Category: STORY

LIGI KUU YA NBC KUPIGWA MIKOA MITATU TOFAUTI LEO.

 

LIGI KUU ya NBC inaendelea leo kwa michezo mitatu katika mikoa mitatu tofauti baada ya kusimama kwa siku moja.

Mchezo wa kwanza utazikutanisha Tanzania Prisons dhidi ya Namungo katika uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya saa 8:00 Mchana.

Geita Gold watawaalika Singida FG katika uwanja wa Nyankumbu, Geita saa 10:00 alasiri.

Mchezo wa mwisho utapigwa saa 1:00 usiku Kagera Sugar dhidi ya Azam FC katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.

Kagera anaingia kwenye mchezo huu akiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa mabao matatu dhidi ya Simba huku Azam akiifunga JKT Tanzania kwa mabao 2-1 katika uwanja wa Azam Complex.

COASTAL, DODOMA HAZIKAMATIKI LIGI KUU YA NBC

 

LIGI Kuu ya NBC imeendelea Leo kwa Michezo miwili kuchezwa kwenye mikoa miwili tofauti.

Mchezo wa mapema saa 10:00 alasiri ulizikutanisha JKT Tanzania dhidi ya Coastal Union katika uwanja wa Azam Complex, Dar na kushuhudia Coastal Union akiibuka na Ushindi wa Bao moja lililofungwa na Maabad Maulid Dakika ya 87 .

Coastal Union imepanda hadi nafasi ya 6 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikifikisha jumla alama 19.

Mchezo wa pili ulizikutanisha Dodoma Jiji dhidi ya Ihefu katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma na kumalizika kwa Dodoma kuibuka na ushindi wa bao 1 lililofungwa na mchezaji Yasin Mgaza dakika 55 ya mchezo.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa mchezo nmoja kati ya Mtibwa Sugar na Mashujaa Saa 10:00 alasiri katika uwanja Manungu, Morogoro.

MKUTANO MKUU WA 10 TPLB WAFANYIKA DAR ES SALAAM

Mkutano mkuu wa 10 wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania umefanyika Disemba 8, 2023 kwenye ukumbi wa mikutano wa wa NSSF, Ilala na Mgeni Rasmi akiwa ni Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo nchini Mh. Damas Ndumbaro.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa soka akiwemo Katibu Mkuu Mtendaji wa (BMT) Neema Msitha na Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred.

Akifungua mkutano huo wa 10 mgeni rasmi, Mh Ndumbaro aliisisitiza Bodi ya Ligi na TFF kuendelea kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha ligi kuu inakuwa namba moja Afrika.

Alisema Katika miaka 10 Bodi ya Ligi imefanya mambo mengi mazuri, ikiwa ni pamoja na kutoa ligi katika nafasi ya 10 hadi hadi kuwa ligi ya 5 kwa ubora Afrika huku akiwataka kuweka mkakati wakuifanya iwe namba moja.

Aidha alisema ubora wa ligi kuu ndio umefanya hivi karibuni CAF ikatuamini na kutupatia uwenyeji kwenye ufunguzi wa mashindano mapya ya African Football Leagu na kuwataka watanzania na wadau wa soka kuwasifu, kujivunia pamoja na kuunga mkono utendaji na usimamizi bora kwenye sekta hiyo ya mpira wa miguu.

Kwa upande wa Afisa Mtendaji Mkuu Almasi Kasongo alisema kupitia mkutano huo wanaamini watakwenda kufikia maazimio yaliyopangwa kwa mwaka ujao kama ambavyo taratibu zao zilivyo za kuboresha kila mwaka.

alizitaka timu zote kuzingatia utekelezaji wa udhibiti na ukaguzi wa klabu (club licencing) huku akisisitiza timu hizo kusimamia maeneo yanayounda udhibiti na ukaguzi wa klabu (Club licencing) hasa katika kuimarisha uchumi wa klabu na kudhibiti madeni ambayo yamekuwa yakirudisha nyuma hadhi ya klabu na ligi kwa hatua ya Kitaifa na kimataifa.

Mkutano huo wa 10 wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ulihudhuliwa na viongozi mbalimbali kutoka TFF na Bodi ya ligi pamoja na viongozi waliowakilisha timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya NBC, Ligi ya NBC Championship na First League.

IHEFU, TANZANIA PRISONS KUKIWASHA LIGI KUU YA NBC.

TIMU za Ihefu na Tanzania Prisons zinashuka uwanjani leo kwenye mchezo pekee wa Ligi Kuu ya NBC utakaochezwa kwenye uwanja wa Highland Estates, Mbeya saa 10:00 alasiri.

Ihefu inashuka uwanjani ikiwa haijashinda katika michezo saba iliyopita ikikusanya alama tisa na kushika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Tanzania Prisons inaingia uwanjani ikiwa imeshinda mchezo uliopita nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji kwa bao 1-0 na kukusanya alama 10 huku ikishika nafasi ya 13 kwenye msimamo.

GEITA YATAMBA, KAGERA IKIBANWA LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya Geita Gold ya mkoani Geita imepata ushindi katika uwanja wa nyumbani wa Nyankumbu kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu baada ya kuifunga JKT Tanzania ya Dar es salaam bao 1-0.

Huu ni ushindi wa pili kwa Geita msimu huu unaowafanya kufikisha alama 10 katika nafasi ya 10 ikipoteza michezo minne na kutoa sare minne.

Kagera imeshindwa kutamba nyumbani dhidi ya KMC baada ya kulazimishwa sare ya bao moja kwenye uwanja wa nyumbani Kaitaba mkoani Kagera.

Bao namba 10 kwa KMC msimu huu lililofungwa na Waziri Junior kwenye mchezo wa leo limeifanya KMC kusalia nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na alama 16 huku bao la Kagera likifungwa na Deus Bukenya na kuwafanya Kagera kukaa nafasi ya saba ikiwa na alama 13.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena kesho Novemba 23, Tanzania Prisons ikiikaribisha Coastal union kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya saa 10:00 alasiri huku Namungo ikiwa mwenyeji wa Ihefu kwenye uwanja wa Majaliwa, Lindi saa 1:00 usiku.