Category: STORY

LIGI KUU NBC KUWAKA VIWANJA VITATU LEO.

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo kwa michezo mitatu itakayochezwa kwenye viwanja vitatu tofauti, miwili ikipigwa jijini Dar es salaam na mwingine mkoani Lindi.

Mchezo wa kwanza utazikutanisha timu za KMC dhidi ya Fountain Gate kwenye uwanja wa KMC Complex uliopo Dar es Salaam  saa 10:00 alasiri.

Fountain Gate inashika nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi Kuu  ya NBC ikiwa na alama 24 huku KMC ikiwa nafasi ya11 na alama 24.

Mchezo mwingine utachezwa  saa 1:00 usiku kati ya Namungo ya mkoani Lindi na Singida Black Stars ya Singida kwenye uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.

Namungo ipo nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na alama 23 na Singida BS ikishika nafasi ya nne baada ya kukusanya alama 41.

Mchezo wa tatu utachezwa saa 3:00 usiku kati ya Azam iliyotoka sare na Namungo kwenye mchezo uliopita dhidi ya Tanzania Prisons itakayokuwa ugenini kwenye uwanja wa Azam  Complex, Dar es Salaam.

Azam iliyoshindwa kupata ushindi kwenye michezo mitatu ya Ligi Kuu ya NBC mfululizo itajiuliza dhidi ya Prisons iliyopoteza mchezo wake uliopita ugenini dhidi ya Fountain Gate huku ‘Maafande’ hao wakiwa juu ya mstari wa kushuka daraja kwa nafasi moja pekee.

KENGOLD,MASHUJAA HAKUNA MBABE LIGI KUU NBC

MZUNGUKO wa 23 wa Ligi Kuu ya NBC umeendelea kwa mchezo mmoja uliochezwa uwanja wa Sokoine Mbeya majira ya saa kumi alasiri.

Mchezo ulianza kwa timu zote kusomana kwa kuwa zilikuwa zinahitaji kupata alama tatu mhimu ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi.

Iliwachukua dakika 21 kwa Mashujaa kupata bao la kwanza kupitia mchezaji Jafari Kibaya ambapo dakika  ya 26 mchezaji wa Mashujaa, Yusuf Dunia, alijifunga na kufanya mchezo kusomeka 1-1 matokeo yaliyobaki mpaka mwisho wa kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa ambapo dakika ya 47 mchezaji wa KenGold, Mishamo Daudi, aliiongezea timu yake bao la pili kabla ya Ally Nassor wa Mashujaa kuongeza bao la pili kwa mashujaa  hivyo ubao kusomeka 2-2 mpaka mwisho wa mchezo.

KenGold walifikisha alama 16 wakiwa nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC huku Mashujaa wakifikisha alama 24 wakiwa nafasi ya 10.

Mchezaji wa Mashujaa,Ally Nassor ‘Ufudu’ alitangazwa kuwa nyota wa mchezo huo.Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo kwa michezo mitatu.

ARAJIGA

ARAJIGA PILATO WA ‘DERBY’ YA KARIAKOO.

BODI ya Ligi Kuu Tanzania leo Februari 5, imetangaza orodha ya maofisa watakaosimamia mchezo wa ‘DERBY’ ya Kariakoo wakiwemo waamuzi wa mchezo huo, Ahmed Arajiga kutoka Manyara aliyeteuliwa kuwa mwamuzi wa kati akisaidiwa na Mohamed Mkono kutoka Tanga na Kassim Mpanga wa Dar es Salaam huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Amina Kyando kutoka Morogoro.

Maofisa wengine walioteuliwa kusimamia mchezo huo ni Pamoja na Salim Singano Kamisaa wa Mchezo, Soud Abdi Mtathmini wa Waamuzi, Baraka Kizuguto Mratibu wa Mchezo, Jonas Kiwia Mratibu wa Mchezo Msaidizi, Karim Boimanda Afisa Habari, Fatma Abdallah Afisa Protokali, Jerry Temu Afisa Masoko, Manfred Limbanga Daktari wa mchezo, ASP Hashim Abdallah Afisa Usalama na Ramadhan Misiru Msimamizi wa Kituo.

Ni siku tatu pekee zimesalia kwenda kushuhudia mchezo huo mkubwa zaidi kwenye Ligi namba nne (4) kwa ubora barani Afrika.

KENGOLD ,MASHUJAA HAPATOSHI SOKOINE LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo kwa mzunguko wa 23 kuanza rasmi katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya majira ya saa kumi alasiri.

Timu ya KenGold ndio mwenyeji wa mchezo huo ikiikaribisha timu ya Mashujaa kutoka Kigoma ambapo timu zote mbili zikitaka alama tatu muhimu.

KenGold  iko nafasi ya 16  kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imekusanya alama 15 huku wakifunga mabao 18 na kuruhusu mabao 38 .

Mashujaa ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imekusanya alama 23 kufungaa mabao 17 na kuruhusu mabao 26.

Mchezaji wa kuchungwa katika mchezo huo wa kikosi cha  KenGold  ni Seleman Bwenzi akiwa amecheza michezo sita na kufunga mabao matano ikiwa ni mchezaji aliyeingia kwenye dirisha dogo la usajili.

Kwa upande wa Mahujaa mchezaji wa kuchungwa ni David Ulomi akiwa amefunga mabao manne.

 

DIARRA, CAMARA

HUKU DIARRA KULE CAMARA MILANGO IPO SALAMA.

Zimesalia siku nne kuelekea kwenye kwenye ‘DERBY’ ya Kariakoo ambapo Young Africans itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Machi 8, 2025 kuanzia saa 1:15 usiku.

Young Africans na Simba zinaingia kwenye mchezo huu zikiwa ndio timu zilizoruhusu mabao machache zaidi ya kufungwa, Young Africans ikiruhusu tisa (9) huku Simba ikiruhusu mabao nane (8) pekee.

Moussa Camara wa Simba anaongoza kwa kuwa na hati safi (Cleansheets) akiwa nazo 15 kwenye michezo 20 aliyocheza akitumia jumla ya dakika 1800 huku Djigui Diarra wa Young Africans akifuatia akiwa nazo 11 kwenye michezo 15 aliyoitumikia Young Africans msimu huu akitumia jumla ya dakika 1451.

Ubora wa walinda milango hawa umezifanya timu za Young Africans na Simba kuwa na wastani mdogo wa mabao ya kufungwa hivyo kuufanya mchezo huu wa ‘Derby’ ya kariakoo kuwa na mvuto wa aina yake.