Category: STORY

YOUNG AFRICANS YAILIZA FOUNTAIN GATE.

UTAMU wa Ligi  Kuu ya NBC unazidi kukolea ambapo jana katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara  timu ya Fountain Gate iliikaribisha timu ya Young Africans katika mchezo uliochezwa majira ya saa kumi jioni.

Katika mchezo huo timu zote zilianza kucheza kuwa kasi ili kuweza kupata alama tatu muhimu ambapo iliwachukua dakika 38 timu ya Young African kufungua ukurasa wa abao kupitia mshambuliaji wao Clement Mzize huku dakika ya 43 Kiungo wa timu hiyo Aziz Ki akiongezea bao la pili hivyo kuwafanya kwenda mapumziko wakiwa wanaongoza 0-2.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Fountain Gate wakitafuta nafasi ya kusawazisha ambapo hatahivyo ndoto zao zilizimwa baada ya dakika ya 70 Clement Mzize kuongeza bao la tatu huku Clatous Chama akiweka bao la nne dakika ya 89 hivyo mchezo kutamatika kwa matokeo ya 0-4.

Mchezaji wa Young Africans,Clement Mzize alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.

 

KENGOLD YAAGA RASMI LIGI KUU YA NBC.

TIMU ya KenGold imekuwa timu ya kwanza kuaga Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/25 na kushuka daraja baada ya kupoteza jana kwa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

KenGold iliyokuwa bingwa wa Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2023/24 na kufanikiwa kupanda ligi kuu imedumu kwa msimu mmoja pekee na kurejea tena kwenye ligi ya Championship.

Hadi sasa mabingwa hao waliopita wa Championship wameshinda michezo mitatu pekee ya Ligi Kuu ya NBC wakifungwa 17, huku wakitoka sare michezo saba na kukusanya alama 16 pekee huku ikisalia michezo mitatu kukamilika kwa msimu.

KenGold hadi sasa imeruhusu mabao 50 na kufunga 22 huku ikiwa timu ya pili kuruhusu mabao mengi nyuma ya Fountain Gate ya Manyara iliyofungwa mabao 51 hadi sasa.

COASTAL UNION YATAMBA MKWAKWANI.

Ligi Kuu ya NBC ilitimua vumbi tena kwenye uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga majira saa moja jioni ambapo ulizikutanisha timu ya Coastal union na Kengold na Coastal kushinda 2-1.

Timu zote zilikuwa na shauku ya kupata alama tatu muhimu na hasa Kengold ambayo ipo nafasi ya mwisho katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC na ushindi pekee ungeweka  matumaini yao ya kusalia ligi kuu.

Dakika ya 20 Bakari Msimu wa Coastal Union aliipatia bao la kwanza timu yake na kuamsha mashabiki kwa shangwe na dakika ya 37 mchezaji Amara Bagayoko alipigilia msumari wa pili na kuzima matumaini ya KenGold kusalia ligi kuu.

Dakika ya 39 zikiwa zimesalia dakika 6 kipindi cha kwanza kutamatika Kengold  ilipata bao pekee lililofungwa na Sadalah Lipangile hivyo mchezo kumalizika 2-1.

Ushindi huo umeiweka Coastal union nafasi ya 8 na alama 31 huku Kengold ikiwa nafasi ya 16 ambayo ni ya mwisho ikiwa na alama 16 na kushuka daraja rasmi.

MAFUNZO YA ‘VAR’ YAFUNGWA DAR ES SALAAM.

Kozi maalum ya Teknolojia ya Msaidizi wa Video (VAR) iliyofanyika kwa takribani siku 5 kwenye ukumbi wa uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam imefungwa rasmi Jana Aprili 18, 2025 ikijumisha waamuzi 20 kutoka Tanzania Bara na Visiwani ikiwa ni mwendelezo wa Kozi hiyo yenye jumla ya moduli 6 mpaka kutamatika.

Kozi hiyo ambayo ni sehemu ya mkakati wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhakikisha nchi inakuwa na waamuzi waliobobea kwenye matumizi ya teknolojia hiyo ya kisasa inayotumika kusaidia kutoa maamuzi sahihi uwanjani imefungwa rasmi Kwa awamu ya pili na Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa TFF Boniface Wambura ambaye pia ndiye msimamizi Mkuu wa Kozi hiyo inayowezeshwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Akizungumza baada ya kufunga rasmi awamu ya pili ya Kozi hiyo Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura aliwapongeza waamuzi waliomaliza mafunzo hayo na kuwataka kwenda kutumia vyema ujuzi walioupata kwa maendeleo ya soka la Tanzania.

Aidha Wambura alieleza kuwa Kozi hiyo ni muendelezo na kwamba TFF itaendelea kuwekeza kwenye teknolojia hiyo Kwa kutoa elimu Kwa waamuzi wengi zaidi na hata kuzalisha wakufunzi wazawa ili kuhakikisha usimamizi wa mechi nchini unaendana sawa na mabadiliko kulingana na wakati Kwa kufuata viwango vya kimataifa.

Ikumbukwe kozi hiyo ni hatua muhimu kuelekea maandalizi ya matumizi rasmi ya VAR katika mechi za ligi kuu ya NBC na mashindano mbalimbali yatakayofanyika ndani ya Tanzania.

MTIBWA KUREJEA LIGIKUU

ALAMA TANO KUIREJESHA MTIBWA LIGI KUU YA NBC.

VINARA wa Ligi ya Championship ya NBC Mtibwa Sugar inahitaji alama tano pekee kujihakikishia nafasi ya kurejea Ligi Kuu ya NBC kwa Mara nyengine tena msimu wa 2025/2026.

Mtibwa Sugar imekusanya jumla ya alama 63 kwenye michezo 26 ya Ligi ya Championship ya NBC ambapo alama tano zitamfanya kufikisha alama 68 huku ikiwa timu moja pekee yenye uwezo wa kufikia alama hizo (Mbeya City).

Ikumbukwe timu mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC zinapanda moja kwa moja Ligi Kuu ya NBC.

Timu zinazoshika nafasi ya tatu na nne kwenye Ligi ya Championship ya NBC zinacheza mchezo wa mtoano kumtafuta mshindi mmoja wa kucheza mchezo wa mtoano wa kupanda (Promotion PlayOff) kwa timu ya Championship au kushuka (Relegation PlayOff) kwa timu ya Ligi Kuu.