Category: STORY

JKT, PAMBA HAKUNA MBABE LIGI KUU YA NBC

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kwa mzunguko wa 14 kuchezwa michezo miwili iliyopigwa mkoani Dar es Salaam na Kagera.

Timu ya JKT Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Pamba Jiji ya Mwanza katika uwanja wa Isamuhyo, Dar es Salaam saa kumi alasiri na kumalizika kwa suluhu.

Katika mchezo huo golikipa wa Pamba Jiji Yona Amos alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kuokoa mashambulizi mengi yaliyolenga lango lake.

Mchezo mwingine ulichezwa uwanja wa Kaitaba, Kagera na kushuhudia Kagera Sugar ikiialika Namungo katika mchezo ulioisha kwa sare ya 1-1.

Dakika ya 64 ya mchezo huo Kagera Sugar walijibu mapigo kupitia mchezaji wao Peter Lwasa aliyesawazisha na kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare huku Erick Mwijage wa Kagera akitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Ligi Kuu itaendelea leo kwa michezo miwili Singida Black Stars watawakaribisha Dodoma Jiji saa nane mchana na KMC watawakaribisha Mashujaa saa kumi jioni kwenye uwanja wa KMC, Dar.

CHIKOLA BORA LIGI KUU YA NBC NOVEMBA

MSHAMBULIAJI wa Tabora United Offen Chikola amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Novemba wa Ligi Kuu ya NBC huku Kocha wa Azam Rachid Taoussi akichaguliwa kuwa kocha bora wa mwezi huo.

Chikola amewashinda Yacouba Sogne wa Tabora United na Moussa Camara wa Simba alioingia nao fainali za tuzo hizo baada ya kufunga mabao 3 katika dakika 351 alizocheza ndani ya mwezi huo.

Tabora ilizifunga Yanga mabao 1-3, Mashujaa 1-0, KMC 0-2, na ilitoka sare ya mabao 2-2 na Singida Black Stars hivyo kukusanya pointi 10.

Aidha Kocha wa Azam Rachid Taoussi amefanikiwa kuwa kocha Bora wa mwezi huo baada ya kuwashinda Davis Fadlu wa Simba na Hamad Ali wa JKT Tanzania baada ya kushinda michezo mitatu ambayo timu yake ilicheza ndani ya mwezi huo.

Azam walishinda dhidi ya Singida Black Stars 2-1, Yanga 0-1,na Kagera Sugar 1-0 hivyo kupanda hadi nafasi ya 2.

Kamati ya Tuzo pia imemchagua Meneja wa Uwanja wa Lake Tanganyika Shaaban Rajabu kuwa Meneja bora kutokana na usimamizi mzuri wa matukio ya michezo na masuala ya miundombinu.

Kwa upande wa Ligi ya Championship ya NBC kamati imemchagua mchezaji wa Mtibwa Sugar Anuary Jabir kuwa mchezaji bora wa Ligi hiyo baada ya kufunga mabao manne katika dakika 136 alizocheza akiwashinda Abdulaziz Shahame wa TMA na Naku Kazimoto wa Mbuni.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma amechaguliwa kuwa kocha bora wa ligi hiyo kwa mwezi novemba ambapo aliiongoza timu yake kushinda michezo minne na kufanikiwa kupanda kutoka nafasi ya pili mpaka ya kwanza katika msimamo wa ligi hiyo.

Continue reading “CHIKOLA BORA LIGI KUU YA NBC NOVEMBA”

AZAM YATAMBA NYUMBANI

LIGI Kuu ya NBC jana iliendelea mkoani Dar es salaam kwa mchezo mmoja uliochezwa Uwanja wa Azam Complex na kushuhudia Azam ikishinda 2-1 dhidi yaSingida Black Stars.

Kiungo wa Azam Feisal Salum alifungua ukurasa wa mabao kwa kufunga bao dakika ya 38 akipokea pasi kutoka kwa Idd Selemani Nado hivyo Azam kwenda mapumziko wakiwa wanaongoza kwa 1-0.

Kipindi cha pili mshambuliaji wa Azam Jhonie Blanco aliiongeza bao la pili timu yake dakika ya 57 ya mchezo huo akipokea pasi kutoka kwa Iddi Seleman .

Dakika ya 62 ya mshambuliaji wa Singida Black Stars Elvis Rupia alifunga bao hivyo kufanya ubao wa matokeo kusomeka 2-1 mpaka mwisho wa mchezo huo .

Mchezaji wa Azam Idd Seleman Nado alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa michezo miwili kati ya KMC na Tabora United kwenye uwanja wa KMC Complex, Dar na Fountain Gate dhidi ya JKT Tanzania kwenye uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara.

MOTO ULIWAKA LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC ilirejea kwa kasi mwishoni mwa wiki iliyopita kwa michezo iliyochezwa katika viwanja mbalimbali nchini.

Pamba Jiji ya Mwanza ilikuwa mwenyeji wa Simba katika Uwanja wa CCM Kirumba Novemba 22, na Simba kuondoka na alama zote tatu huku mshambuliaji wao Lionel Ateba akitajwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kufunga bao pekee la mchezo huo kwa mkwaju wa penati.

KenGold waliwakaribisha Coastal Union jumamosi ya Novemba 23 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kutoka sare ya 1-1 huku bao la Coastal lilifungwa na Abdallah Hassan ambaye pia alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo na Emmanuel Mpuka wa KenGold akisawazisha dakika ya 87 ya mchezo huo.

Mashujaa waliwakaribisha Namungo kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma ambapo Mashujaa waliibuka na ushindi wa bao moja lilifungwa na Abdurahman Mussa huku mchezaji wa Mashujaa Ibrahim Ame alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Azam waliwakaribisha Kagera Sugar jumamosi ya Novemba 23 katika Uwanja wa Azam Complex Dar es Salaam na Azam kuibuka na ushindi wa bao moja lililofungwa na Feisal Salum aliyeibuka mchezaji bora wa mchezo huo .

JKT Tanzania walicheza na Tanzania Prisons katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa bao moja lililofungwa na Hassan Kaparata ambaye pia aliyeibuka mchezaji bora wa mchezo huo .

Dodoma Jiji ilikuwa nyumbani kwenye uwanja wa Jamhuri kuwakaribisha KMC na Dodoma kushinda 2-1 huku mabao ya Dodoma yakifungwa na Iddy Kipagwile na Paul Peter ambaye pia alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo na bao la KMC likifungwa na Ali Shaban.

Ligi Kuu itaendelea leo kwa mchezo mmoja uliopaswa kuchezwa jana kati ya Tabora United na Singida Black Stars ambao ulioahirishwa kutokana na uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora kujaa maji baada ya mvua kubwa kunyesha mkoani Tabora.

LIGI KUU YA NBC KUREJEA.

LIGI namba sita kwa ubora barani Afrika Ligi Kuu ya NBC inarejea Novemba 22 baada ya mapumziko ya kalenda ya FIFA ambapo ijumaa Pamba Jiji ya Mwanza itakuwa mwenyeji wa Simba ya Dar es Salaam.

Pamba wamecheza michezo 11 mpaka sasa huku wakiwa wamevuna alama nane na wakiwa nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu.

Simba wamecheza michezo 10 wakiwa wamevuna alama 25 na kushika nafasi ya kwanza katika msimamo.

Mchezo huo utachezwa siku ya ijumaa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza majira ya saa 10 alasiri.