LADHA ZA LIGI KUU NBC ZAREJEA YANGA WAKIWALIZA KAGERA SUGAR

Ladha za Ligi Kuu ya NBC zimerejea rasmi leo Februari 1 kwa mchezo mmoja uliochezwa uwanja wa KMC mkoani Dar es Salaam ambapo timu ya Yanga waliwakaribisha Kagera Sugar.

Mchezo ulianza majira ya saa kumi alasiri kwa timu zote kushambuliana kwa kasi huku Yanga wakionekana kuutawala mchezo.

Ilimchukua dakika 32 mshambuliaji wa Yanga Clement Mzize kufungua akaunti ya mabao na kuifanya timu yake kwenda kifua mbele mapumziko licha ya kiungo wa timu hiyo Aziz Ki kushindwa kufunga mkwaju wa penati waliopata timu yake.

Kipindi cha pili kilianza ambapo dakika ya 60 Mudathir Yahya aliongeza bao la pili kwa Yanga huku wakionekana kuzidi kulisaka lango la mpinzani wao na kutaka mabao zaidi.

Pacome Zouzoua aliongeza bao la tatu kwa mkwaju wa penati baada ya mchezaji wa Kagera Sugar kumfanyia madhambi Max Nzengeli  kabla ya Kennedy Musonda kufunga bao la nne hivyo Yanga kufikisha alama 42 wakiwa wamefunga mabao 36 na wakiruhusu 6.Mchezaji wa Yanga Max Nzegeli amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Ladha za Ligi Kuu ya  NBC zitaendelea kesho mkoani Tabora ambapo timu ya Tabora United watawakaribisha Simba saa kumi alasiri katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

One comment

Join the Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *