Category: STORY

KARIAKOO DERBY

YANGA WAKALI WA MABAO, SIMBA HAWAFUNGIKI KIRAHISI LIGI KUU YA NBC.

ZIMESALIA siku tano (5) pekee kuelekea mchezo wa ‘DERBY’ ya Kariakoo ambapo Young Africans itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi ya Machi 8, 2025.

Yanga inaingia kwenye mchezo huu ikiwa timu iliyofunga mabao mengi zaidi kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu ikifunga (58) kwenye michezo 22 iliyocheza huku ikiruhusu mabao tisa pekee.

Kwa upande wa Simba silaha yao muhimu mpaka sasa ni kuzuia mabao ambapo kwa msimu huu ndio timu iliyoruhusu mabao machache zaidi ikifungwa mabao nane pekee kwenye michezo 21 iliyocheza mpaka sasa huku ikifunga mabao 46.

Yanga ipo kileleni mwa msimamo ikiwa na alama 58 kwenye michezo 22 huku Simba ikiwa nafasi ya pili na alama 54 kwenye michezo 21 ikiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya Dodoma Jiji utakaopangiwa tarehe mpya baada ya kuahirishwa kutokana na ajali iliyopata timu ya Dodoma mkoani Lindi.

AZAM,NAMUNGO WAGAWANA ALAMA,PAMBA KUKIWASHA NA YANGA LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana kwa michezo miwili ya mzunguko wa 22 kuchezwa viwanja viwili jijini Dar es Salaam.

Mchezo wa kwanza ulichezwa saa kumi jioni ambapo timu ya JKT Tanzania iliwakaribisha timu ya KenGold kutoka Mbeya katika uwanja  wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni mkoani Dar es Salaam.

Mchezo ulianza kwa kasi ambapo kila mchezaji alipambana kuhakikisha  timu yake inapata alama muhimu ,dakika ya 45 mchezaji wa JKT, Edward Songo aliipatia timu yake goli  kwa  mkwaju wa penati  hivyo kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa kifua mbele.

Kipindi cha pili kianza ambapo Ken Gold walionekana wakilisaka kwa kasi lango la JKT Tanzania na dakika ya 85 mchezaji wa wao Selemani Bwenzi aliwaamsha mashabiki wa ‘makarasha’ kwa kuipatia timu yake bao la  kusawazisha  na kufanya mchezo kuisha wakiwa wamegawana alama moja moja.

Mchezaji wa Ken Gold Seleman Bwenzi alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo  baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.

JKT Tanzania wamefikisha alama 27 wakiwa wamefunga mabao 16 na kuruhusu mabao 16 na wakiwa nafasi ya sita baada ya kucheza mizunguko 22 ya Ligi Kuu ya NBC 2024/2025.

KenGold wanaendelea kusalia nafasi ya 16 kwenye msimamo wakiwa na alama 15 wakifunga mabao 18 kuruhusu 38 baada ya mizunguko 22 ya Ligi Kuu ya NBC.

Mchezo wa pili ni timu ya Azam iliwapokaribisha timu ya Namungo katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi mchezo uliochezwa saa moja jioni.

Ilimchukua dakika 12 mchezaji wa  Namungo, Hamis Halifa kuwaweka mbele timu yake kabla ya mchezaji wa Azam, Gibril Sillah kuweka mzani sawa  katika dakika ya 43 ya mchezo huo hivyo timu zote kwenda mapumziko ubao ukisomeka  1-1 matokeo yaliyobaki mpaka mwisho wa mchezo.

Mlinda mlango wa Namungo, Jonathan Nahimana alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Azam wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC wakiwa na alama 45 wakifunga mabao 32 kufungwa 12 huku Namungo wakiwa nafasi ya 12 wakiwa na alama  23 wakifunga mabao 16 na kuruhusu mabao 27.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo kwa michezo miwili ambapo timu ya Pamba Jiji itawakaribisha Young Africans katika uwanja wa CCM Kirumba huku Tabora United wakiwakaribisha Dodoma Jiji katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

JKT,KEN GOLD HAPATOSHI LEO LIGI KUU YA NBC

LIGI Kuu ya NBC inaendelea kwa michezo miwili inayopigwa mkoani Dar es salaam katika viwanja vya Meja Jenerali Isamuhyo na Azam Complex.

JKT Tanzania wazee wa ‘kichapo cha kizalendo’ itawakaribisha Ken Gold ‘wazee wa makarasha’ katika mchezo utakaochezwa saa kumi alasiri.

