Category: STORY

KMC YAREJEA NYUMBANI KIBABE LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya KMC ya Dar es Salaam imefanikiwa kupata ushindi wa kwanza nyumbani dhidi ya Singida Black Stars kwa mabao 2-0 tangu kurejea kwa Ligi Kuu ya NBC iliyokuwa kwenye mapumziko mafupi.

Mabao mawili yaliyofungwa na Oscar Paulo kipindi cha kwanza yalitosha kuzamisha jahazi la Singida BS ambayo haijapata ushindi tangu kurejea kwa ligi hiyo.

KMC imefanikiwa kupata ushindi baada ya kupoteza mchezo uliopita ugenini dhidi ya Coastal Union kwa mabao 2-1 huku Singida ikilazimishwa sare ya 2-2 mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar.

KMC imefikisha alama 22 na ‘kukwea’ hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC huku Singida BS ikisalia nafasi ya nne na alama 31.

JKT, YOUNG AFRICANS  HAKUNA MBABE

LIGI Kuu ya NBC imezidi kushika kasi   JKT Tanzania iliwakaribisha timu ya Young Africans katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo mkoani Dar es Salaam jana.

Mchezo huo ulipigwa majira ya saa kumi na robo ambapo timu zote zilionekana kuzitaka alama zote ili ziweze kuwa katika  nafasi nzuri

Yanga walizitaka alama hizo ili waweze kuendelea kukaa kileleni huku JKT ikitamani  kujiweka katika nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Mpaka dakika 45 zinatamatika timu zote zilienda mapumziko bila ya kufungana hivyo kuwapa kazi ngumu makocha wao kujiuliza nini cha kufanya kwa kipindi cha pili ili kuweza kupata matokeo.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na timu zote zilifanya mabadiliko ya vikosi mara kwa mara ili kuweza kuona kama wanaweza kushinda mchezo huo.

Mpaka dakika 90 za mchezo huo zinatamatika sio wenyeji JKT Tanzania ama wageni Young Africans walioambulia goli lolote hivyo mchezo kumalizika kwa sare pacha ya kutokufungana ikiwa ni msimu wa pili kwa Young Africans kutokushinda katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo kwa michezo mitatu ambapo Mashujaa watawakaribisha Coastal  Union katika uwanja wa Lake Tanganyika,Simba ikiumana na Tanzania Prisons uwanja wa KMC Complex na Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Tabora United uwanjani Kaitaba mkoani Kagera.

PAMBA JIJI YAWADUWAZA AZAM, NAMUNGO YATOSHANA NGUVU NA DODOMA JIJI.

LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana kwa michezo miwili ambapo Pamba Jiji iliwakaribisha timu ya Azam katika mchezo uliochezwa uwanja wa CCM Kirumba Mwanza na Namungo iliwakaribisha Dodoma Jiji uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.

Mchezo wa Pamba Jiji ulianza majira ya saa kumi alasiri ambapo timu zote zilikuwa zikishambuliana kwa kasi na kuonyesha nia ya kuzitaka alama zote tatu mhimu za mchezo huo hivyo kwenda mapumziko wakiwa suluhu ya kutokufungana bao lolote.

Kipindi cha pili kilianza ambapo Pamba Jiji ilionekana kurejea kwa kasi zaidi huku ikizima mashambulizi yaliyokuwa wakianzishwa na Azam mara kwa mara na dakika ya 86 ya mchezo huo Pamba Jiji walipata bao kupitia mchezaji wao Deus Kaseke ambae aliingia dakika chache kabla ya kufunga bao hilo pekee lililopeleka kilio kwa ‘matajiri wa jiji la Dar es Salaam’ baada ya mchezo kuisha kwa Pamba 1-0.

Mchezo wa pili ulianza majira ya saa moja jioni ambapo Namungo ‘Wauaji wa Kusini’ iliwakaribisha Dodoma Jiji huku timu ya Namungo ikionekana kushambulia zaidi.

Iliwachukua dakika 21 timu ya Dodoma Jiji kupitia mchezaji wao Paul Peter kufungua ukurasa wa mabao na dakika kumi mbele Apolo Otieno aliiongezea bao la pili Dodoma Jiji na dakika ya 44 Namungo  walipata bao kupitia mchezaji wao Pius Buswita hivyo kwenda mapumziko ubao ukisoma 1-2.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa Namungo wakisaka bao la kusawazisha huku Dodoma Jiji wakisaka bao zaidi, dakika ya 56 ya mchezo huo mchezaji wa Namungo Erasto Nyoni aliiongezea timu yake bao la pili kupitia mkwaju wa penati  hivyo matokeo kuwa 2-2 mpaka mwisho wa mchezo.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo katika viwanja vitatu ambapo KenGold watawakaribisha Fountain Gate katika uwanja  wa Sokoine jijini Mbeya na mkoani Dar es Salaam KMC watawakaribisha Singida Black Stars huku JKT wakiwakaribisha Young Africans uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.

SILLAH AWALIZA ‘WATOTO WA MJINI’ LIGI KUU NBC

MCHEZAJI wa Azam Gibril Sillah amepeleka kilio kwa KMC ‘Watoto wa mjini’ baada ya kufunga mabao mawili kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Azam ilizitafuta kwa nguvu alama tatu ikicheza kwa kasi huku KMC  ikicheza kwa tahadhari kubwa na kujilinda ingawa Ilimchukua dakika 26 mchezaji wa Azam Gibril Sillah kufungua akaunti ya mabao na hadi mapumziko Azam ilienda kifua mbele ikiongoza kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku KMC ikionekana kutaka kusawazisha kwa kuwashambulia Azam ambao muda wote waliziba njia na mipango ya KMC na dakika ya 65 Sillah alirejea tena ‘kambani’  na kufanya ubao kusomeka 2-0.

Mpaka mchezo huo unatamatika Azam ilifanikiwa kubakisha alama tatu muhimu za mchezo huo wakiendelea kuwa nafasi ya tatu na alama 39 katika msimamo huo.

Matokeo hayo yanaifanya Azam kupata ushindi kwenye michezo yote miwili iliyocheza dhidi ya KMC msimu huu baada ya mzunguko wa kwanza kuifunga mabao 4-0 kwenye uwanja wa KMC Complex, Dar.

LIGI KUU YA NBC

LIGI KUU YA NBC KUCHEZWA ARUSHA, SINGIDA LEO.

LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo Februari 7, 2025 kwa michezo miwili kuchezwa kwenye mikoa ya Arusha na Singida kuanzia saa 10:00 Alasiri.

Mkoani Arusha Coastal Union itaikaribisha JKT Tanzania kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid huku ikiingia kwenye mchezo huu ikishika nafasi ya 11 ikikusanya alama 18 kwenye michezo 16 na JKT Tanzania ikishika nafasi ya nane baada ya kukusanya alama 19 wakiwa na tofauti ya alama moja (1) pekee kati yao.

Mkoani Singida, timu ya Singida Black Stars itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar ya mkoani Kagera kwenye uwanja wa CCM Liti huku mara ya mwisho timu hizi kukutana Agosti 24, 2024 mkoani Kagera, Singida Black Stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0 likifungwa na Mchezaji Anthony Tra Bi dakika ya 90+3 ya mchezo huo.

Michezo hii miwili inakamilisha michezo ya mzunguko wa 17 wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 ambapo mpaka sasa timu ya Young Africans ikishika usukani na alama 45 huku Kengold ikiburuza mkia ikiwa na alama sita pekee.