Category: STORY

GUNNERS HAUSUNG NBC CHAMPIONSHIP.

GUNNERS YAUNGANA NA HAUSUNG NBC CHAMPIONSHIP.

HATIMAYE timu ya Gunners ya mkoani Dodoma imeungana na Hausung ya mkoani Njombe kupanda moja kwa moja Ligi ya Championship ya NBC kwa msimu unaofuata wa 2025/2026 baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mapinduzi na kufikisha alama 35 hivyo kuongoza msimamo wa First League kundi B.

Baada ya kutamatika kwa Ligi hiyo kinachofuata sasa ni mchezo wa kutafuta Bingwa wa First League kwa msimu wa 2024/2025 ambapo kinara kundi A Hausung atakutana na kinara wa kundi B Gunners sambamba na  michezo ya mtoano (PlayOff).

Wakati huo huo timu za African Lyon kutoka kundi A na Ruvu Shooting kutoka Kundi B zimeshuka daraja baada ya kumaliza nafasi za mwisho kwenye makundi yao.

Katika hatua nyengine Ruvu Shooting imekumbana na adhabu ya kushushwa daraja na kufungiwa kushiriki Ligi kwa misimu miwili baada ya ombi lao la kujitoa katika Ligi ya First League kwa kile walichoeleza kuwa ni kushindwa kumudu gharama za uendeshaji kulikosababisha kuondokewa na wachezaji wao kadhaa kukubaliwa na Bodi ya Ligi.

FIRST LEAGUE KUHITIMISHWA LEO.

FIRST LEAGUE KUHITIMISHWA LEO.

LIGI ya First League inahitimishwa leo kwa michezo ya Kundi A na B kwa timu zote kundi A na timu sita kundi B kutupa karata zake kuanzia saa 10:00 jioni,

Tayari timu ya Hausung ya mkoani Njombe imeshakata tiketi ya moja kwa moja  kushiriki Ligi ya championship ya NBC msimu wa 2024/2025 kutoka kundi A huku ikisubiriwa timu ya kupanda moja kwa moja kutoka kundi B ambapo timu za Rhino Rangers, Gunners, na Tanesco zina nafasi kubwa ya kufanya hivyo.

Ikumbukwe kuwa timu inayoshika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa First League Kundi A na B Inafuzu moja kwa moja kushiriki Ligi ya Championship ya NBC.

Wakati timu zinazoshika nafasi ya pili na ya tatu kwenye kila kundi zikicheza michezo ya mtoano (PlayOff) kupata washindi wawili wa kucheza mtoano wa kupanda (Promotion PlayOff) na timu mbili za ligi ya Championship ya NBC.

 

HAWA HAPA WABABE WA UWANJA WA NYUMBANI LIGI YA CHAMPIONSHIP YA NBC.

LIGI ya Championship ya NBC inazidi kushika kasi ikiwa ni mzunguko wa 24 huku timu nyingi zikionyesha uwezo ambapo kila timu inataka kufuzu kwenda Ligi Kuu ya NBC msimu 2025-26 huku  timu za Mtibwa Sugar, Mbeya City, Geita Gold, Mbeya Kwanza na Songea United zikiwa hazijapoteza mchezo wowote nyumbani hadi sasa.

Mtibwa Sugar ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo ikiwa na alama 57 ikicheza michezo 12 kwenye uwanja wake wa Manungu Complex na kufanikiwa kushinda michezo yote.

Mbeya City iko nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ikishinda michezo tisa na kupata sare tatu katika michezo 12 waliyocheza uwanja wao wa nyumbani.

Geita Gold ipo nafasi ya nne katika  msimamo ikishinda michezo 11 na kupata sare mchezo mmoja katika michezo 12 iliyocheza ikiwa uwanja wao wa Nyankumbu.

Mbeya Kwanza ipo nafasi ya sita katika msimamo ikicheza michezo 11 nyumbani ikishinda michezo saba na kupata sare michezo minne.

Songea United  ipo nafasi ya nane katika msimamo ikicheza michezo 10 nyumbani na kushinda michezo sita huku ikipata sare michezo minne na kukamilisha idadi ya timu ambazo hadi sasa hazijapoteza mchezo wowote nyumbani.

MOUSSA CAMARA ANA JAMBO LAKE LIGI KUU YA NBC.

IKISALIA mizunguko saba kutamatika kwa Ligi Kuu ya NBC ‘Mlinda lango’ wa timu ya Simba Moussa Pinpin Camara ameendelea kushikilia usukani wa vinara ambao hawajaruhusu mabao kwenye ligi hiyo.

Camara hadi sasa amefikisha idadi ya michezo 15 aliyocheza bila kuruhusu nyavu zake kuguswa huku timu yake ikifungwa mabao nane pekee hadi sasa.

Golikipa huyo wa Simba amemzidi michezo minne mpinzani wake Djigui Diarra wa Yanga anayemfuatia kwa karibu akiwa amekusanya jumla ya michezo 11 bila kuruhusu bao.

Patrick Munthali wa timu ya Mashujaa iliyoruhusu mabao 28 hadi sasa anashika nafasi ya tatu akiwa na michezo 10 bila kuruhusu bao huku idadi hiyo ikiwa sawa na golikipa wa Azam Mohammed Mustapha huku Azam ikiruhusu mabao 12 hadi sasa ikisalia na michezo saba kutamatisha msimu.

LADHA ZA LIGI KUU YA NBC KUREJEA APRIL MOSI

LIGI Kuu ya NBC inatarajia kurejea mapema mwezi ujao baada ya mapumziko ya takribani wiki mbili  kupisha michezo ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026.

Kurejea kwa Ligi Kuu ya NBC ni mwanzo wa mzunguko wa  24  huku ikibaki mizunguko takribani sita ligi hiyo kutamatika.

April mosi Tabora United  itawakaribisha ‘watoto wa Jangwani’ Young Africans kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi  mkoani Tabora mchezo utakaochezwa majira ya saa kumi alasiri.

April mbili itapigwa michezo mitatu Pamba Jiji itaikaribisha Namungo majira ya saa 8:00 mchana katika  uwanja wa CCM Kirumba huku KMC ikiwaalika Tanzania Prisons kwenye uwanja wa KMC Complex mkoani Dar es Salaam majira ya saa 10:15 na mchezo wa mwisho utapigwa Tanzanite Kwaraa kati ya Fountain Gate itakayoikaribisha Singida Black Stars saa 10:15 alasiri.

April tatu itaanzia katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo JKT Tanzania ikiwakaribisha Dodoma Jiji, Ken Gold ikiwaalika Azam katika uwanja wa Sokoine michezo yote ikichezwa saa 10:00 alasiri huku Kagera Sugar ikiwaalika Coastal Union katika uwanja wa Kaitaba majira ya saa 1:00 usiku.

Mchezo wa Simba na Mashujaa utachezwa Mei mbili kutokana na timu ya Simba kukabiliwa na michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika ambayo kwa sasa ipo katika batua ya robo fainali.