Category: STORY

FOUNTAIN GATE YASHINDWA ‘KUFURUKUTA’ KWA SINGIDA LIGI KUU YA NBC.

Ligi Kuu ya NBC mzunguko 24 imeendelea huku mchezo uliochezwa mkoani Manyara kati ya Fountain Gate na Singida Black Star ukishuhudia Fountain ikishindwa kutamba na kufungwa mabao 3-0.

Dakika ya 29 zilitosha kuipa uongozi Singida Black Star  kwa bao la kwanza kupitia mchezaji wake Jonathan Sowah aliyefunga bao lake la 7 tangu kujiunga na miamba hiyo ya Singida.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Singida Black Star waliendelea kushambulia lango la Fountain Gate na mchezaji Frank Kwabena kuongeza bao la pili dakika ya 56 na dakika ya 71 mchezaji Emmanuel Kwame aliongeza bao la tatu kwa timu yake hivyo Singida Black Star kuongoza kwa mabao matatu na Fountain kumaliza bila bao mpaka mwisho wa mchezo.

Katika mchezo huo mchezaji kiungo wa Singida Black Star Keyeheh Emmanuel alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo huku Singida ikiwa nyuma ya Azam inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo.

 

PAMBA JIJI YABANWA NYUMBANI LIGI KUU YA NBC.

IKICHEZA mchezo wa tano mfululizo timu ya Pamba Jiji imeshindwa kupata ushindi baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na timu ya Namungo kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Namungo ilikuwa ya kwanza kufungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Jacob Massawe huku Pamba ikisawazisha kupitia kwa Nyota Abdoullaye Camara anayecheza kwa mkopo kutokea timu ya Singida Black Stars huku likiwa bao lake la pili msimu huu.

Matokeo hayo yanaifanya Pamba kushuka kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC hadi nafasi ya 13 ikiwa juu ya mstari wa kushuka daraja kwa tofauti ya alama tano.

Namungo imepanda hadi nafasi ya 12 baada ya kupata alama moja na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusalia kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025-26 chini ya kocha Juma Mgunda aliyewahi kufundisha timu za Coastal Union na Simba.

YANGA YAENDELEA ILIPOISHIA LIGI KUU YA NBC.

VINARA wa Ligi Kuu ya NBC Young Africans imeendelea kugawa ‘dozi’ inapocheza uwanja wa ugenini baada ya kuifunga Tabora United mabao 3-0 kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora.

Mchezo wa jana umeshuhudia wachezaji wa Young Africans Prince Dube na Clement Mzize wakifunga bao moja kila mmoja na wote kufikisha mabao 11 msimu huu huku Israel Mwenda akifunga bao la pili msimu huu.

Huu ni mchezo wa tatu mfululizo kwa Young Africans kushinda ugenini baada ya kuifunga Mashujaa 5-0 kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma na Pamba JIji 3-0 kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Kwenye michezo hiyo Young Africans imefanikiwa kufunga mabao 11 na kufikisha jumla ya mabao 61 huku ikiwa imeruhusu mabao tisa na kuwa timu ya pili kuruhusu mabao machache msimu huu nyuma ya Simba iliyoruhusu mabao nane pekee.

Ratiba ya Ligi Kuu ya NBC 2025/2026

LIGI KUU YA NBC KUWAKA VIWANJA VINNE LEO

LADHA za Ligi namba nne kwa ubora barani Afrika zinarejea rasmi leo kwa michezo minne itakayopigwa kwenye viwanja tofauti nchini ikiwa ni baada ya mapumziko ya michuano ya kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Mchezo wa kwanza utakuwa jijini Mwanza ambapo timu ya Pamba Jiji itakuwa mwenyeji wa timu ya Namungo katika uwanja wa CCM Kirumba majira ya saa nane mchana.

KMC itacheza dhidi ya timu ya Tanzania Prisons katika uwanja wa KMC Complex uliopo mkoani Dar es Salaam huku Tabora United itakuwa mwenyeji wa Young Africans katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora na mchezo wa mwisho utakuwa kati ya Fountain Gate itakayoialika Singida Black Stars katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara huku michezo yote mitatu ikichezwa saa 10:15 alasiri.

MBEYA STAND NBC CHAMPIONSHIP

MBEYA, STAND VITA YA NAFASI NBC CHAMPIONSHIP LEO.

‘VITA YA NAFASI’ ndivyo unavyoweza kuuita mchezo huu ambapo MBEYA City itaikaribisha Stand United kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya kuanzia saa 10:00 alasiri, kwenye muendelezo wa michezo ya  Ligi ya Championship ya NBC.

Mbeya City ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikiwa na alama 52 sawa na Stand United iliyo nafasi ya tatu zikitofautiana kwenye mabao ya kufunga na kufungwa, timu yeyote itakayoshinda mchezo huu itajichukulia kijiti cha nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi hiyo.

MChezo wa mwisho kwa leo utachezwa mkoani Mtwara ambapo Mbeya kwanza ya mkoani hapo itaialika Transit Camp ya Dar es Salaam kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona saa 10:00 alasiri.