Category: STORY

DODOMA JIJI KUMALIZA ‘KIPORO’ CHA LADHA ZA LIGI KUU YA NBC KESHO.

LIGI Kuu ya NBC inatarajiwa kuendelea kesho kwa mchezo namba 148 ambapo timu ya Simba itaikaribisha timu  ya Dodoma jiji katika uwanja wa KMC Complex mkoani Dar es Salaam majira ya saa kumi jioni.

Simba ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa  na alama 54 ikifunga mabao 46 na kuruhusu mabao 8 katika michezo 22 timu hiyo iliyocheza mpaka sasa.

Dodoma Jiji iko nafasi ya nane  kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya  NBC  huku ikiwa na alama 27 ikifunga mabao 22 na kuruhusu 27 katika michezo 22 iliyocheza mpaka sasa.

Mechi hiyo ya Simba na Dodoma Jiji iliahirishwa kutokana na ajali iliyopata timu ya Dodoma Jiji ikitokea Ruangwa mkoani Lindi  kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya  timu ya Namungo

 

 

MTIBWA ‘MBABE’ NYUMBANI NA UGENINI NBC CHAMPIONSHIP.

TIMU ya Mtibwa Sugar inayoshikilia usukani wa Ligi ya Championship ya NBC imeendelea kuwa ‘Mwiba’ kwa timu za ligi hiyo kwa kushinda michezo mingi nyumbani na ugenini kuliko timu zote.

Mtibwa imeshinda michezo 11 nyumbani kwenye uwanja wa Manungu Complex, Morogoro huku ikishinda sita kwenye michezo yake ya ugenini na kuwa kinara wa ushindi nyumbani na ugenini.

Geita Gold inafuata ikiwa imeshinda michezo 10 kwenye uwanja wa Nyankumbu, Geita huku ikishinda minne ugenini sawa na timu za Mbeya Kwanza na Songea United.

Stand United ya Shinyanga na TMA FC ya Arusha zinashika nafasi ya tatu kwa kushinda michezo mingi kwenye uwanja wa nyumbani zikishinda michezo 9.

KYARUZI,SIMCHIMBA WANG’ARA TUZO ZA NBC CHAMPIONSHIP

BEKI wa Mtibwa Sugar  Erick Kyaruzi amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Januari wa Ligi ya NBC Championship 2024/25, huku Awadh Juma wa Mtibwa Sugar akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Kyaruzi aliyeingia fainali katika mchakato huo na Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar na Boniface Maganga wa Mbeya Kwanza, alionesha kiwango chenye mwendelezo katika safu ya ulinzi, huku pia akisaidia timu yake kwa kufunga mabao mawili katika dakika 270 za michezo mitatu aliyotumika.

Kwa upande wa Awadh aliyeingia fainali na Zuberi Katwila wa Bigman na Emmanuel Massawe wa Mbeya Kwanza, aliiongoza timu yake kupata ushindi katika michezo yote mitatu iliyocheza ikivuna pointi tisa na kuendelea kuongoza ligi hiyo.

Pia kamati imemchagua Andrew Simchimba wa Geita Gold kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Februari wa Ligi ya NBC Championship 2024/25, huku Mohamed Muya pia wa Geita Gold akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.

Simchimba aliyeingia fainali katika mchakato huo na Oscar Tarimo wa Mbeya Kwanza na Mwisho Yangson wa Polisi Tanzania alionesha kiwango chenye mwendelezo ikiwa ni pamoja na kufunga mabao manne katika michezo mitatu kwa dakika 253 alizocheza.

Kwa upande wa Muya aliyeingia fainali na Zuberi Katwila wa Bigman na Juma Hussein wa Stand United, aliiongoza timu yake kushinda michezo minne kati ya mitano iliyocheza mwezi huo.

DUBE MCHEZAJI BORA FEBRUARI LIGI KUU YA NBC

MSHAMBULIAJI wa timu ya Young Africans (Yanga) ya Dar es Salaam, Prince Dube, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Februari wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2024/25, huku Miloud Hamdi pia wa Yanga akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.

Dube alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Aziz Ki wa Yanga na Selemani Bwenzi wa KenGold, alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo saba ambayo Yanga ilicheza mwezi huo na kufunga mabao matano na kuhusika na mengine matano kwa dakika 562 alizocheza. Yanga ilishinda michezo sita na kutoka sare mmoja.

Kwa upande wa Hamdi aliyeingia fainali katika mchakato huo na Fadlu Davids wa Simba na Fred Minziro wa Pamba Jiji, aliiongoza Yanga kushinda michezo minne na sare moja, ambapo kwa mwezi huo Yanga ilicheza michezo saba.

Hamdi aliiongoza Yanga ilipotoka suluhu na JKT Tanzania, kisha ikazifunga KMC mabao 1-6, Singida Black Stars (2-1), Mashujaa (0-5) na Pamba Jiji (0-3). Mechi nyingine ambazo Yanga ilishinda mwezi huo lakini haikuwa chini ya Hamdi ni dhidi ya KenGold (6-1) na dhidi ya Kagera Sugar (4-0).

Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Dar es Salaam, Ashraf Omar, kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Februari kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

NBC CHAMPIONSHIP ‘BOLI’ LINACHEZWA.

TAYARI michezo 176 kati ya 240 ya Ligi ya Championship ya NBC imeshachezwa huku ushindani mkubwa ukionekana baina ya timu zinazoshiriki ligi hiyo ambayo Mtibwa Sugar ipo kileleni kwasasa ikiwa na alama zake 54 baada ya michezo 22 ya Ligi hiyo.

Kwa upande wa nafasi nne za juu ushindani ni mkubwa huku kila timu zikitafuta nafasi ya kupanda Ligi Kuu ya NBC moja kwa moja ambapo nafasi hizo nne za juu zinashikiliwa na Mtibwa akiwa nafasi ya kwanza na alama 54, Mbeya City ikiwa nafasi ya pili ikiwa na alama 46 sawa na Stand United iliyo nafasi ya tatu wakitofautiana kwenye mabao ya kufunga na kufungwa na nafasi ya nne ikishikiliwa na Geita Gold yenye alama 45.

Cosmopolitan, African Sports, Transit Camp na Biashara United zinaendelea kupambana kwenye nafasi nne za chini kujinasua kutokushuka daraja kwa msimu huu, Biashara United inaburuza mkia kwenye Ligi hiyo ikiwa na alama nne pekee, Transit Camp ipo nafasi ya 15 ikiwa na alama 11, African Sports inashika nafasi ya 14 ikiwa na alama 14 wakati Cosmopolitan ikiwa na alama 15 kwenye nafasi ya 13.

Timu mbili za juu kwenye msimamo zinapanda moja kwa moja kwenye Ligi Kuu ya NBC huku mbili za mwisho zikishuka moja kwa moja na kushiriki First League.