheza michezo 27 katika Ligi hiyo.

Mbeya Kwanza imefanikiwa kufunga mabao 38 baada ya kucheza michezo 27 ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 24 na ikiwa nafasi  ya sita katika mbio za ubingwa wa Ligi hiyo.