Category: STORY

MWALIMU KINARA WA TUZO LIGI YA NBC.

Mchezaji wa Fountain Gate Seleman Mwalimu ameendelea kuwa mwiba kwa mabeki wa timu za Ligi Kuu ya NBC kutokana na kufunga mabao sita hivyo kuwa mshambuliaji hatari zaidi awapo langoni mwa mpinzani.

Licha ya kuongoza kwa idadi kubwa ya mabao pia Mwalimu anaongoza kuwa na tuzo nyingi kuliko mchezaji yoyote wa Ligi hiyo baada ya kufikisha tuzo tano.

Mwalimu amefanikiwa kuwa mchezaji bora wa michezo minne tofauti ya Fountain Gate dhidi ya KMC, Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na KenGold.

Aidha Mwalimu alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi septemba hivyo kumfanya kuwa mchezaji mwenye tuzo tano katika Ligi Kuu ya NBC.

AHOUA HAKAMATIKI LIGI KUU NBC

Kiungo wa Simba Jean Ahoua amekuwa tishio katika Ligi Kuu ya NBC baada ya kuchangia mabao 9 kati ya 21 ambayo timu yake ya Simba imefunga katika mizunguko 10 iliyocheza.

Ahoua ambaye amesajiliwa na Simba mwanzoni mwa msimu huu amefanikiwa kufunga mabao matano katika Ligi Kuu na kuhusika katika pasi nne zilizozaa mabao.

Mchezaji huyo pia amefanikiwa kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Agosti na pia amechukua tuzo mbili za mchezaji bora wa mechi kati ya Simba na Fountain Gate baada ya kufunga bao moja na kutoa pasi ya mwisho moja na mchezo kati ya Simba na KMC alipofunga mabao mawili hivyo kuchangia ushindi wa mabao manne ilioupata timu yake.

Ligi Kuu ya NBC inazidi kushika kasi ambapo mpaka sasa timu nyingi zimekuwa zikileta ushindani na upinzani mgumu jambo linalodhihirisha ubora wa Ligi hii

YANGA KUJIULIZA KWA TABORA LEO.

BAADA ya kupoteza dhidi ya Azam, leo timu ya Yanga inashuka uwanjani kuikaribisha Tabora United ya Tabora saa 12:00 jioni kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar.

Yanga iliyopoteza mchezo uliopita nyumbani leo itakuwa tena mwenyeji wa Tabora iliyopata ushindi kwenye mchezo wake uliopita dhidi ya Mashujaa kwa bao 1-0.

Yanga itajaribu kupata ushindi leo ili kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kupoteza nafasi hiyo inayoshikiliwa na Simba kwa sasa baada ya kushinda mchezo wa jana dhidi ya KMC.

Hadi sasa Yanga imefungwa mchezo mmoja na bao moja pekee ikiwa timu ya pili kwa wastani mzuri wa mabao (12) nyuma ya Simba yenye (18).

SIMBA YAITOLEA UVIVU KMC.

LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana kwa mchezo mmoja uliochezwa katika Uwanja wa KMC, Dar es Salaam Simba waliwakaribisha KMC majira ya saa 10 alasiri na kufanikiwa kushinda 4-0.

Awesu Awesu alifungua ukurasa wa mabao dakika 25 ya mchezo huo baada ya kupokea mpira kutoka kwa mshambuliaji wa timu hiyo Steven Mukwala hivyo kuiweka mbele timu yake ya Simba.

Dakika ya 38 ya mchezo Jean Ahoua alifanikiwa kuipatia timu yake bao la pili kwa mkwaju wa penati baada ya mchezaji wa KMC, Raheem Shomari kufanya faulo kwa Shomari Kapombe hivyo Simba kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0.

Baada ya mapumziko mchezo uliendelea kwa timu zote mbili kushambuliana kwa kasi na dakika ya 66 Edwin Balua alifanikiwa kuiongezea timu yake bao la tatu akipokea pasi kutoka kwa Valentin Nouma huku bao la mwisho likifungwa na Jean Ahoua dakika ya 69 ya mchezo huo na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea katika Uwanja wa Azam Complex ambapo Yanga watawakaribisha timu ya Tabora United mchezo utakaochezwa saa 12 jioni.

PAMBA JIJI YAONJA RAHA YA USHINDI, SIMBA, KMC HAPATOSHI LEO.

Ligi Kuu ya NBC jana iliendelea kwa mchezo mmoja uliochezwa katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara ambapo Fountain Gate waliwakaribisha timu ya Pamba Jiji kutoka Mwanza.

Iliwachukua dakika 28 Fountain Gate kufungua ukurasa wa mabao kupitia mchezaji wake Ellie Makono ambapo dakika ya 34 Pamba Jiji waliweka mzani sawa kwa kupata bao kupitia mchezaji wake James Mwashinga kabla ya kuongeza bao la pili katika dakika ya 45 ya mchezo huo kupitia mchezaji Salehe Masoud hivyo kwenda mapumziko wakiwa wanaongoza.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana na dakika ya 85 ya mchezo huo mchezaji Ally Ramadhan aliiongezea Pamba Jiji bao la 3 hivyo kuifanya timu hiyo kupata ushindi wao wa kwanza tangu kupanda Ligi kuu ya NBC huku wakiwa wamecheza michezo 11.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo mkoani Dar es Salaam ambapo timu ya Simba itakuwa mwenyeji wa KMC katika Uwanja wa KMC Complex, uliopo Mwenge majira ya alasiri.