Ikumbukwe kuwa JKT Tanzania ipo nafasi ya sita kwenye msimamo ikiwa imefunga mabao 15 ikiruhusu mabao 15 na kukusanya alama 26 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Kwa upande wa Ken Gold ipo nafasi 16 ikiwa imefunga mabao 17 ikiruhusu 37  ikiwa imekusanya alama 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Mchezo wa pili utachezwa Azam Complex uliopo Chamazi Dar es Salaam majira ya saa moja usiku ambapo timu ya Azam itawakaribisha Namungo.

Azam ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imefunga mabao 31 ikiruhusu mabao 11 na  ikikusanya alama 44 .

Namungo ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imefunga mabao 15 ikiruhusu mabao 26 na kukusanya alama 22.

 

FOUNTAIN GATE YAJIPATA,MASHUJAA MAMBO MAGUMU

LIGI Kuu ya NBC jana michezo iliendelea kwa michezo mitatu iliyochezwa mikoa mitatu tofauti Manyara,Singida na Kagera.

Fountain Gate iliwakaribisha timu ya Tanzania Prisons katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa mchezo uliochezwa majira ya saa nane mchana.

Dakika ya 27  Fountain Gate walipata bao kupitia mchezaji wao Amos Kadikilo kwa mkwaju wa penati na ambalo ndio bao pekee katika mchezo huo na lilipelekea timu hiyo kuvuna alama zote tatu na kufikisha alama 25 nafasi ya nane ya katika msimamo wa Ligi Kuu.

Mchezaji wa Fountain Gate Amos Kadikilo alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo dhidi ya timu ya Tanzania Prisons ambayo ipo nafasi ya 14 ikiwa na alama 18.

Singida Black Stars iliwaalika Mashujaa majira ya saa kumi alasiri uwanjani CCM Liti, mchezo ulianza kwa kasi na timu zote zilishambuliana kwa kasi hadi kufikia mapumziko hakuna aliyeona lango la mwenzake.

Kipindi cha pili kilianza ambapo dakika ya 57 mshambuliaji wa Singida,Jonathan Sowah alifungua ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penati na dakika ya 60 aliongezea bao la pili huku Elvis Rupia akiongeza bao la tatu dakika ya 90 ya mchezo huo ambao uliisha kwa ubao kusomeka 3-0.

Mshambuliaji wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo akiisaidia timu yake kufikisha alama 41 wakiwa nafasi  ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu huku Mashujaa wakiwa nafasi ya 11 na wakivuna alama 23.

Mchezo wa mwisho ni Kager Sugar iliwakaribisha timu ya KMC majira ya saa moja jioni katika uwanja wa Kaitaba.

Mchezo ulikuwa wa kasi ambapo timu zote mbili zilikuwa zikishambuliana kwa kasi jambo lililopelekea mcheo huo kumalizika kwa 0-0 na mchezaji wa Kagera Sugar,Eric Mwijage atichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.Kagera walifikisha alama 16 wakiwa nafasi ya 15 huku KMC wakiwa nafasi ya 10 na alama 24.

MTIBWA

MTIBWA YAISHUSHIA MVUA YA MABAO GEITA, NBC CHAMPIONSHIP IKIENDELEA.

JUMLA ya mabao 13 yamefungwa  kwenye michezo mitano (5) ya Ligi ya Championship ya NBC iliyochezwa leo Februari 26, 2025 kwenye mikoa minne tofauti.

Mtibwa Sugar ikiwa nyumbani kwake Manungu mkoani Morogoro imeibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Geita Gold mpinzani wake wa karibu kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC, kwa matokeo hayo Mtibwa inasalia kileleni mwa msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC ikifikisha alama 51 kwenye michezo 21 iliyocheza.

Transit Camp ikiwa nyumbani ikakubali kichapo cha bao 0-1 dhidi ya Green Warriors, Cosmopolitan ikapokea kichapo cha bao 0-1 dhidi ya Kiluvya huku Bigman ikiifunga Biashara UTD kwa bao 2-0.

Mchezo wa Mwisho kwa leo ulizikutanisha Mbuni dhidi ya Mbeya City ambapo Mbeya City ikiwa ugenini ikaibuka na ushindi wa mabao 1-3, ushindi huu unaipandisha Mbeya City hadi nafasi ya tatu (3) kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho Februari 27 kwa michezo miwili (2) kuchezwa ambapo African Sports itakuwa mwenyeji wa Polisi Tanzania huku TMA ikiwakaribisha Songea United.