Category: STORY

DABI YA MZIZIMA RASMI KWA MKAPA

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imebadili uwanja na muda wa kuanza kwa mchezo namba 167 wa Ligi Kuu ya NBC (Simba SC vs Azam FC) ambao ulipangwa kufanyika kwenye uwanja wa KMC Complex Februari 24, 2025 kuanzia saa 10:00 alasiri.

Mchezo huo sasa utafanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku Februari 24, 2025.

Sababu ya mabadiliko hayo ni kutoa nafasi kwa mashabiki wengi zaidi kuhudhuria mchezo huo ambao ni moja ya michezo mikubwa ya Ligi Kuu ya NBC inayovuta hisia za watu wengi.

Uwanja wa Benjamin Mkapa wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 60,000 umekuwa ukitumika kwa michezo mingi mikubwa na inayohusisha mashabiki wengi zaidi.

Klabu shiriki (Simba na Azam) pamoja na wadau wengine wa mchezo huo wametumiwa taarifa rasmi ya mabadiliko haya na maandalizi yake yanaendelea vizuri yakiwemo mazingatio ya kiusalama.

Bodi inawatakia wadau wote maandalizi mema ya mchezo huo maarufu kwa jina la ‘Mzizima Derby’.

TANZANIA PRISONS KUJIULIZA TABORA UNITED,JKT WAKIWAKARIBISHA KAGERA SUGAR LIGI KUU YA NBC.

MZUNGUKO wa 21 wa Ligi Kuu ya NBC unaanza leo rasmi ambapo michezo miwili itachezwa katika viwanja vya Sokoine jijini Mbeya na Meja Jenerali Isamuhyo mkoani Dar es Salaam.

Katika mchezo utakaochezwa majira ya saa nane mchana, timu ya Tanzania Prisons ‘wajelajela’ watakuwa wenyeji wa Tabora United ikiwa ni mchezo wa duru ya pili.

Tanzania Prisons ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imefunga mabao  11 na kuruhusu mabao 25 katika michezo 20 iliyocheza mpaka sasa na ikikusanya alama 17.

Tabora United ipo nafasi ya tano kwenye msimamo na imefunga mabao 24  na kuruhusu mabao 25 huku ikivuna alama 33 katika michezo 20 iliyocheza mpaka sasa.

Mchezo wa pili utachezwa uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo mbweni Dar es Salaam ‘wazee wa kichapo cha kizalendo’ wataikaribisha timu ya ‘wanankurukumbi’ kutoka misenyi Kagera.

JKT Tanzania ipo nafasi ya nane katika msimamo huku ikiwa imekusanya alama 23 ikifunga mabao 13 na kufungwa mabao 15.

Kagera Sugar ipo nafasi ya 15 ikiwa imekusanya alama 15 ikifunga mabao 16 ikiruhusu mabao 28 katika michezo 20 waliyocheza mpaka sasa.

 

 

CAMARA HASHIKIKI ‘HATI SAFI’ LIGI KUU NBC

AMESHINDIKANA ndivyo unavyoweza kusema kwa golikipa wa timu ya Simba, Moussa Camara ambae ni kinara wa ‘hati safi’ katika  michezo 19 Ligi Kuu ya NBC baada ya kuwaacha mbali wapinzani wake wa karibu.

Camara amesajiliwa na Simba katika dirisha kubwa la usajili  anaongoza kutokuruhusu mabao  ambapo mpaka sasa amekusanya hati safi 15 katika michezo ya Simba dhidi ya Tabora United nyumbani na ugenini,Fountain Gate,Prisons nyumbani na ugenini,Dodoma Jiji,Namungo nyumbani na ugenini,Azam,Mashujaa,JKT Tanzania,Pamba Jiji,Singida Black Stars,Ken Gold na KMC.

Pamoja na hati safi hizo Camara pia ndio golikipa ambaye ameruhusu mabao machache zaidi katika Ligi Kuu ya NBC ikiwa ni mabao 6 tu tangu msimu wa 2024/2025 uanze.

Golikipa huyo ameruhusu mabao katika mechi dhidi ya Coastal Union mawili,Young Africans,Kagera Sugar mawili na Fountain Gate mawili huku mabao mawili ni ya timu yake kujifunga dhidi ya Young African na dhidi ya Fountain Gate.

Patrick Munthali wa timu ya  Mashujaa ndie anaefuatia kwa kukusanya hati safi akiwa nazo 10 katika michezo 20 aliyocheza mpaka sasa huku timu yake ikiwa imeruhusu mabao 18.

Mlinda mlango wa Young Africans Djigui Diarra ndio wa tatu kwenye hati safi akiwa amekusanya hati tisa na kuruhusu mbao tisa katika michezo 20 ambayo timu yake imeshacheza.

Mohamed Mustafa wa  timu ya Azam  amekusanya hati tisa pia  wakiwa wameruhusu mabao tisa  sawa na Young Africans.

Yona Amos wa Pamba Jiji amekusanya hati safi nane  na  ameruhusu mabao 18,Metacha Mnata  wa Singida Black Stars  akiwa ameruhusu mabao 17 na  kukusanya hati safi 7 na Yakoub Suleiman wa JKT Tanzania akiwa na hati 7 na kufungwa mabao 15 katika michezo 20 waliyocheza mpaka sasa.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo kwa michezo miwili ya mzunguko wa 21 ambapo  timu ya Tanzania Prisons   itaikaribisha katika uwanja wa Sokoine timu ya Tabora United saa nane mchana na JKT Tanzania watakuwa wenyeji wa timu ya Kagera Sugar katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.

 

 

MZIZE,AHOUA HAPATOSHI VITA YA UFUNGAJI BORA

VITA ya ufungaji bora inazidi kushika kasi baada ya Kiungo wa Simba, Jean Ahoua, kufikisha mabao 10 sawa na mchambuliaji wa Young Africans, Clement Mzize, ambae ndio kinara wa mabao baada ya kutamatika mzunguko wa 20 wa Ligi Kuu ya NBC.

Ahoua ambae awali alikuwa na  mabao nane alifanikiwa kufunga mabao mawili ya penati  wakati wa mchezo wa Namungo dhidi ya Simba uliochezwa katika uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi licha ya Simba kuwa na mchezo mmoja wa kiporo dhidi ya Dodoma Jiji ambao uliahirishwa kutokana na timu hiyo kupata ajali.

Nafasi ya tatu ni mshambuliaji wa Young Africans,Prince Dube akiwa na mabao tisa mpaka sasa huku Elvis Rupia  wa Singida Black Stars na Leonel Ateba wa Simba wakiwa  nafasi ya nne na tano wakiwa na mabao manane kila mmoja.

Kwa upande wa kiungo wa Young Africans Pacome Zouzua na Peter Lwasa wa Kagera Sugar wanashikiria nafasi ya sita na saba huku wakiwa na mabao saba kila mmoja.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea kesho ambapo mzunguko wa 21 utaanza kwa michezo miwili ambapo JKT Tanzania watawakaribisha Kagera Sugar  uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbeni mkoani Dar es Salaam na Tanzania Prisons wakiwakaribisha Tabora United katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

 

LIGI KUU YA NBC KUTIMUA VUMBI LEO.

BAADA ya timu za KenGold, JKT Tanzania na Dodoma Jiji kuchukua alama tatu baada ya kushinda michezo yao hapo jana Ligi Kuu ya NBC inatarajiwa kuendelea tena leo kwa michezo mitatu itakayopigwa viwanja vitatu tofauti.

Mkoani Arusha timu ya Coastal Union iliyopoteza mchezo wake uliopita dhidi ya Pamba Jiji itakuwa mwenyeji wa Azam kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid saa 10:00 alasiri.

Azam inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mchezo uliopita nyumbani dhidi ya Mashujaa kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Zidane Sereri na Yoro Diaby.

Mkoani Kigoma timu ya Mashujaa iliyopoteza mchezo wake uliopita ugenini itakuwa mwenyeji wa timu ya Pamba Jiji ambayo imeshinda michezo mitatu mfululizo iliyopita bila kuruhusu bao katika michezo hiyo.

Mchezo wa mwisho utazikutanisha timu za Namungo itakayokuwa mwenyeji wa simba saa 12:30 jioni kwenye uwanja wa Mjaliwa, Lindi.

Timu ya Namungo inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusalia kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu ujao huku Simba ikihataji ushindi ili kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa msimu huu.